The House of Favourite Newspapers

Ndoto Nzuri ya Mb Dogg, Nancy Sumari!

0

MIAKA 13 iliyopita si karibu, ni umri wa mtu, lakini kuna kisa cha mastaa wawili ‘Hot’ Bongo, kimejirudia leo katika ndoto zangu.

Mwaka 2005 ilichipuka sura ya mrembo anayeitwa Nancy Sumari, huyu alifanikiwa kutwaa taji la Miss Tanzania mwaka huo.

 

Kama ilivyokuwa kwenye mashindano hayo, mshindi aliwakilisha nchi kwenye mashindano makubwa kabisa ya Dunia ya ulimbwende.

Nancy hakurudi mikono mitupu mwaka huo katika mashindano hayo, alinyakua taji la mrembo wa dunia kwa Afrika nzima.

 

Maana yake, ukitaja warembo wa Afrika kwa mwaka huo kwa levo ya dunia, wa kwanza alikuwa Nancy. Si vibaya kumzawadia angalau kwa kumpigia makofi.

Sijachelewa kukupakulia ndoto niliyoota, nitakusimulia tu, hivi ninavyorukaruka ndiyo naipika, cha msingi ukae mkao wa kula.

 

Waliokuwepo enzi hizo watakumbuka jinsi Nancy alivyorejea nchini kwa kishindo, mrembo yeye na miss maarufu ni yeye!

Alipotua Bongo alikuwa kama swala katupwa kwenye msitu wa simba, vigogo, mapedeshee enzi hizo ndiyo wanatamba, miruzi ya wakware ikamfuata mrembo huyo kila alipokatiza.

 

Kila mtu alikuwa ‘anataka’ hiyari ikawa kwa Nancy akupe au akunyime, kwangu mimi nakomea hapa maana huko ninakotaka kwenda hakufai.

Basi waliojaribu bahati yao sina orodha yao, waliopata na kukosa siwajui lakini kuna jamaa mmoja alivunja rekodi ya kutongoza.

 

Huyu si mwingine ni Mbwana Mohammed Ali ‘Mb Dogg’, jamaa alionekana kumzimikia sana mrembo huyo, alichokuwa anakitaka kwake sikijui, lakini ukweli alimpenda.

Kila alipokuwa akifanya intavyuu kwenye media, hakusita kumtaja Nancy kuwa ni chaguo lake. Kadiri siku zilivyokuwa zinakwenda, akaona mtoto halielewi somo lake, akaona “Ata” nimtungie wimbo kimwana huyu.

 

Msela akaketi gheto akaandika mistari mikali ya wimbo wa Ina Maana, ndani ya vesi akatupia mazima na jina la Nancy ili tu kumlainisha mtoto akunjue moyo.

Hii sasa ndiyo ndoto niliyoona leo, yamenirejea mashairi makali ya wimbo huo na kunifanya nijiulize Nancy mgumu kiasi hiki?

 

Maana sina data kwamba msela alikula au aliishia kunawa; ila kusema kweli wimbo huo ulihiti kinoma.

Enzi hizo Mb Dogg siyo huyu anayekula dona Sinza, jijini Dar es Salaam, alikuwa maarufu usipime.

 

Sasa chukua umaarufu wake enzi hizo Mb Dogg halafu sikiliza mistari hii:

“Ina maana hujui kama, nakupenda sana wee, jinsi ulivyoumbika duu, mi nakonda na we.”

Mashairi haya yalikuwa yanamhusu Nancy, siyo demu mwingine wa Uswahilini, ni Miss Dunia na Afrika, mtoto kisu ile mbaya mpaka mwenyewe anajiogopa.

 

Mpaka hapa huamini kwamba Ina Maana ulimhusu Nancy? Basi sikiliza mashairi ya wimbo huo ambao yalitaja jina lake moja kwa moja:

“Uzuri wa sura yako baby maa, umekufanya nikupe taji la Afrika. Nimejikaza nisiseme Nancy Sumari, eeh! Mi nashindwa nawe.

 

“Naposikia jina lako oh, natamani nikufate ulipo maa, huwa sili silali Nancy Sumari, hey! Mi nakonda na we, unafaa kuheshimika sio kwa taji waliokuvika, umzuri wa asili idara zote umekamilika.

“Umrefu kama twiga, kifuani kama miba,” huku ndiyo kuaprochi kwa msela Mb Dogg.”

 

Nilipomaliza ndoto zangu kuhusu kisa hiki na kufumbua macho, nikajikuta namuona Wema Sepetu, Hamisa Mobeto, Lynn, Poshy Queen na Tunda wakiwa mbele yangu.

Kilichofuata baada ya hapo nikajiuliza wangekuwa wao ndiyo akina Nancy wangeweza kuchomoa kwa mistari kama hii, wasiingie kingi?

 

Hili lilikuwa swali la kizushi tu lakini meseji yangu hapa ni kwamba, warembo wana kila sababu ya kuitambua thamani yao.

Kwenye mitandao ya kijamii nilikopita wakati naandaa makala haya kuhusu kisa cha Mb Dogg na Nancy, maoni ya wengi yalikuwa “Kama Nancy angekubali misifa akatoa, leo hii angekuwa wapi?”

 

Mimi nasema maisha ni maisha, lakini wengine wanasema mbele kunahitaji jicho kali kuliko nyuma na mahali ulipo.

Ni kweli wasanii wengi wamekuwa wakifanya uamuzi wa ajabu kwa sababu ya msukumo wa hapo ulipo, lakini wanashindwa kujua kuwa uamuzi wao wa leo ni matokeo yao ya kesho.

 

Siku hizi mrembo akisifiwa kidogo tu na msanii, basi anapagawa kiasi cha kutamani hata kuvua nguo ili amfurahishe msanii wa Bongo Fleva.

Muhimu kutambua kuwa kila mtu amekuja kuziishi ndoto zake, kama ambavyo Nancy alifanikiwa kujilinda na kuilinda statasi yake, warembo wengine wanatakiwa kuwa hivyo.

 

Siyo sifa kidogo tu basi tayari umeshaanguka; kumbuka utakapoinuka utakuta maisha yamekukimbia na kukuacha ukiwa mtupu.

Hii ni ndoto yangu tu ambayo nimeota ya nyuma na kuyalinganisha na ya leo. Katika Bongo hiihii, kuna watu ambao walikuwa wasanii, lakini leo ni waheshimiwa.

 

Angalia Prof Jay, Sugu na Jokate; wote hawa hawakufika hapo kwa bahati mbaya, bali walitazama mbali na macho yao yakaona fursa mbele, wakajiheshimu na sasa wanakula matunda ya heshima yao.

MAKALA: RICHARD MANYOTA

 

Leave A Reply