The House of Favourite Newspapers

Penzi lisiloisha     047

0

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kufanya chochote kumsaidia msichana huyo. Licha ya tofauti kubwa ya hali zao kiuchumi, Anna akitokea kwenye familia ya kitajiri na kijana huyo akitokea kwenye familia ya kifukara, mapenzi yao yanashamiri kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.

Awali, Jafet alikuwa akisomeshwa na kanisa kwa makubaliano kwamba akimaliza masomo atajiunga na mafunzo ya upadri kwa ajili ya kulitumikia kanisa, lakini baadaye anabadilisha uamuzi na kukataa kwenda kusomea tena upadri kutokana na jinsi alivyokuwa anampenda Anna.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Baada ya Jafet na Anna kuhitimu kidato cha nne, Anna anaanza maandalizi ya kutafuta shule ili wakasome pamoja kidato cha tano na sita, gharama zote zikiwa ni juu yake kwani wazazi wa Jafet hawakuwa na uwezo wa kumsomesha.

Msichana huyo anafanya kila kinachowezekana na hatimaye wawili hao wanajiunga kidato cha tano kwenye shule moja, bila wazazi wa Jafet kujua chochote. Baadaye Anna anaanza kuumwa figo, baada ya kuhangaika sana Jafet anaamua kumtolea figo moja, wanasafiri hadi India ambako wanafanyiwa upasuaji na msichana huyo kuwekewa figo nyingine kutoka kwa Jafet.

Zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio makubwa kisha wanarejea Tanzania. Wiki kadhaa baadaye, wazazi wa Anna wanamshinikiza Jafet awapeleke nyumbani kwa wazazi wake ili wakawashukuru kwa wema wake, anakuwa mgumu lakini baadaye anakubali, wanafunga safari mpaka kijijini Rwamgasa.

Wazazi wa Anna wanamkataa Jafet baada ya kujua maisha yake halisi na kwa juhudi za mama yake, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani kisha anapelekwa bila hata kuagana na Jafet, jambo ambalo linamuumiza mno kijana huyo kutoka familia ya kimaskini. Moyo wake unabaki na majeraha makubwa yasiyopona na kujikuta akipata matatizo ya figo yake moja iliyosalia. Anna naye anajikuta akianza kuzoeana na William, Mtanzania mwenzake waliyekuwa wakisoma naye chuoni nchini Marekani.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Wiki moja baadaye, kama alivyokuwa ameahidi, Jafet alifunga safari mpaka jijini Mwanza, kufuata vyeti vyake vya elimu ya kidato cha tano na sita. Jafet aliposhuka kwenye stendi ya mabasi jijini Mwanza, alianza kutafuta usafiri wa kumpeleka shuleni kwake lakini ghafla, alisikia jina lake likiitwa kwa nguvu.

“Jafet! Jafet! Jafetiii!”

Harakaharaka aligeuka kutazama sauti ile ilikokuwa inatokea. Akakutana uso kwa uso na mlinzi wa nyumbani kwa akina Anna, Babu Malata ambaye walikuwa wakielewana sana kipindi cha nyuma wakati akiwa na uhusiano mzuri na familia hiyo.

“Jafet! Ni wewe? Vipi za siku? Mbona umekonda sana?”

“Ni mimi babu Malata? Za siku nzuri kabisa. Nimepungua nilikuwa naumwa.”

“Ooh! Pole sana, nini zaidi?”

“Aah! Kawaida tu, nilikuwa na matatizo ya figo lakini namshukuru Mungu sasa hivi naendelea vizuri.”

“Maskini pole Jafet! Nimefurahi kukuona lakini nasikitika sana kwa kilichokutokea. Mshukuru Mungu kwa kila jambo.”

“Nashukuru babu, nimekuja kuchukua vyeti vyangu kwenye shule niliyokuwa nasoma.”

“Kwani siku hizi unasoma wapi?”

“Nipo chuo kikuu, Dar es Salaam nasomea udaktari.”

“Ooh! Hongera sana na Mungu akutangulie. Mimi ni miongoni mwa watu ambao tuliumizwa sana na kitendo ulichofanyiwa na Anna pamoja na familia yake. Ila ninachoamini bado Anna anakupenda kwa sababu hata siku ambayo anaondoka alikuwa akilia sana huku akikutaja.”

“Nimeshasamehe na naamini Mungu atanilipia.”

“Nimesikia baba na mama yake wanasema anaweza kurudi kesho kwa ajili ya mapumziko mafupi. Anakuja na ndege ya saa nane mchana,” alisema mlinzi huyo, kauli ambayo iliupasua mno moyo wa Jafet. Hata hivyo, hakutaka kuonesha waziwazi hisia zake, akajikaza kisabuni na kuendelea kuzungumza na mlinzi huyo kisha wakagaana.

Baada ya kuagana na mlinzi huyo, Jafet alishindwa kuendelea na safari yake, ikabidi atafute sehemu tulivu na kukaa kwa dakika kadhaa akitafakari alichoambiwa na mlinzi huyo. Ni kweli kwamba Anna alikuwa amemuumiza sana Jafet kwa kitendo chake cha kuondoka bila kumuaga na kwenda nchini Marekani lakini kumbe nyuma ya pazia msichana huyo naye hakupenda iwe hivyo ila ilikuwa ni shinikizo kutoka kwa wazazi wake. Kilichozidi kumfanya aamini kauli hiyo ni kwamba hata siku moja hakuwahi kumtamkia kwamba hampendi.

Akawa anajiuliza maswali mwenyewe bila kupata majibu, mwisho akaamua kwamba aende uwanja wa ndege kuonana na Anna ili amsikie kwa mdomo wake kama bado anampenda au hamtaki tena. Aliamini kwamba akimsikia akizungumza kwa mdomo wake, atakuwa na uhakika zaidi wa msimamo wa msichana huyo ambaye bado alikuwa akiendelea kuutesa moyo wake kila anapomkumbuka.

Mwisho alifikia muafaka kwamba aende kuchukua vyeti vyake shuleni kwao, Lake Zone High School kama alivyokuwa amepanga kisha baada ya hapo, atafute nyumba ya kulala wageni ambapo atapumzika mpaka mchana wa siku iliyokuwa inafuatia ili aende kushuhudia Anna akiwasili na ndege.

Japokuwa ulikuwa ni uamuzi unaohitaji ujasiri, Jafet alipiga moyo konde kwa lengo la kujua hatma yake na Anna. Akaenda mpaka shuleni kwao ambako alipokelewa kwa uchangamfu na walimu pamoja na wanafunzi waliokuwa wanamfahamu, wengi wakaonesha kumshangaa kwa jinsi alivyokuwa amedhoofika.

Baada ya kukamilisha taratibu zote shuleni hapo, alikabidhiwa vyeti vyake na kuondoka, akarudi mjini ambako alitafuta nyumba ya kulala wageni ya bei rahisi na kupumzika. Fedha kidogo alizosafiri nazo kutoka jijini Dar es Salaam zilimsaidia kufanya mambo madogomadogo aliyokuwa anayataka.

Baada ya kulipia chumba na kupata chakula cha jioni, Jafet alitoka na kwenda kukaa pembezoni mwa Ziwa Victoria, akawa anarusharusha mawe kwenye maji huku akiendelea kutafakari mambo mbalimbali kichwani mwake. Kadiri muda ulivyokuwa unasonga mbele ndivyo shauku ya kumuona Anna ilivyokuwa inazidi kuongezeka ndani ya moyo wake.

Kuna wakati alimlaumu babu Malata kwa kumpa taarifa juu ya Anna kwani japokuwa alikuwa ameshamsahau, kitendo cha kuambiwa kwamba alikuwa mbioni kurejea nyumbani kiliamsha vuguvugu jipya ndani ya moyo wake. Upande mwingine, alimshukuru kwani baada ya kupotezana kwa muda mrefu, hiyo ilikuwa nafasi yake nyingine ya kipekee ya kuonana naye.

Muda ulizidi kuyoyoma na hatimaye siku hiyo ikapita, Jafet akiwa ndani ya nyumba hiyo ya kulala wageni. Kesho yake, aliwahi kuamka na kama kawaida yake, akafanya mazoezi mepesi ya viungo, akapata kifungua kinywa kisha akaondoka kuelekea Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Japokuwa aliambiwa Anna angewasili saa nane za mchana, saa nne juu ya alama tayari Jafet alikuwa ameshawasili uwanjani hapo, akaingia kwenye jengo la kusubiria wageni na kutafuta sehemu ya kukaa, ambayo haikuwa rahisi kwa mtu mwingine yeyote kumuona.

Alijua lazima ndugu zake Anna, wakiwemo wazazi wake watafika kwa ajili ya kumpokea lakini hakutaka kabisa kukutana nao, alichokitaka ilikuwa ni kumuona Anna tu, basi! Watu wengi waliendelea kuwasili uwanjani hapo, wengine wakiwa ni wasafiri na wengine wakiwa ni watu waliokuwa wameenda kuwapokea ndugu zao.

Muda ulizidi kuyoyoma na hatimaye ikatimia saa saba za mchana, watu wengi wakazidi kumiminika kwenye jengo la kupokelea abiria, kwani ndege ya kutoka jijini Dar es Salaam ilikuwa imebakiza muda mfupi kabla ya kuwasili.

Miongoni mwa watu waliokuwa wanaendelea kuwasili, Jafet alifanikiwa kuwaona mama yake Anna, mdogo wake pamoja na ndugu zake wengine, wakiwa wamebeba maua na kadi zilizokuwa na ujumbe wa kumkaribisha Anna.

Kumbukumbu zake zilimrudisha nyuma, akakumbuka mapokezi aliyoyapata akiwa na Anna, walipokuwa wakirejea kutoka nchini India alipoenda kumtolea figo, akajikuta akishindwa kuzizuia hisia zake, machozi yakawa yanamtoka.

Muda mfupi baadaye, sauti ya mhudumu wa uwanja huo wa ndege ilisikika ikiwataarifu watu wote kwamba ndege iliyokuwa ikitarajiwa kuwasili kutoka jijini Dar es Salaam, tayari imeshawasili jijini Mwanza na muda wowote itatua kwenye uwanja huo. Watu wote wakasimama na kuanza kujipanga, tayari kwa kuwapokea ndugu zao.

Dakika saba baadaye, lango kubwa la kutokea uwanjani hapo lilifunguliwa na abiria wakaanza kutoka, mapigo ya moyo ya Jafet yakawa yanaamuenda mbio kuliko kawaida, akiwa na shauku kubwa ya kumuona Anna.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko. 

Leave A Reply