The House of Favourite Newspapers

Ndoa na Shetani-7

0

ILIPOISHIA:
Nilirudi hadi chumbani kwangu na kuanza kulia kwa hali aliyokuwa nayo Abdul, kama kweli angekuwa ameumia kama alivyonieleza basi lazima hakutakuwa na mapenzi, hawezi kunisamehe.SASA ENDELEA…

Siku ile ilipita, hakukuwa na mtu wa kuja kunijulia hali mpaka siku ya pili nilipopata ruhusa ya kwenda nyumbani. Japo bado nilikuwa naumwa lakini nilikuwa na afadhali kubwa. Kabla ya kuondoka nilikwenda chumba alicholazwa Abdul, ajabu nilikuta shuka tupu kitandani. Wazo langu lilikimbilia kuwa Abdul amekufa na kuanza kulia kwa sauti ya juu iliyowavuta wauguzi kutaka kujua kulikoni.

“Vipi da’ Konso mbona unalia?”
“Jamani Abdul yupo wapi..au ameshakufa?”
“Hapana dada hajafa.”

“Sasa atakuwa wapi au amezidiwa sana yupo chumba cha wagonjwa mahututi?”
“Hapana hayupo chumba cha wagonjwa mahututi.”
“Sasa atakuwa wapi?”
“Ametolewa hospitali.”

“Amepona?”
“Hapana.”
“Kwa nini basi ametoka?”
“Amehamishwa hospitali na ndugu zake.”
“Ha! Kwa nini hamkuniambia?”

“Alikataa tusikuambie.”
Kauli ile ilinikata maini, niliongea kwa sauti ya kukata tamaa.
“Oooh! Maskini Konso mkosi gani huu?”

Sikuwa na jinsi zaidi ya kugeuka na kuondoka, nilikodi gari hadi nyumbani. Njiani nilikuwa na wazo nikifika nyumbani nikimkuta Bantu namfukuza kama mbwa aliyekula mayai. Nilipofika ajabu sikumkuta mtu, nilijiuliza Bantu atakuwa amekwenda wapi. Ilibidi nimuulize mlinzi wa getini.

“Eti Chodo, Bantu yupo wapi?”
“Leo siku ya pili sijamuona, mmh! Nakumbuka siku ya mwisho kama sikosei majira ya usiku aliniaga kuwa anatoka mara moja, lakini sikumuona kurudi mpaka leo hii.”
“Atakuwa amekwenda wapi?”
“Hata mimi nashangaa.”
“Ina maana ndiyo tabia yake kuondoka kwa muda wa siku nyingi ninapokuwa nimetoka?”

“Mmh! Ha…ha…pana yaani Bantu bwana siku hizi huwa hatoki, akitoka sana huja hapa kupiga stori kisha hurudi ndani hata chakula akinunua kama haupo huwa tunakula pamoja…Yaani Bantu mtu freshi sana.”

“Mm..mmh! Sasa atakuwa ameenda wapi, lakini Chodo utakuwa unajua vizuri kama Bantu rafiki yako lazima utajua yupo wapi.”
“Ukweli sijui mama, mara nyingi hata siku ambazo hutoka usiku huwa hachelewi kuja na akirudi huniletea mzinga wa pombe kali, husema siku moja moja hujichanganya viwanja..halafu alisema eti wewe ulimpiga mkwara juu ya wanawake.”

“Mmh!” Nilishusha pumzi ndefu na kuinama huku nikiwaza bila kupata majibu, nilijiuliza ina maana baada ya ugomvi ule Bantu kaamua kuondoka moja kwa moja.
Kwa nini basi asichukue nguo zake au ndiyo kaenda kwa mashoga zangu waliokuwa wakimfuatafuata kama fisi mwenye njaa.

“Chodo hebu nieleze vizuri ina maana Bantu alipoondoka juzi usiku hajarudi tena?”
“Ndiyo, mama.”
“Aliondoka saa ngapi?”
“Majira ya saa moja na nusu usiku.”
“Acha utani yaani saa moja juzi mpaka leo hajarudi?” nilishtuka kusikia vile.
“Ni kweli mama kwani kuna nini?”

“Mmh! Shughuli ipo,” nilisema huku nikiingia ndani.
“Mama kwani kuna nini?”
Mlinzi aliniuliza, sikumjibu niliingia ndani na kwenda moja kwa moja hadi kitandani na kujilaza chali macho nikiwa nimetizama juu kwa mawazo mazito niliwaza;

“Ina maana Bantu kitendo changu cha kumdanganya kimemuuma sana na kuona kila siku nilikuwa namdanganya? Mmh! Ni nani aliyemwambia mimi nipo kule, lazima kuna wachawi wanaoniwangia kila siku na kutaka kujua maisha yangu yanavyokwenda ili waharibu.
Itaendelea katika Gazeti la Risasi Jumamosi.

Leave A Reply