The House of Favourite Newspapers

Nay Kabla ya Kukamatwa Nilipewa Vitisho Vikali

Na Musa Mateja/CHAMPIONI/GPL
STAA wa Ngoma ya Wapo, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’, baada  ya juzi kuachiliwa huru ameibuka na kuweka wazi kuwa, tangu atoke studio wiki moja nyuma, hakuwai kusinzia kutokana na misukosuko aliyokuwa akikabiliana nayo kutoka kwa watu waliokuwa wakimpigia simu za vitisho.
Nay amekuwa na mfululizo wa kutoa nyimbo zenye ujumbe mkali kama ilivyo katika wimbo wake wa Salam Zao, Shika Adabu Yako, Pale Kati Patamu na huu wa sasa wa Wapo, ambao umezua gumzo kubwa nchini kiasi cha kumfanya hadi jana  Rais John Pombe Magufuli kudaiwa kumuita Ikulu kwa ajili ya kuzungumza naye.
Akizungumza na Championi Jumatano, Nay alisema kwamba, hajapata muda wa kulala na takribani wiki nzima sasa kwani tangu alipoachia wimbo huo amekuwa akipigiwa simu mbalimbali kutoka kwa watu asiowajua, ambapo mwanzo alipigiwa simu na kuambia aachane na wimbo huo kama anajipenda jambo ambalo alilipuuza kwa kujua ni watu tu wanamchezea akili zake.
“Kwa kifupi sijalala sasa ni wiki, maana simu ambazo nimekuwa nikizipata juu ya wimbo huu hakika kama nisingekuwa mtu mwenye misimamo yangu basi ningeweze kufa na presha, lakini pia utaona nimemaliza tu kufanya ngoma hii, nikaenda Morogoro kwa ajili ya shoo na nilipokuwa kule ndiyo nilikamatwa na kusafirishwa hadi Dar kwa ajili ya kesi hii.
“Hadi hapo utaona sijalala kwa muda ila tu nimshukuru rais na waziri mwenye dhamana ya sanaa yetu kwa kuliona na kuamua kuachia huru wimbo wangu, maana baada ya kukamatwa nilijua kwa vyovyote ningefungiwa na kama si kufungiwa basi ningeingia kwenye malumbano makubwa na serikali yangu.
“Kwa kuwa muziki ndiyo uchumi mkubwa wa kwanza kwangu, hivyo malumbano yangekuja tu kutokana na kudai uhuru wa mawazo yangu.
“Ningependa tu kwa sasa nisiliongelee sana hili kwa kuwa wakuu wameliona na kulifanyia kazi ila nimelala sana kwenye sakafu hivyo ninahitaji kupumzika, ili niende kuonana na Waziri Harisson Mwakyembe kule Dodoma ambapo ameniita,” alisema Nay wa Mitego.

Comments are closed.