The House of Favourite Newspapers

Ndugu Zangu Walinichukua Msukule-4

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Cha ajabu sasa, mimi mwenyewe nilikuwa nauona mwili ule kwenye jeneza ni mgomba wa ndizi lakini waombolezajieti wao walikuwa wanauona ni mwili wangu  na kila aliyeufikia alikuwa akizidisha kilio, hasa wanawake.

ENDELEA MWENYEWE…

Mara tu baada ya mazishi, wale wanawake walinichukua,  tukaanza kuondoka polepole kwenda kusikojulikana huku nyuma mama na ndugu wengine wakilia sana. Ilikuwa mwendo kidogo, tukafika sehemu moja kama kuna handaki.

Mwanamke mmoja kati ya wale akainama, akafunua jiwe kama mfuniko na kuweka pembeni, akaandika pale chini kwa mkono kisha akafunika. Nilibaini kwamba aliandika kama ishara kwamba kazi aliyotumwa au waliyotumwa waliimaliza.

Tulianza kutembea tena mpaka tukaenda kuingia kwenye handaki lenyewe ndani kabisa. Muda wote huo mawazo yangu yalikuwa ni juu ya wapi tunakwenda, kufanya nini, mimi ni nani na hali ya mama kule nyumbani baada ya mazishi yangu ikoje? Hayo ndiyo yalikuwa mawazo yangu.

Sehemu tuliyokuwa tunapita kulikuwa na ulinzi wa hali ya juu kiasi kwamba unaweza kufananisha na ikulu. Tuliwakuta watu wakikatwa ndimi na kulikuwa na mistari miwili imepangwa. Yaani kuna wale waliokuwa tayari wameshakatwa na wengine wakiwa kwenye foleni ya kwenda kukatwa. Ndipo nikawaona wale vijana wa kijijini kwetu waliofariki dunia kabla yangu.

Mimi nilijichanganya katika kundi la watu waliokuwa bado hawajakatwa ndimi. Mara, mkataji akasema amechoka mpaka kesho yake.

Kesho yake, mkataji aliamuru watu ambao bado wapange tena mstari. Mimi nikawa nimepanga kule kwa ajili ya kukatwa lakini mbele yangu kulikuwa na watu wengi, mkataji akasitisha tena akasema kwa siku ile ndimi alizokata zilikuwa zinatosha na tulikuwa wengi, hatupungui mia moja na watu walikuwa wakiongezeka kila siku.

Kutokana na uzoefu wangu wa kuhudhuria mikutano na matamasha mbalimbali duniani, kwa ngome zima kulikuwa na watu kama elfu tatu hadi nne na asilimia kubwa ya watu waliokuwemo mule ndani ni vijana wakifuatia watoto walio chini ya mwaka mmoja. Wazee walikuwa wachache sana.

Mimi baadaye niliunga ukaribu na yule kijana aliyekuwa fundi seremala aliyekufa kabla yangu, tukawa tunapanga njama za kutoroka kwenye ile ngome. Si kwa kuongea bali kwa vitendo kitu ambacho kilikuwa kigumu kutokana na ulinzi ulivyoimarishwa lakini tuliendelea kutafuta mbinu za namna ya kuondokana na tabu ile ila vitengo vya kazi ndiyo vilisababisha mipango yetu isitimie.

Kila mtu pale alikuwa na kitengo chake maalum cha kazi. Mimi nilikuwa kwenye kitengo cha kulima kwa sababu hata kwenye maisha yangu ya duniani ni mkulima hodari sana.

Basi, pale kengele ilipogongwa nilikimbilia jembe na kuanza safari ya kuelekea shambani. Tulilima bila kujua kama ni mchana au usiku na hata akili zetu zilikuwa tayari zimeshapumbazwa, tukawa tumezoea yale maisha ya kule kwani tulikuwa tukiongea kwa ishara.

Hayo ndiyo yakawa maisha mapya niliyoanza kuishi katika ulimwengu ule. Chakula kikuu kilikuwa pumba hizi wanazokula hata kuku na nyama zingine zisizo za kawaida, ikiwemo ya binadamu.

Muda wa chakula ulipowadia kila mtu alikimbilia bakuli lake kwa ajili ya kuwekewa chakula na kula bila kujali.

Kule kuko kama ambavyo serikali ya huku ilivyo kwa sababu kuna mbuga za wanyama, yaani kuna kila aina ya mnyama. Mfano, leo ikitolewa amri kuwa inatakiwa nyama ya nyati au swala basi watu wanakwenda mbugani kuwakamata wanyama hao.

Kuna wakati tulikuwa tunakula utumbo wa ndege aina ya cheche ambapo nilikuwa nikila nalazimika kwenda sehemu ambayo nitawakuta ndugu zangu. Hali hiyo ikawa inanifanya niende mpaka nyumbani au hata maeneo ya karibu na nyumbani ikawa kama ni maji ni lazima nikanywe sehemu ambayo watu wa nyumbani walikuwa wakichota au usiku nalazimika nikanywe maji kwenye mtungi wa nyumbani.

Nikila utumbo, nilikuwa najikuta narudi nyumbani kwa miguu tu lakini hakuna aliyekuwa akiniona zaidi ya kusikia sauti.

Waliposikia sauti yangu walikuwa wakipiga mayowe huku wakikimbia na kusema walinisikia kisha nilitoweka kimiujiza. Kuna siku nikiwa nakwenda nyumbani, niliwakuta marafiki zangu niliokuwa naishi nao mtaani wakiogelea mtoni, nikaanza kuwaita kwa majina.

Leave A Reply