The House of Favourite Newspapers

Ndoto ya Amina Chifupa Iliyoyeyuka

0

Amina Chifupa akila kiapo bungeni-ALL PHOTOS BY JOHN BADI

Amina Chifupa.

Na Leonard Msigwa
KAMWE hakuna binadamu atakayeishi duniani milele, la hasha!  Kila nafsi lazima ionje mauti, kila moja kwa wakati wake. Aliyekuwa mwanamuziki mahiri hapa nchini, marehemu Ramadhan Ongala, maarufu kama ‘Dr Remmy’  aliwahi kutunga kibao maarufu kwa jina la Siku ya Kufa.

Moja ya mashairi yaliyomo ndani ya wimbo huo ni,  “Siku ya kufa wandugu kwaheri, siku ya kufa nyama yote ya udongo, siku ya kufa ujana wote unakwisha, siku ya kufa akili yote inapotea”.  Haya ni mashairi yanayoonesha baada ya kifo cha mwanadamu nini hufuata.

Jumanne ya tarehe 26 Juni mwaka 2007 Tanzania iligubikwa na simanzi kubwa baada ya kutangazwa Amina Chifupa amefariki dunia Hospitali ya Taifa ya Jeshi Lugalo (JWTZ). Ilikuwa ni simanzi kila kona nchini ila ukweli ulibaki kwamba hatimaye aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) hatunaye tena duniani.

Mwanadada huyo shupavu aliyejitoa mhanga kutaja vigogo nchini wanaohusika na biashara za uingizaji madawa ya kulevya hatimaye alifariki. Jambo la kusikitisha zaidi pia ndoto yake iliyeyuka, ilitoweka kwa kasi ya ajabu.   Hakuna tena mbunge shupavu kama yeye aliyesimama kusema kwa sauti namna gani anaumizwa na vigogo wanaoshiriki kuingiza madawa ya kulevya.

Watu wengi waliguswa sana na kifo chake  mmoja wao ni mimi wakati huo nikiwa mwanafunzi wa kidato cha tatu.  Nakumbuka mwalimu Mkemwa aliyekuwa mwalimu wangu wa somo la Kiswahili alikuja darasani kwetu akatuambia, “ama kweli watu wema na wazuri hawadumu…. Amina Chifupa amefariki dunia.”  Kauli yake ilileta simanzi na nakumbuka siku hiyo hakufundisha zaidi alitupa kazi ya kujisomea riwaya ya Watoto wa Mama Ntilie.

Ni miaka tisa sasa imepitika amekuwa nyama ya udongo, ni maneno mazito yanayoumiza na kutia majonzi moyoni ila ukweli utabaki Amina hatupo naye. Akiwa bado kijana wa miaka 26 uhai wake ulikatishwa kwa kile kilichoitwa maradhi ya mfadhaiko wa akili yaani “depression”.

Tujikumbushe kidogo kilichotokea kabla ya kifo chake; kwa mara ya kwanza taarifa za kuugua kwake zilitangazwa ndani ya Bunge la tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Spika wa wakati huo, Samuel Sita, akiwaomba wabunge kumwombea mbunge mwenzao.

Maradhi yake yalikuwa kama mzaha baada ya kugubikwa na habari za yeye kutalikiwa na mmewe Mohammed Mpakanjia (ambaye sasa ni marehemu) kwa kile kilichoelezwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mbunge wa wakati huo wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye kwa sasa ni mbunge wa Kigoma Mjini kupitia chama cha ACT-WAZALENDO.

Wadadisi wa mambo walihusisha ugonjwa wake wa kufadhaika akili ulitokana na shinikizo baada ya kupewa talaka na mmewe Mpakanjia, lakini baada ya kifo chake ripoti ya madaktari wa Lugalo ilionesha Amina alifariki kutokana na maradhi ya malaria na shinikizo la damu.

Kifo chake kilizua mjadala mkubwa katika jamii kila mmoja akizungumza lake, wapo walioenda mbali zaidi kwa kuhusisha kifo chake na harakati zake za kupambana na vigogo wanaojihusisha na uingizaji madawa ya kulevya nchini.

Historia yake, Amina alizaliwa Mei 20, 1981 jijini Dar es Salaam, alisoma Shule ya Msingi Ushindi, Mikocheni, Dar (1988-1994) kabla ya kujiunga na masomo ya sekondari ya kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Wasichana ya Kisutu, Dar (1995-1998). Elimu ya Juu ya Sekondari alisoma katika shule ya Makongo (1999-2001) kabla ya kujiunga na Chuo cha Uandishi wa Habari cha Royal (2001-2003) ambako alifuzu Diploma ya Uandishi wa Habari.

Mwaka 1999 alianza kazi ya utangazaji wa kituo cha redio cha Clouds FM cha jijini Dar na aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Mama Shughuli.  Katika siasa alikuwa kada wa CCM, Kamanda wa CCM wa Umoja wa Vijana katika tawi la Mikocheni A jijini Dar, Katibu wa Kamati ya Uchumi ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoa wa Dar, Mama Mlezi wa UVCCM na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) matawi ya Bunju na Mbagala.

Mwaka 2005 aliteuliwa kuwa mbunge akiwakilisha kundi la vijana kupitia CCM ambako alidumu na cheo hicho kwa muda mfupi na hatimaye 26 june 2007alifariki.

Alizikwa Juni 28, 2007 kijijini Lupembe Wilayani Njombe mkoa wa Iringa (sasa ni mkoani Njombe) karibu kabisa na eneo alilokuwa akiishi bibi yake. Mazishi yake yalihudhuriwa na watu wengi maarufu wakiiongozwa na Spika wa Bunge wa wakati huo Samwel Sita.

Kupambana na mihadarati

Amina Chifupa daima atakumbukwa kwa kujitolea kupambana na matajiri wanaofadhili au kujihusisha na uingizaji wa dawa za kulevya nchini. Alikuwa mbunge mdogo zaidi katika historia ya chombo hicho maalum kwa ajili ya kutunga sheria na kupitisha bajeti ya nchi yetu.
Alisimama kidete na kutamka bayana angewaweka hadharani vigogo wote wanaojihusisha na madawa ya kulevya, pia alienda mbali zaidi kwa kutamka hata kama angekuwa mume wake anahusika naye angemtaja.

Amina Chifupa hakumung’unya maneno, alikuwa jasiri kiasi ambacho alifikia uamuzi wa kuwasilisha majina ya vigogo waliokuwa wakifanya biashara ya “unga” makao makuu ya Jeshi la Polisi Jijini Dar es Salaam.

Aliamua kujitoa mhanga kutetea kizazi cha vijana kinachoteketea kwa kutumia madawa ya kulevya ilihali waoingiza wanazidi kuwa matajiri tishio na baadhi yao wana nguvu ya ushawishi katika nyanja mbalimbali serikalini.

Alikuwa ni hazina kwa taifa na mfano kwa vijana wenye umri mdogo kama wake kwamba inawezekana kujitoa pasipo woga kulitetea taifa na kuwaweka wazi wote wanaotumia utajiri wao, vyeo vyao kufanya au kuwezesha uhalifu hususani katika suala zima la madawa ya kulevya. Ametoa somo la kujiamini na kutekeleza kile alichokiamini pasipo kujali umri.

Alikuwa mwanasiasa chipukizi aliyejitolea kushughulikia kero za wananchi bila woga. Kwa muda mfupi aliotumikia nafasi yake kabla ya mauti yake, Amina alijitolea kushughulikia kero za wananchi bila kujali itikadi za vyama au maeneo.

Kwake yeye taifa lilikuwa kwanza vyama baadaye na hili lilijidhihirisha wakati wa kuuaga mwili wake jijini Dar ambapo katibu mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif, Mbunge wa Kibamba John Mnyika (wakati huo akiwa mbunge wa Ubungo na katibu wa vijana wa Chadema) walikuwa miongoni wa waombolezaji walioudhuria.  Hii ilidhihirisha alikuwa kipenzi cha wananchi wote bila kujali vyama.

Amina alifariki akiwa na msuguano na baadhi ya viongozi wa UVCCM ambao walituhumiwa  kumwona kuwa tishio  katika nafasi ya uenyekiti wa umoja huo ngazi ya taifa. Walimwona tishio kwa sababu moja kubwa zaidi kwamba alikuwa na uwezo wa kujenga hoja na kuisimamia pasipo woga wala kuyumbishwa.

AminaChifupa2xxx

Amina alifariki siku ya maadhimisho ya kilele cha madawa ya kulevya duniani. Hakika kila ifikapo tarehe 26 Juni kila mwaka jina la Amina haliishi kutajwa kwa kujitoa mhanga kuokoa vizazi vyetu vinavyoendelea kuteketea kutokana na kukithiri kwa biashara ya madawa ya kulevya nchini.

Ndoto iliyoyeyuka

Ni dhahiri ndoto ya Amina imeyeyuka kwa kasi ya ajabu, yale aliyokuwa akiyapigania na kupambana kuyaondoa leo yameota mizizi na kuwa sugu. Taifa linazidi kuteketea kwa vijana wengi zaidi kujiingiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya.

Sio siri tena vijana waliokuwa wakiyatumia na wanaoendelea kuyatumia, kwa mfano,   wanamuziki Ray C, Chid Benz na marehemu Banza Stone wote ni wahanga wakuu wa matumizi ya madawa ya kulevya, ndoto zao zinayeyuka taratibu huku baadhi yao wakiwa tayari wametangulia mbele za haki.

Hakuna mbadala wake

Ni dhahiri Amina alifariki na akili yake imeyeyuka inaonekana kuyeyuka, kwani  hakuna tena mbunge kijana aliyejitoa mhanga kama Amina kupambana na biashara hii haramu na kusimama kidete kulitetea taifa na kuhakikisha inawezekana kuwa na kizazi kisichoathirika na madawa ya kulevya.

Taifa linateketea kwa kuzalisha kizazi cha mateja, vijana wanazidi kuathirika zaidi kila siku. Ni wakati sasa serikali kumuenzi Amina Chifupa kwa kutekeleza ndoto yake, kuhakikisha wanaohusika na biashara ya kulevya wanawekwa hadharani, wanafilisiwa ikiwa ni pamoja na kuweka sheria kali za kuwabana wote wanaojihusisha na matumizi au biashara hii haramu.

Naamini ndoto ya Amina Chifupa ndiyo muarobaini wa tatizo hili sugu.  Kamwe biashara hii haramu haiwezi kumalizika kama tutaishia kuwakamata watumiaji wa chini kabisa na kuwaacha waingizaji wakuu wa madawa hayo nchini.

Ni miaka tisa tangu Amina Chifupa afariki, hakika kifo chake kinabaki kwenye kumbukumbu za Watanzania walio wengi hususani vijana. Tunamkumbuka sana Amina Chifupa kwa umahiri na ujasiri wake.
Sisi sote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea ambako tutaenda kuhesabiwa amali zetu.

Leave A Reply