The House of Favourite Newspapers

Nchi Gani Iliwahi Kupigwa Mnada Sababu ya Mkopo? – Video

0

MBUNGE wa Kawe na Askofu Mkuu wa Makanisa ya Ufufuo, Dkt. Josephat Gwajima amemshauri Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai ajiuzulu wadhifa wake huo ili awaachie watu wengine waendeshe muhimili huo muhimu kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania.

 

Gwajima ameyasema hayo leo, Januari 6, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya New Africa jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa kauli alizozitoa spika huyo, zinakwenda kuwagawa wabunge ambao wengi wanamuunga Rais Samia, jambo linaloweza kumpa ugumu katika kusimamia shughuli za bunge. 

 

Kauli hiyo ya Gwajima inakuja kufuatia kitendo cha Ndugai cha kupinga mkopo wa shilingi Trilioni 1.3 uliokopwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

 

“Awamu ya sita sio ya kwanza kukopa, wakati Mwl. Nyerere anamaliza muda wake kulikuwa na deni la dola mil. 9,998, Mwinyi dola mil. 5,370, Mkapa alikuta deni la Tsh tril 9.95, Kikwete Tsh tril 33.3, Magufuli ameacha deni la Tsh tril 56.15, kwa nini mama abebeshwe tril 70?”

“Mhe. Ndugai alichokifanya ni kumtaja Mama (Rais Samia) kana kwamba yeye ndiye amekopa binafsi, Rais anapokopa hakopi mtu, inakopa nchi na inalipa nchi sio mtu, Mhe. Ndugai alisema ‘Mama juzijuzi amekopa Tsh trl 1.3’ hii ni kufanya mambo ya Kitaifa kuwa binafsi.

 

“Ndugai anambebesha Mama (Rais Samia) madeni yote utadhani yeye ndiye amekopa Tsh tril 70 wakati madeni mengi ameyarithi kutoka kwa watangulizi wake. Mhe. Rais Samia amekopa kiasi kidogo tu ndani ya huo muda ambao amekuwa madarakani.

“Ninaanza ku-note nia ya Mhe. Spika haikuwa nzuri, akasema ‘…nyie wenyewe mtaamua 2025 kama mtaleta mwingine..’ Mkuu wa Muhimili wa Bunge na mwanachama wa CCM anaweza kusema vile wakati anajua mila za CCM, Rais akipitishwa na chama anakaa miaka 5.

 

“Ni nchi gani iliwahi kupigwa mnada kwa sababu ya mkopo? Hii ni kugombanisha Mhe. Rais na wananchi… Mnada maana yake wanakuja Wachina, Wakorea, Wajapani, Wamarekani wanauliza… ‘Dodoma shilingi ngapi, Mwanza shilingi ngapi…, wananchi wanachonganishwa kumchukia Rais.

“Spika anawezaje kusema hivyo, inanipa picha kuwa Spika huenda ana mtu wake ama anacho anachokiwaza. Watu watahoji kwa nini leo Gwajima anamtetea Rais Samia, mimi hapa kipindi cha Bashite niliwalipua kwa sababu sipendi kuonewa wala kuona mtu anaonewa. Kwa hili nasema si sawasawa Mhe. Spika alichosema.

 

“Hii ni kuonyesha deni la taifa limesababishwa na Mama Samia, hii ni kumdhoofisha Mhe. Rais na juhudi zake za kutafuta pesa na kuliletea maendeleo Taifa letu. Haijawahi kutokea hapa nchini Mkuu wa Muhimili akatoka hadharani na kumpinga Rais kuhusu juhudi zake anazofanya,” amesema Ndugai.

 

Leave A Reply