NBC Kwenye Kongamano la Kigoda cha Mwl. Nyerere; JK, Pinda Ndani ya Nyumba
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeshiriki kikamilifu kwenye uzinduzi wa Kongamano la 13 la Kigoda Cha Mwalimu Nyerere uliofanyika leo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Kongamano hilo la siku tatu limezinduliwa na Mkuu wa Chuo hicho, Rais Mstaafu wa Awamu ya nne Mh Jakaya Mrisho Kikwete, ambae aliongoza viongozi mbalimbali wa kisiasa, kitaaluma na kiserikali akiwemo Waziri Mkuu mstaafu Mh Mizengo Pinda.
Mbali na kuwa mmoja wa wadhamini muhimu katika kongamano hilo, Benki ya NBC kupitia tawi lake la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliweza kuandaa banda maalum kwa ajili ya kutoa huduma zake kwa washiriki wa kongamano hilo sambamba na kushiriki katika kongamano hilo.
“Benki ya NBC tunatambua mchango na farsafa za Hayati Mwalimu Julius Nyerere si tu kitaifa bali pia katika uanzishwaji wa benki hii. Hii imekuwa ni moja ya sababu muhimu kabisa ya sisi kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kufanikisha na kushiriki katika masuala yote yanayohusiana na Hayati Mwalimu Julius Nyerere likiwemo Kongamano hili muhimu,’’ alisema Bi Anne Mwaisaka, Meneja wa Benki ya NBC Tawi la chuo hicho.