The House of Favourite Newspapers

Ngoma apewa sh.millioni 200

Donald-Ngoma-1Donald Ngoma.

Wilbert Molandi, Dar es Salaam
SIJUI utatafsiri vipi lakini habari mpya mjini ni kuwa Klabu ya Yanga imeweka pembeni dau la dola 100,000 (zaidi ya shilingi milioni 200) kutoka kwa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa ajili ya usajili wa straika Donald Ngoma.

Wiki iliyopita gazeti hili liliripoti kuwa klabu hiyo ya Sauz inamhitaji straika huyo raia wa Zimbabwe na tayari mazungumzo yameshaanza kwa siri.

Pamoja na mazungumzo hayo ya usajili, lakini Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, aliweka wazi mapema kuwa hataki kumuuza mchezaji huyo kwa kuwa ni muhimu kikosini kwake.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zinaeleza kuwa, uongozi ulikuwa tayari kumuuza mshambuliaji huyo kwa shilingi bilioni 2 na siyo ofa ya dola 100,000 ambayo ilitolewa na Wasauz.

“Ngoma alinunuliwa kutoka FC Platinum (ya Zimbabwe) lengo kubwa likiwa ni kumtumia katika Ligi ya Mabingwa Afrika, kumuuza bila ya kumtumia katika michuano hiyo itakuwa ni kazi bure.

“Ndiyo maana uongozi umekataa ofa ya dola 100,000 kutoka kwa hao Wasauz. Hata hilo dau la bilioni mbili ni kama kuwakomoa hao jamaa ili wasirudi kumuwania,” kilisema chanzo hicho.

Upande wa Pluijm alipoulizwa tena juu ya suala hilo alisema: “Sitakuwa tayari kumuuza Ngoma na mchezaji mwingine yeyote kwenye kikosi changu hiki kwa sasa, kwa kuwa tuna michuano mikubwa mbele yetu ikiwemo ligi kuu na ligi ya mabingwa.”

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha, kuzungumzia sakata hilo, simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa.

Comments are closed.