The House of Favourite Newspapers

Nilitaka kumuua mwanangu mara 3, leo ananisaidia!

0

HABARI za leo wapendwa wasomaji wa safu hii. Wiki iliyopita tulimaliza kusoma mkasa wa mwanadada Tumia Njiru aliyetuhabarisha juu ya uovu alioufanya kwa tajiri aliyemuajiri kwa kazi za ndani. Hata hivyo, tunapata faraja kwamba pamoja na ukatili huo, leo anajutia alichokifanya.

Katika safu hii leo, tunaye bwana mmoja mwenye zaidi ya miaka 60, ambaye ameomba afahamike kwa jina moja tu la mzee John anayetusimulia jinsi alivyojaribu mara tatu kumuua mtoto wake kipenzi, lakini akashindwa.

“Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa hai hadi leo, kwani ananipa hukumu niliyostahili kabisa. Kila mara najikuta nikiangua kilio na miaka yote nimeshindwa kumweleza ukweli kijana wangu ambaye hivi sasa ndiye ananipa msaada mkubwa sana.

“Mimi nimezaliwa mkoani Tabora ingawa wazee wangu ni wenyeji wa Mkoa wa Iringa. Niliishi kule hadi nilipomaliza elimu ya msingi na kwa vile sikufanikiwa kuendelea na masomo, nikaanza harakati za kutafuta maisha nikiwa bado mdogo. Nikaondoka Tabora kuelekea Dar es Salaam.

“Nilipanda treni nikiwa sina hata hela, sikulala usiku kazi yangu ilikuwa ni kumkimbia TT (Mkaguzi wa tiketi ndani ya treni) hadi nafika. Nilipofika Dar sikuwa na mtu ninayemfahamu, hivyo nikafikia sokoni Kariakoo shimoni ambako nilikuwa nalala. Kazi yangu ilikuwa ni kusubiri usiku wakati malori ya mazao yanapoingiza bidhaa, nikawa nachomoa vitu kidogo kidogo.

“Likija lori la viazi, navizia vinavyoanguka na vingine navichomoa, likija la maharage hivyo hivyo, nyanya hali kadhalika, najaza kwenye viroba, asubuhi nikawa nauza. Niliendelea na maisha hayo kwa muda wa kama miezi mitano hivi, nikawa naweka hela kidogo kidogo hadi nikapata za kutosha kupanga chumba kule Manzese Midizini.

“Lakini kwa kuwa nilishazoeleka pale shimoni Kariakoo, kazi ile sikuiacha maana tulikuwa vijana wengi tunafanya hivyo, sasa badala ya kuuza pale, mimi nikawa nakuja na vitu vyangu mtaani, nikawa navipanga barabarani pale Manzese, nikawa napata faida mara mbili ya awali.

“Nikafanikiwa kupata meza sokoni hadi nikafikia kununua mwenyewe mizigo kutoka mikoani badala ya kuiba na kuvizia vinavyoanguka pale Kariakoo. Namshukuru Mungu maisha yangu yalianza kubadilika na miaka michache baadaye nikafanikiwa kumpata binti mmoja nikamchukua na kuanza kuishi naye.

“Nikahama pia pale nilipokuwa nimepanga awali, kwani chumba kilikuwa kidogo na nyumba yenyewe haikuwa nzuri, hivyo nikapata vyumba viwili maeneo ya Mburahati Motomoto, nikaanza maisha mapya. Pale jirani kulikuwa na banda ambalo lilijengwa lakini likawa halitumiki, nikamtafuta mmiliki akanikodisha. Nikaweka genge la vyakula, nikawa napika na chips.

“Maisha yalibadilika haraka sana, nikajikuta naanza kupata pesa za kutosha. Nikawa nawasiliana na wazazi nyumbani Tabora, nikawa nawatumia pesa ili kutatua matatizo yao madogo madogo na ya ndugu zangu. Nakumbuka nikiwa na miaka 23 hivi, nikajaaliwa kupata mtoto wangu wa kwanza wa kike, Asha, nilifurahi sana.

“Maisha yaliendelea vizuri kwani nilibahatika kununua kiwanja kule Tabata, nikaanza ujenzi na kumaliza baada ya miaka miwili tu, nikahamia na familia yangu na kwa hakika, nuru ya maisha mazuri niliiona, niliamini nikiendelea na juhudi zile, basi huenda nami ningekuwa mmoja kati ya watu wenye fedha za kutosha mjini.

“Nikaachana na kile kibanda kule Mburahati, nikafungua duka kubwa sana maeneo ya Tabata Bima, nikawa nauza vyakula na vitu vingine vingi vya nyumbani. Nikawa napata heshima mtaani, nikifika walipokaa watu, nilipishwa kiti, nilipata faraja na kuanza kuota ndoto za utajiri.”

Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia mkasa huu wa kweli katika toleo lijalo.

Leave A Reply