The House of Favourite Newspapers

Waoo..! kama jana vile!-26

0

ILIPOISHIA RISASI JUMAMOSI:

“Sasa anti mbona unaficha hicho kipimo? Kusudi unipe majibu ya uongo, si ndiyo ee?” alikuja juu mama Monica.

Hata kabla mpimaji hajamjibu, meseji iliingia kwenye simu ya mama Monica, akaifungua haraka sana ili kuisoma…

“Namshukuru sana Mungu kwa kuamua kuondoka mwenyewe nyumbani kuliko ningekuondoa mimi.”

SASA ENDELEA…

Mama Monica alishtuka sana, akaanza kuogopa hata kuendelea kusubiri tena majibu ya Ukimwi. Alikuwa akitetemeka ghafla…

“Anti, majibu ya hapa Palestina ni ya kweli tupu. Sijaficha lakini pia si vizuri wewe uone mchakato wote wa jinsi kipimo kinavyosoma. Unatakiwa kupewa majibu tu,” alisema yule dada mpimaji.

Mama Monica akili haikuwa pale tena. Alichofanya ni kumtumbulia macho mpimaji kwani akilini alianza kutafuta namna ya kuanza maisha mapya baada ya hali kwa baba Monica kufikia hatua ile…

“Sasa anti upo tayari kupokea majibu ya vipimo vyako vya Ukimwi?”

“Si ndiyo maana nilikuja!”

“Unaweza kuja lakini katika hatua hii ukawa umebadili mawazo…”

“Ningesema.”

“Oke! Kwa hiyo umejiandaa kwa majibu yoyote?”

“Niambie bwana…mbona manenomaneno mengi! Kwani lengo lenu nyie ni kupima na kutoa majibu au kutisha watu kwanza?” mama Monica alikuja juu…

“Anti si hivyo…ni utaratibu wetu… huwezi kumpa majibu mteja bila kumpa ushauri nasaha ili kama ameathirika ajue namna ya kuishi…”

“Kama hajaathirika je?” aliuliza mama Monica…

“Pia tunamshauri namna ya kuishi salama ili asiambukizwe…”

“Kama aliishi salama mpaka akaja kupima mkagundua hana maana yake si alishajua namna ya kuishi salama? Mimi nahisi kama sitakubaliana na majibu yenu!”

“Kwa hiyo tusikupe?”

Mama Monica alijifikiria kwa muda kisha akajifunza kwamba, akisema asichukue ina maana ataondoka akiwa hajui lolote lakini pia akajifunza kwamba, akisema asubiri na majibu yakatoka ya kumuumiza yeye, atakuwa na hali ngumu zaidi…sasa hapo lipi bora..?

“Nipeni,” aliamua mama Monica…

“Oke…sasa anti kulingana na vipimo vyetu hapa ni kwamba majibu yameshapatikana,” alisema mpimaji kisha akasogeza kiti ndani ya meza na kukaa sawasawa…

“Lakini napenda kusema kwamba, si wote wenye Virusi vya Ukimwi wanakufa kwa Ukimwi…unaweza kuwa na virusi lakini maisha yakaendelea tena kwa afya njema kabisa ilimradi kufuata masharti…”

“Una maana gani?” aliuliza mama Monica…

“Maana yangu ni kwamba, wapo wenye Virusi vya Ukimwi lakini wakafa kwa magonjwa mengine, wengine wapo mpaka sasa kwa miaka kumi na zaidi…”

“Kwa hiyo hayo maneno yako unaniambia kwa sababu na mimi nina virusi siyo?”

“Anti mbona una haraka sana?”

“Ungekuwa wewe usingekuwa na haraka?”

“Ningekuwa nayo lakini subira pia ningekuwa nayo…”

“Kwa hiyo kumbe hapa sifanyi kosa kuonesha nina haraka?”

“Hufanyi kosa…”

“Oke, nipe majibu sasa…”

“Anti kipimo kinaonesha umeathirika tayari kwa hiyo….”

Mpimaji huyo hakumaliza kusema kwani mama Monica alikuwa chini ameanguka na kupoteza fahamu…

“Da! Huyu mdada tangu mwanzo alionekana mtata. Inaonekana alikuwa tayari kupima lakini hakuwa tayari kupokea majibu,” alisema yule dada mpimaji akiwaambia wafanyakazi wenzake…

“Kazi tunayo, sijui itakuaje?” alihoji mfanyakazi mwingine mama mtu mzima kiasi.

Walimbeba mteja huyo mpaka nje kwenye fomu na kumpepea huku wakihakikisha usalama wake kimazingira.

Baada ya dakika kumi, mama Monica alizinduka, akakaa. Kulia na kushoto kwake kulikuwa na wafanyakazi wa chumba hicho cha vipimo na ushauri ambao walimtuliza mama Monica kwa maneno mazuri yenye kutia moyo…

“Hili lako si zito dada angu…wewe umeshajijua mshukuru Mungu kuna watu wanaishi hawajui kama wameathirika au la! Wao wasemeje sasa? Kama umejijua naona kama umemaliza kazi,” alisema mfanyakazi mmoja…

“Ni kweli dada‘angu. Halafu ukweli ni kwamba, kama unahisi huwezi kuendelea kuishi kwa sababu umeathirika utakuwa unafanya makosa makubwa. Wewe sasa ni imara…tena utaishi maisha mazuri sana kuliko mtu ambaye hajapima.”

Mama Monica alikohoa kidogo, akafumbua macho bila kuchezesha, akasema…

“Kwa hiyo Magembe ndiyo furaha yake hii… si ndiyo?”

“Magembe! Magembe ni nani dada…ni mumeo?”

“Ndiyo aliyeniambukiza Ukimwi…”

“Kwa hiyo siyo mumeo? Au hujaolewa?”

“Nina mume, baba Monica lakini naye kaniacha leo asubuhi. Hivi hapa nimetoka kuachwa ndiyo nikaja kupima,” alisema mama Monica.

Maneno yake yaliashiria kwamba kichwani hakuwa sawasawa ni kama alikuwa akiropoka tu lolote lile…

“Nitampeleka Magembe polisi,” alisema tena.

Ilibidi wale wafanyakazi wakae kimya, waliamini mama Monica atarejea katika hali yake ya kawaida baadaye.

Kweli, ndani ya dakika kama ishirini tangu azinduke, mama Monica akawa ni yuleyule tena. Alijitambua sasa kiasi kwamba akajutia kama alisema maneno yake ya siri kwa wale wafanyakazi…

“Da! Mimi mama Monica nina Virusi vya Ukimwi! Kweli au naota? Ina maana zile elfu kumikumi za Magembe haya ndiyo majibu yake? Hapana, nitakufa na Magembe,” aliwaza moyoni mwake…

“Naomba mniruhusu niende zangu,” aliomba mama Monica. Akaulizwa kama yupo sawa, akajibu yupo sawa. Alipewa kila kilicho chake, kwa maana ya simu na mkoba wake wa begani.

Aliondoka. Lakini kwa tabia za kibinadamu, kila alipopita aliyemwangalia alihisi sababu ya kuangaliwa ni kwamba amegundulika ana Virusi vya Ukimwi. Kuna ambao alikutana nao macho, yeye akayakimbiza yake pembeni.

Nje ya hospitali hiyo kuna kituo cha daladala, sasa zilipita kama tatu bila kusimama, mama Monica akahisi wanamwacha kwa sababu yeye ana virusi.

Daladala ya nne aliamua kuipungia mkono ili isimame, konda akamjibu…

“Chukua Bajaj bwana, we mgonjwa hutaweza humu.”

JIUNGE NA GLOBAL BRAKING NEWS

GLOBALBREAKINGNEWS100.jpg

Leave A Reply