The House of Favourite Newspapers

Nelly Muosha Magari wa Posta-27

1

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale Nelly akiwa na rafiki yake Ipyana wakielekea Posta kufanya kazi ya kuosha magari. Wakiwa kwenye daladala kijana huyo mpenda mademu alikuwa akimkazia macho mrembo aliyekuwa amesimama naye karibu baada ya kukosa siti. Je, kilifuatia nini? Songa mbele…

Kufuatia kumkazia sana macho, mrembo huyo akawa anaangalia pembeni kwa aibu jambo lililompa nguvu Nelly ya kuendelea kumtazama. Kila mrembo alipomtazama Nelly macho yao yaligongana mwishowe mtoto wa kike akaachia tabasamu.

Gari lilipofika Keko Fenicha, abiria waliokaa siti ya karibu yao waliteremka ndipo Nelly na yule mrembo wakaichangamkia siti hiyo, walipokaa tu Nelly akamsabahi yule dada.

“Mambo vipi mrembo?”

“Poa, ila wewe mkaka ni mchokozi sana, unajua ilibakia kidogo nicheke kwa ulivyokuwa ukinitazama,”  yule mrembo alimwambia Nelly.

“Utanisamehe, lakini na wewe si umezidi kuwa mrembo?” Nelly alimfagilia yule mrembo aliyeishia kutabasamu.

“Acha masihara yako, hivi kwa mfano warembo mia moja wakipanga mstari na mimi naweza kuwemo?” yule dada aliyeonekana anapenda sana stori alimwuliza Nelly.

“Siyo mia moja, hata wakiwa kumi wewe lazima uwe wa tatu,” Nelly alimfagilia.

Alipoelezwa hivyo, yule dada alicheka na kumwambia haya bwana kama ni kweli kisha akamwambia akumbuke kama angekuwa mrembo wala asingepanda daladala.

Nelly  alicheka na kumfahamisha kila kitu na wakati wake, hivyo awe na subira gari lake lilikuwa njiani kutoka Ulaya.

“Da! Wewe kaka una maneno sana, eti gari langu linakuja kutoka Ulaya haya bwana maneno yako yawe ya heri,” yule mrembo alimwambia Nelly, wakacheka.

Kwa kuwa asubuhi hiyo hakukuwa na foleni, kufumba na kufumbua walijikuta wapo Mnazi Mmoja, kama kawaida Nelly aliona atafanya kosa kubwa asipoomba namba ya simu ya yule mrembo.

“Unahitaji namba yangu ya nini?” mrembo alihoji.

“Si gari lako likifika nikupigie uje ulichukue!”  Nelly alimwambia.

Mrembo alicheka sana na kufuatia ucheshi wa sharobaro Nelly, akajikuta akimuomba kijana huyo ampatie simu yake ndipo Nelly alitoa akaiwasha na kumpatia, akaiandika na kumwambia asevu jina la shangazi.

“Unaitwa shangazi au unapenda niwe nakuita hivyo?” Nelly akamwuliza.

“Ndiyo jina langu, wengi wanapenda kuniita Aunt lakini wewe niite shangazi tu,”  yule mrembo alimwambia Nelly bila kujua asingemaliza muda mrefu bila kutafunwa na kijana huyo mpenda mademu wazuri.

“Sawa, lakini mimi nitakuwa nakuita Aunt,” Nelly alimwambia, wakacheka.

Gari lilipofika Posta, wote waliteremka ambapo yule mrembo alisema anakwenda Masaki ndiko alikokuwa akifanya kazi, walipoagana Ipyana akamfagilia Nelly kwa ushapu wake mpaka kuzoeana na yule mrembo kwa muda mfupi.

“We acha tu ndugu yangu tena mpaka namba yake kanipa,” Nelly alimwambia Ipyana.

Ipyana ambaye hakuwa mpenzi sana wa mambo ya wasichana akaishia kucheka, wakati marafiki hao wanaelekea kwenye ofisi za wizara moja ambayo Ipyana alikuwa akifanya ujasiriamali wa kuosha magari, Nelly alikumbuka  hakuzima simu baada ya kusevu namba ya yule mrembo, akaizima.

Alifanya hivyo kuhofia kupigiwa simu na Doreen ambaye hakutaka kabisa kuzungumza naye muda huo, kwa kuwa ofisi hizo za wizara hazikuwa mbali, waliwasili ndipo Nelly akashangazwa na jinsi wafanyakazi wa wizara hiyo na madereva walivyomchangamkia Ipyana.

“Dogo vipi hujambo?” dereva mmoja alimsalimia Ipyana.

Si huyo pekee, wafanyakazi mbalimbali walimsalimia kwa furaha na wengine walimwambia atayakuta magari yao sehemu aliyokuwa akioshea hivyo ayaoshe.

Ipyana aliwaambia sawa huku akimtambulisha Nelly kwamba alikuwa ndugu yake, alifanya hivyo mpaka kwa walinzi ambao kwa jinsi walivyomuamini dogo huyo hawakuwa na wasiwasi.

Ipyana na Nelly walipofika eneo la kazi, waliyakuta magari manne ya mabosi ambayo walipaswa kuyaosha, Ipyana alimuelekeza jinsi ya kufanya kazi hiyo Nelly.

Je, kitafuatia nini baada ya Nelly kuanza kazi ya kuosha magari huko Posta? Usikose wiki ijayo. Maoni nicheki kupitia namba hiyo hapo juu.

1 Comment
  1. Makongoro says

    mmmh cjui itakuaj…

Leave A Reply