The House of Favourite Newspapers

Niliolewa na Mganga kwa Tamaa ya Cheo Kazini-27

0

ULIPOISHIA:

Wakati huo mkewe alikuwa amempokea mizigo aliyokuwa nayo na kupeleka ndani na kutuacha wawili. Kabla ya kusema kitu alipaza sauti kutaka maziwa, mmoja  wa wakeze alikuja na kibuyu cha maziwa. Ilionesha jinsi gani mzee yule alivyokuwa akiwanyanyasa wakeze, kama hayupo basi hakuna kulala mpaka arudi.

SASA ENDELEA…

Baada ya kunywa maziwa alitulia kwa muda kisha alisema:

“Nina imani kazi itafanyika usiku huu ili uondoke alfajiri uwahi kazini.”

Kauli ile ilinishtua na kuamini mzee Sionjwi anajua mambo bado yako vilevile, ilibidi niingilie kati maneno yake.

“Babu.”

“Nina imani majina umeyapata hivyo nipe nikayafanyie kazi sasa hivi ili usiku nimalize kazi kwa kuwazika na kuipandisha nyota yako juu yao.”

“Babu mambo yamekwenda tofauti.”

“Kivipi?”

Nilimweleza hali ilivyokuwa , baada ya kunisikiliza sikumuona kushtuka zaidi ya kusema:

“Bado nafasi yako iko palepale.”

“Mmh! Babu maneno yako yana ukweli?”

“Binti hujawahi kunifundisha kazi hata siku moja, wewe unaitaka nafasi au unataka kujua utaipataje?”

“Hapana babu, mazingira yamenikatisha tamaa.”

“Sasa kama yamekukatisha tamaa kwa nini umekuja huku?” aliniuliza kwa sauti ya ukali kidogo.

“Nisamehe babu, nimechanganyikiwa,” niliomba msamaha baada ya kuona nimeingilia kazi yake.

“Wewe kazi yako kuleta tatizo litakalobaki niachie mwenyewe.”

“Sawa babu nimekuelewa.”

“Haya nipe hayo majina ya watu wako, kwa vile kuna kazi mpya imeingia nipe jina la huyo msichana aliyechaguliwa ambalo nitaanza nalo kisha nimalizie hao mabosi wako. Kazi zote zinafanyika usiku huu ili kesho uwahi kazini. Safari yako iko palepale na tarehe ikifika lazima uende wewe.”

Mmh! Zilikuwa habari njema kwangu, lakini majina sikuwa nayo hata huyo msichana sikuwa na jina lake. Nilijikuta nikichanganyikiwa mtoto wa kike, lakini nilikumbuka mtu muhimu wa kunipatia majina alikuwa Safia. Nilimkubalia mzee Sionjwi kumpatia majina ya watu watakaokuwepo kwenye kikao na jina la msichana aliyechaguliwa kwenda kusoma.

Mwaka wa mkosi ni wa mkosi kumbe simu yangu tangu jana haikuwa na chaji na nilitegemea kuichajia ofisini lakini kutokana na kuchanganywa sikuchaji simu iliyokuwa inaishia chaji.

Pia sikutegemea kutumia simu nikiwa kijijini kwa vile sikuwa na kitu cha kuhitaji mjini kutokana na muda niliokuwa nao huko na kuwahi kurudi mjini.

Kila nilipojaribu kuiwasha simu iliwaka nilipojaribu kupiga ilizimika, mwanzo ilikuwa inawaka lakini baadaye ilikataa  kabisa .

Nilijikuta nikijilaumu kwa kuitanguliza hasira mbele na kuondoa akili ya kufikiri. Nakiri kuchanganyikiwa baada ya kujua nimeikosa nafasi niliyoiona kama bahati ya mtende.

Kwa vile nilichanganyikiwa nilisahau hata kujua jina la msichana aliyechaguliwa, kuhusu majina ya watu wa bodi ukweli wa Mungu sikuwa na shida nayo baada ya kupata ukweli kuwa mtu wa kuondoka tayari kachaguliwa mpaka tiketi na viza vipo tayari kilichokuwa kikisubiriwa ni safari tu.

Kitendo cha simu yangu kuzimika kilinikosesha raha kwa kuamini zoezi lile litashindikana na kujilaumu sana kwa kushindwa kutekeleza  niliyoagizwa na mzee Sionjwi na kujifanya najua kumbe naungua na jua.

Sikuwa na jinsi ilibidi nimweleze ukweli mzee Sionjwi aliyekuwa amekwenda ndani mara moja.  Nilimtuma mmoja wa wakeze aniitie mzee ili nizungumze naye nijue atanisaidia vipi. Niliambiwa anaoga kisha apate chakula ndipo azungumze na mimi.

Kwa hatua ile niliona hakukuwa na umuhimu wowote wa kulala pale kwa vile sikuwa na kitu cha kufanya. Nilitamani nikutane haraka na mzee Sionjwi ili niwahi kurudi mjini kuchukua majina ya watu watakaokaa kwenye bodi na jina ya mhusika.

Hamu ya kukaa kijijini iliniisha na kupachukia kuendelea kuwa pale kwa muda ule. Mzee Sionjwi nilijua anajua nina majina hivyo kazi ingefanyika usiku ule kumbe mwenzake nilishafanya upuuzi.

Baada ya saa moja kupita mzee Sionjwi alikuja na sufuria lililokuwa limefungwa shanga za rangi nyingi na kitambaa cha sanda. Wakati huo ilikuwa imefika saa nne na nusu za usiku, alipofika alisema:

“Haya mjukuu nipe hayo majina nikuonesha muujiza anaofanya Mungu kuwachukia wachawi kwa vile huwa tunageuza anachokifanya. Hii kazi sawa na kumfufua mtu aliyekufa kitu ambacho kimewashinda waganga na wachawi wote duniani,” mzee Sionjwi alisema huku akiweka sufuria mbele yangu.

“Babu,” nilimwita ili nijitetee.

“Mjukuu huu si muda wa kuitana nipe kwanza majina hayo nikayazike, naomba katika hayo majina uandike na lako liweke kwa juu kisha nilichoree nyota ili kuonesha mwanga.”

Mmh! Nilijiona mtu mwenye mkosi kufanya papara za kukimbilia kwa mganga  bila kupeleka nilivyotumwa. Mzee Sionjwi aliendelea kuzungumza bila kujua mwenzake nipo kwenye hali gani.

“Bibi hebu fanya haraka kwa vile kazi kubwa itafanyika usiku wa manane unaoga na kuondoka. Siku ya pili ukifika ofisini utaniambia mimi ni nani. Hata ungetaka ukurugenzi wa kampuni ningeweza kukupatia hapa ni zaidi ya kufuru.”

“Sawa babu nimekuelewa ila..”

“Nini tena mjukuu sema kinachokusibu wala usiwe na wasi siwezi kumrudisha aliyekufa tu lakini tatizo lako lolote hapa ndipo kiboko yake. Huu ni muda wa kunitumia nikifa usijejuta.”

“Sawa babu ila…” nilijkuta nikishindwa kumalizia sentesi nilianza kulia kitu kilichomfanya mzee Sionjwi kunisogelea na kunishika begani, mmh! Makubwa ngozi yake kavu ya mkono ilipogusana na ya kwangu nilihisi msisimko wa ajabu.

“Una nini mjukuu?” aliniuliza kwa sauti ya kubembeleza.

“Sina majina uliyonituma.”

“Ha! Mjukuu, kwa sababu gani umekosa majina?”

Je, nini kitaendelea? Fuatilia wiki ijayo. katika Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

Leave A Reply