The House of Favourite Newspapers

Hassan William Mbeya: ‘Nilikuwa Msukule kwa Miaka 12’

0
Picha ya mtandao.

DAR ES SALAAM: Kazi ipo! Hassan William (28) ni kijana, mwenyeji wa Kijiji cha Uturo, Mbeya ameibuka na kudai kuwa, alichukuliwa msukule kwa miaka 12 na kupotezana na wazazi wake, Judith Wambura na William Mgaya.

USHUHUDA WAKE NI HUU Akizungumza na Uwazi juzi, Kigamboni jijini hapa alikohifadhiwa na wasamaria wema, Hassan alisema, ilikuwa mwaka 2003 akiwa darasa la tano katika Shule ya Msingi Uturo, siku hiyo ghafla alipatwa na maumivu makali ya kichwa na baada ya muda mfupi tu akafariki dunia.

WALIZIKA MGOMBA Alisema jitihada za mazishi zilifanyika kwa mila na desturi za kabila lao, bila watu kujua wakiwemo wazazi wake kwamba wanakwenda kuuzika mgomba.

“Wakati watu wakinizika, mimi nilisimama pembeni nikishuhudia kila kitu lakini sikuweza kuongea. Niliwaona  kabisa watu wanazika mgomba. Hapo mimi nilikuwa  nimeshachukuliwa msukule na wachawi, nikapelekwa nyumbani kwa ndugu yangu mmoja ambaye ndiye  aliyenifanyia ubaya huo.

AFANYISHWA KAZI NZITO

“Huko nilikopelekwa nilikutana na watu wengine sita ambao walishakatwa ulimi. Tukapelekwa kuishi kwenye pango tukifanyishwa kazi mbalimbali huku chakula chetu kikubwa kikiwa ni pumba, unga, damu na nyama mbichi ambazo nyingine hata hatukujua zilikuwa za wanyama gani.”

Akifafanua kazi alizokuwa akizifanya huko, Hassan alisema ni kwenda kwenye maduka ya watu waliowaweka msukule kufanya usafi ili kuvuta wateja na kubeba mizigo, ikiwemo kuhamisha vitu kupeleka wanapopataka wao, pia kulima mashamba na kazi nyingine ambazo ni ngumu.

SIKU YA KUTOKA KWENYE MSUKULE

“Kwa kipindi chote hicho, nashukuru Mungu mimi sikuwa nimekatwa ulimi kama wenzangu, kwa kuwa wenyewe wachawi walikuwa hawajaamua. Nakumbuka Juni mwaka 2015, tulikwenda kubeba mizigo kwenye meli tukachoka sana. Ulipofika muda wa chakula, wenzangu wakapewa pumba, mimi nikapewa wali na njegere.

“Nilipokula kile chakula ghafla nikajiona tofauti, nikashangaa nipo kijiji kingine jirani na kijiji chetu, nikaona nimezingirwa na watu wengi wakinishangaa. Watu wa kanisani wakanichukua, wakaniombea na kunisafisha zaidi ya mara tatu ili kutoa uchafu niliokuwa nao na kunikata nywele, kwani zilikuwa ndefu na zinanuka sana,” aliongeza.

ACHUKULIWA NA MAMA MCHUNGAJI

Hassan aliendelea kusema kuwa, baada ya hapo akawa anaishi nyumbani kwa mama mchungaji anayeitwa mama Fausta Mwakifamba ambaye alimtafutia mtu akawa anamfundisha kuongea hadi akarejea kwenye hali ya kawaida, ndipo akaenda kuwasaka wazazi wake kijijini kwao na kuambiwa walihamia jijini Dar es Salaam.

“Mzee mmoja akasema hajui baba anaishi Dar sehemu gani, ila akanipa namba ya simu ya mtu mwingine aliyeondoka naye.

ATUA DAR KUSAKA WAZAZI

“Nilimpigia simu huyo mtu, akaniambia hajui wazazi wangu wanaishi wapi Dar lakini kweli wapo Dar. Akasema atanitumia nauli nije ili tumtafute wote. Alinitumia nauli, lakini nilipofika hapa kama wiki mbili zilizopita simpati kwenye simu.

“Mimi sina makazi maalumu, kikubwa nahitaji kuwaona wazazi wangu ambao biashara yao kubwa zamani ilikuwa kuuza magodoro,” alisema Hassan.

KUMPATA HASSAN

Kama wazazi wa kijana huyo watafanikiwa kusoma habari hii, wanaweza kumtafuta mtoto wao kupitia namba; 0653 566207.

Na Mayassa Mariwata/GPL

Leave A Reply