The House of Favourite Newspapers

Nelly Muosha Magari wa Posta-35

0

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale dada Fatu alipomwomba Nelly  aende nyumbani kwake kumsaidia kazi ndipo Ipyana alimwuliza ni kazi gani akamwambia asubiri atakuja kuambiwa na Nelly. Je, ni kazi gani hiyo? Endelea na utamu huuu.

Baada ya Fatu aliyepania kutoka na Nelly siku hiyo ili kumburudisha kufuatia kukaa mufa mrefu bila kuletewa fujo za kikubwa kuondoka, vijana hao walipomaliza kuosha gari lake aina ya RAV 4 wakaenda kunywa chai.

“Nelly nilikwambia jana, Fatu katokea kukupenda naona sasa umeamini na leo hana kazi wala nini anataka kukupa ofa tu, da kijana una balaa wewe!” Ipyana alimwambia Nelly kwa sauti ya chini walipokuwa wakinywa chai.
“We ngoja hiyo jioni ifike, mimi akijipendekeza namlamba bakora zakutosha kwani siyo dada yangu yule,” Nelly alimwambia Ipyana, wakacheka.

Waliporejea eneo la kazi, kwenye saa tano kasorobo alifika  mama Maduu aliyejazia nyuma aliyetokea kumtamani Nelly,  baada ya salamu alimwuliza Ipyana Nelly alikuwa akiishi wapi akamwambia Tandika.

“Kumbe mnaishi eneo moja, sasa nakuomba kama hutajali saa sita twende mara moja pale Vetenary Tazara ukanisaidie kubeba mabati nitakayoyanunua tuyapeleke nyumbani kisha tunarudi, unasemaje?”  mama Maduu alimwambia Nelly.
“Hakuna shida mama yangu, si hatutachelewa sana?” Nelly alimwuliza.

Mama huyo alimwambia wasingechelewa ndipo alifungua pochi na kutoa noti ya shilingi elfu kumi na kuwaambia wagawane na kwamba anakwenda ofisini kwake kumalizia kazi f’lani itakapofika saa sita kamili atamwita Nelly.
“Kwani wewe Nelly hauna simu?” mama huyo alimwuliza.

Nelly alimwambia alikuwa nayo na bila kusubiri aulizwe namba akamwambia namba zake ambapo mama huyo akazisevu, kisha akaachia bonge la tabasamu lililomchanganya sana sharobaro Nelly.

“Kaka wewe una nyota ya kupendwa, nahisi huyo mama hana kazi yoyote zaidi ya kukutunuku, kwa ninavyomfahamu huenda anataka kwenda kukufanyia shopping ya nguvu, ngoja tusubiri,” Ipyana alimwambia Nelly.

Saa sita kasoro dakika tano, simu ya Nelly iliita alipoangalia namba ya mpigaji hakujua ilikuwa ya nani, alipopokea alisikia sauti nzuri ya mwanamke aliyejitambulisha aliitwa mama Maduu!
“Kumbe ni wewe mama!” Nelly aliuliza baada ya kupokea simu.

“Usiniite mama Nelly, niite anti au…” mama huyo hakumalizia sentensi yake na kumwambia Nelly amkute kwenye geti la kutokea.

Nelly aliachia tabasamu na kumwambia Ipyana alikuwa akizungumza na mama Maduu aliyemwambia amkute geti la kutokea nje, Ipyana hakuwa na la kusema zaidi ya kucheka na kumtania Nelly kwamba akirudi naye alitaka zawadi kutoka kwa mama.
Nelly alimuaga Ipyana huku akimwambia kama atapewa zawadi wala asijali angempelekea, kijana huyo aliyebadili nguo na kuvaa alizotokanazo nyumbani alikwenda kumsubiri mama Maduu getini.

Hazikupita hata dakika nne aliliona gari la mama huyo likielekea getini kisha kusimama, Nelly aliingia kwenye gari la mama huyo huku baadhi ya madereva waliokuwepo pale getini wakiwasubiri mabosi wao kuanza kumjadili.
“Jamani mmemuona mama Maduu katoka na yule dogo mgeni anayeosha magari?” dereva mmoja ambaye wenzake walipenda kumwita Mwarabu kutokana na weupe wake aliwaambia wenzake.

“Tumemuona bwana, kwa tabia zake za kupenda viserengeti boy huenda anakwenda kujirusha naye,” dereva Mwarabu aliwaambia wenzake waliokubaliana naye.

Mama Maduu akiwa na Nelly kwenye gari bila aibu alimweleza kwamba hakuelewa kwa nini tangu alipomuona jana yake alitokea kumpenda kiasi cha kumfikiria sana.
“Kwa binadamu hilo ni jambo la kawaida, mimi nashukuru mama kwa kunipenda,” Nelly alimwambia.
“Nimekwambia usiniite mama…niite anti,” mama Maduu alimwambia Nelly huku akikanyaga mafuta hivyo gari kwenda kasi.
“Oke anti,” Nelly alimwambia.

Nelly ambaye hakujua walikuwa wakienda wapi alitulia huku akijisemea moyoni kwamba kama mama huyo akirogwa kutaka mambo angemvuruga kisawasawa.

Mama Maduu aliyeonekana kuwa na furaha alipofika kwenye mataa ya Barabara ya Kawawa na Nyerere alikata kushoto kuelekea Keko, akaongeza mwendo kisha alikata kuelekea Maduka Mawili.

“Awali nilitaka twende Vetenary kununua mabati lakini nimekumbuka kuna kazi f’lani nyumbani ngoja ukanisaidie kwanza hiyo ndipo twende Vetenary kama muda utaruhusu,” mama Maduu alimwambia Nelly.

Je, unajua kilichojiri baada ya mama huyo mpenda viserengeti boy kufika na Nelly nyumbani kwake? Usikose uhondo huu wiki ijayo. Maoni tumia namba hiyo juu.

Leave A Reply