The House of Favourite Newspapers

Niliolewa na Mganga kwa Tamaa ya Cheo Kazini-36

0

Ajabu wakati babu anaondoka nilimsindikiza kwa macho huku hali yangu ikibadilika na kutamani kitu kutoka kwake. Lakini nilijizuia kama isingekuwa ana wake ningemuomba nifuatane naye ili anipe angalau cha majanini ili usiku kwenye kazi  tusiingie majaribuni na kuharibu tena tiba.

                                                          ***

Usiku kama kawaida baada ya chakula cha usiku na kupumzika kidogo safari ya mzimuni ilianza. Nilibeba vitu kama tulivyobeba jana yake ila tuliongeza na kuku mwekundu ambaye tulikwenda naye kwa ajili ya kuuomba msamaha mzimu kutokana na uchafu wetu wa jana yake.

Tulipofika, nilibadili nguo kwa kuvua nguo nilizokwenda nazo na kujifunga upande wa kanga na yeye alijifunga kipande cha shuka nyeupe. Alimchukua kuku na kusogea karibu ya mti ule mkubwa na kusema kwa sauti ya juu.

“Mzimu najua jana uliondoka kwa hasira, leo nimekuletea zawadi nzuuuuri, naomba uje uchukue.”

Alimweka kuku juu ya jiwe lililokuwa mbele ya mti mkubwa, mara ghafla nilisikia mtikisikio ukifuatiwa na upepo  mwanana. Ghafla niliona majani yakizunguka kama kimbunga na kuelekea kwenye lile jiwe na kuzunguka kwa muda kisha ulipanda juu kuelekea juu ya mtu ule mkubwa.

Ajabu ya Mungu kuku yule hakuwepo kuonesha mzimu ulikuja kama kimbunga na kuondoka na yule kuku.  Baada ya muda hali ilitulia na kutokea mguno mzito kisha pakawa kimya.

Mganga alichukua usinga wake na maji ya dawa na kuanza kunyasia kila kona na kusema:

“Asante mzimu, asante kwa kukubali ombi letu na kutuhakikishia kazi iliyofanyika imekwenda vizuri.”

Baada ya kusema vile aliweka  dawa kwenye maji yaliyokuwa kwenye beseni pamoja na majani ya kujisugulia. Alinieleza nijimwagie maji na kujisugua na majani kisha nijimwagie tena maji kuondoa uchafu na baada ya zoezi hilo aliniwekea kipande cha shuka nyeupe pembeni ili nijifunge.

Ajabu ya Musa baada ya kunitayarishia  kila kitu aliondoka na kuniacha peke yangu na yeye kwenda kuendelea na mambo mengine na kuniomba nikimaliza nimjulishe ili tuendelee na zoezi lingine.  Sikutaka kuhoji ya jana yake na ya siku ile.

Nilifanya kama nilivyoelekezwa kwa kujimwagia maji na kujisugua mwili mzima ilikuwa tofauti na jana yake kujisugua kiungo kimojakimoja na kujimwagia maji na kuhamia kingine lakini siku ile baada ya kujimwagia maji mwili mzima nilitakiwa kujisugua na majani yale mwili mzima kisha kujimwagia maji tena baada ya hapo zoezi lile linakuwa limekwisha.

Baada ya kumaliza zoezi  nilivua kanga iliyokuwa imetota kwa maji na kujifunga kipande cha shuka nyeupe kisha nilimwita  babu na kumweleza nimemaliza kuoga maji ya dawa. Babu alikuja na kunieleza nizunguke mti ule mkubwa mbele yake kulikuwa na kichuguu na kunieleza nipande juu ya kichuguu ili anipandishe nyota.

Kabla ya kupanda alinivisha hirizi mbili moja nyeusi na nyeupe na shanga za rangi ileile ya hirizi zile mbili. Baada ya kunivisha hirizi na shanga alinipa kibuyu kidogo kilichokuwa na shanga mchanganyiko shingoni na kunieleza nipande nacho juu ya kichuguu huku nimekibeba kichwani.

Nilifanya vile kisha babu naye alipanda na kuanza kunichanja baadhi ya sehemu alizozichagua.  Baada ya kumaliza kunichanja alinieleza nitoe kibuyu kichwani na kunyoosha mikono kisha niombe mambo ninayoyataka kimoyomoyo. Nami niliomba niipate ile nafasi ya kwenda kusoma ulaya pia niipate nafasi ya juu katika kazi yangu na mshahara mnono.

Wakati nikiomba vitu ninavyovitaka ilishuka mvua ya nguvu ya dakika mbili na kunifanya nihofie kazi yetu kuharibika kwa mara ya pili, lakini babu alisema:

“Mjukuu una bahati kila kitu chako kinaonekana kina baraka toka kwa mizimu. Hakika kila ulichokiomba kitakubaliwa.”

Baada ya zoezi lile alinieleza niteremke chini huku nimenyoosha mikono kwa mbele nikiwa nimekishika kibuyu. Baada ya kuteremka alikichukua kibuyu chake huku akionesha tabasamu kwa kazi yake kwenda vizuri sana.

“Mjukuu una nyota kali sana katika watu waliowahi kuja mzimuni wewe umekuwa na bahati kubwa.”

“Usiniambie!”

“Kweli mjukuu, kila kitu kimekwenda kama ulivyotaka.”

Zoezi la siku ile halikuchukua muda mrefu kama jana yake, tulibadili nguo na kurudi nyumbani kupumzika ili kesho nifanye safari ya kurudi mjini na kuusubiri muujiza wa babu. Pamoja na kupewa matumaini makubwa lakini bado kwangu ilikuwa kama njozi ya mchana.

Sikutakiwa  kuhoji kitu kwani nilionekana kama naingilia kazi pia simuamini. Baada ya kufika nyumbani nililala mpaka siku ya pili, niliamshwa alfajiri na kuogeshwa maji ya fukuto kisha sikutakiwa kurudi ndani nilitakiwa niondoke.

“Mjukuu wangu kazi imekwisha unatakiwa kwenda kwenye gari na kuondoka.”

“Sawa babu.”

Niliondoka bila kuwaaga wenyeji wangu hasa shoga yangu Rose, sikuwa na jinsi yalikuwa ndiyo masharti ya babu. Katika wake wa mzee Sionjwi niliagwa na mkewe mdogo aliyeamka kunipashia maji moto wengine niliwaacha wamelala, nilijiuliza Rose atanilaumu vipi kuondoka bila kumuaga, haikuwa amri yangu bali masharti ya mganga.

Nikiwa kwenye gari langu tayari kurudi mjini nilijiuliza itakuwaje kama nikimuhitaji babu. Ajabu babu hakushughulika tena na mimi baada ya kuniaga alirudi ndani. Niliwasha gari na kuondoka huku nikijawa na mawazo juu ya babu kuja mjini kama nitaipata nafasi ya kwenda kusoma.

Wasiwasi wangu huenda babu kaona ngoma nzito hivyo katafuta sababu ya kutokutaka kuniaga kwa kujua lazima tungeagana aje mjini hivyo asingekuja kutokana na kazi aliyoifanya kwenda kinyume japo yeye mwenyewe alijinadi  hashindwi na kitu  kisicho amri ya Mungu.

Kwa vile ilikuwa alfajili niliendesha gari kwa uhuru mkubwa kutokana na hakukuwa na magari njiani mpaka nilipoanza kuingia mjini ndipo nilikutana na magari machache mpaka naingia nyumbani kwangu sikupata usumbufu wowote.

Je, nini kitaendelea? Tukutane Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko..

Leave A Reply