The House of Favourite Newspapers

Niliolewa na mganga kwa tamaa ya cheo kazini-37

0

ILIPOISHIA:

Kwa vile ilikuwa alfajiri niliendesha gari kwa uhuru mkubwa kwa vile hakukuwa na magari njiani mpaka nilipoanza kuingia mjini ndipo nilikutana na magari machache mpaka naingia nyumbani kwangu sikupata usumbufu wowote.

SASA ENDELEA…

Kwa vile siku ile  ilikuwa ni Jumapili sikutaka kufanya kitu chochote nilijipumzisha kutokana na kushindwa kulala vizuri kwa siku mbili nilizokuwa kijijini. Kutokana na uchovu mkubwa nililala kama mfu, nilishtuka jioni ikiwa njaa inaniuma sana.

 Nilikwenda kwenye bar ya jirani na kuchukua chipsi na kuku na kuja kula.

Baada ya chakula niliandaa nguo zangu za kuvaa siku ya pili kazini kisha nilipanda  tena kitandani kulala. Ajabu nilipopanda kitandani mara ya pili nilijikuta nikilikumbuka penzi la babu na kutamani siku ile kama angekuwa karibu yangu ingekuwa nzuri kwangu.

Kingine kilichonichanganya ni jinsi tulivyoagana na babu bila kupeana miadi ya kukutana, moyoni mwangu nilipanga hata kama nitakwenda kusoma lazima nimlete mjini ili anikate kiu. Usingizi hata ulivyonichukua sikujua mpaka nilipoamshwa na alam ya alfajiri ili nijiandae kwenda kazini.

Niliamka kama kawaida na kwenda kuoga na kuvaa nguo zangu na kuwahi kazini huku nikiwa bado najiuliza alichokisema mzee Sionjwi kitawezekana japo hapo nyuma alinifanyia mambo makubwa lakini lile nililiona zito kutokana na mchakato  na hatua aliyofikia.

Kama kawaida niliwasili ofisini na kujipangia majukumu ya siku ile, kabla ya kuanza kazi nilimpigia simu shoga yangu Safia. Baada ya kusalimiana nilianza kazi kama kawaida huku nikisubiri kupata taarifa yoyote kuhusiana na Happy Kinono msichana aliyechaguliwa kwa hila kwenda kusoma nje.

Japo nilikuwa kazini lakini akili yangu yote ilikuwa kusubiri tukio nililoelezwa na babu.  Ajabu muda uliendelea kukatika bila kupata taarifa zozote, niliangalia saa ya mkononi ilionesha bado kama dakika kumi muda wa kutoka kazini ufike. Sikuiamini saa yangu niliangalia ya ukutani nayo ilinionesha muda uleule nilioangalia kwenye saa ya mkononi.

Kutokana na kuchanganyikiwa hata hiyo sikuiamini niliangalia saa ya kwenye kompyuta haikupishana sana na saa zote nilizoangalia. Nilijikuta nikikata tamaa kuona tulichokifanya kwa babu kilikuwa kazi bure. Niliingiwa wasiwasi huenda tukio la kufanya uchafu mzimuni ulisababisha mambo yaharibike.

Muda ulipotimu nilianza kufungasha vitu vyangu ili niondoke kuwahi nyumbani. Mara simu yangu iliita nilipoangalia ilikuwa inatoka kwa Safia, nilijua tu alitaka kujua kama naondoka kwa vile aliniomba lifti kutokana na mumewe kuwa na udhuru.

Niliipokea kwa kumwambia:

“Shoga nisubiri kwenye gari ndo nafungasha.”

“Shoga nilitaka nikuombe unisubiri hata robo saa kwa vile kuna kazi naimalizia ili tuondoke wote.”

“Hakuna tatizo, basi nitakusibiri ofisini kwangu.”

“Tena shoga nina ubuyu (umbeya) mpya hata sokoni haujaingia,” Safia alinirusha roho.

“He! Wa nini tena?” nilishtuka.

“Shoga kwa vile tunaondoka pamoja basi nitakupakulia wa haja.”

“Mmh! Haya.”

Kwa vile nilikuwa nimesimama niliweka mkoba wangu juu ya meza na kuketi kwenye kiti changu kumsubiri Safia huku nikiwa na shauku kubwa ya kuusikia huo ubuyu ambao haujaingia hata sokoni. Nilijikuta nikiwaza huenda ni taarifa niliyoambiwa na babu Sionjwi ya kusikia taarifa ya kushtua.

Lakini nilikuwa mpole kuusubiri huo ubuyu ili nijue unahusu nini pia yaliyosemwa na mzee Sionjwi yana ubashiri gani. Baada ya dakika ishirini Safia alinifuata ofisini akiwa na tabasamu pana kitu kilichonishtua.

“Vipi shoga unaonekana leo una furaha kulikoni?”

“Mmh! Mbona makubwa madogo yana nafuu.”

“Yepi tena hayo shoga?”

“Kwa vile tunakwenda pamoja nisikuonjeshe ukakinahi mapema.”

Sikutaka kuongeza neno, nilibeba begi langu na kuongozana na Safai kuelekea kwenye gari langu.

Baada ya kuingia ndani ya gari tuliondoka eneo la kazini huku nikiwa na hamu ya kujua ubuyu huo una ladha ya aina gani.

Tulipotoka kidogo  Safia alianza kunipa ubuyu nami nilitega masikio huku mapigo ya moyo ukinienda mbio.

“Basi dada kuna bonge la gogoro.”

“Lipi tena hilo?”

“Aliyeteuliwa kagoma kwenda mpaka aipate ndoa.”

“Mteuliwa nani?”

“Si Happy.”

“Happy yupi?”

“Aliyewaengua na kuchaguliwa kwenda kusoma ili akirudi awe juu yenu.”

“M’hu.”

“Basi ndiyo kagoma kasema haendi mpaka wafunge ndoa anataka aondoke kama mke wa mtu na si mchumba.”

“Sasa kuna tatizo gani bado muda upo wa kufunga ndoa na kwenda kusoma.”

“Kweli walikuwa na mpango wa kufunga ndoa lakini safari ya kwenda kusoma ilivuruga kila kitu.”

“Kama walikuwa wameisha jipanga wanaweza kwenda kufunga ndoa tu, sherehe akirudi.”

“Inavyosemekana walikubaliana kufunga ndoa baada ya kurudi, lakini kuna taarifa kazipata kuwa mchumba wake ana mwanamke mwingine, kitendo cha kwenda kusoma huku nyuma wanafunga ndoa na akirudi akute kila kitu kimekwisha.”

“Mmh! Makubwa, sasa yeye taarifa hizo kazitoa wapi?”

“Hata najua.”

“Wewe nani kakuambia?”

“Mkurugenzi.”

“Ilikuwaje mpaka akakuteleza habari hizo?”

“Huwezi kuamini leo meneja alikuja mapema na kuingia kwa mkurugenzi, wamekaa ndani zaidi ya saa nne. Alipotoka alionekana kachanganyikiwa, si ndiyo mama usipitwe nikamfuata mkurugenzi kutaka kujua kuna kitu gani kimemtokea meneja.

“Ndipo aliponipa ubuyu huu, kuna kitu alinieleza kuwa kama itashindikana wangemteua mtu mwingine haraka kabla ya Jumatano si ndiyo na mimi nikapiga chapuo uende wewe.”

“Ehe! Akasemaje?”

“Akasema anasubiri jibu la meneja atakalompa jioni kuwa mchumba wake anakwenda au haendi. Kama haendi kesho asubuhi waanze mchakato wa kumtafutia viza mtu watakayemteua.”

“Mmh!” nilijikuta nikiguna tu.

“Tena huwezi kuamini maombi yangu yule msichana akatae kwenda ili uende shoga yangu.”

“Bado muda huenda wakakubaliana.”

“Aah, wapi mwanamke yule ameapa hatakwenda bila ndoa.”

“Mmh! Ngoja tuone.”

“Ukweli wa mbivu na mbichi utazijua kesho asubuhi.”

Nilimpeleka Safia mpaka kwake kisha mimi nilirudi nyumbani kupumzika nilijiuliza yaliyozungumzwa na Safia yana ukweli gani. Nilijikuta nikitabasamu mwenyewe baada ya kuiona kauli ya babu inakaribia kuwa kweli. Niliamini jibu la kesho ndilo litanipa picha kamili kama nitakwenda mimi au la.

Wasiwasi wangu ilikuwa kama kitaitishwa kikao cha bodi ya uteuzi ningeweza kupoteza nafasi ile. Lakini majina niliyopeleka kwa babu niliamini yakafanya kazi japokuwa sikuwa na uhakika kama watakuwa ni walewale.

Je, nini kilitokea? Usikose kufuatilia simulizi hii katika Risasi Jumamosi siku ya Jumamosi.

JIUNGE NA GLOBAL BRAKING NEWS

GLOBALBREAKINGNEWS100.jpg

Leave A Reply