The House of Favourite Newspapers

Niyonzima siyo wa mchezo mchezo

0

Sweetbert Lukonge | CHAMPIONI| Dar es salaam

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, juzi Jumamosi aliudhihirishia umma wa wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kuwa yeye siyo mchezaji wa mchezomchezo.

Uwezo wake mkubwa wa kutandaza soka uwanjani ndio ulioiokoa Yanga na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Prisons ya jijini Mbeya katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Wakati akiwa benchi kwa zaidi ya dakika 60, Yanga ilikuwa haina ujanja wa kuipenya ngome ya Prisons iliyokuwa ikiongozwa na Nurdin Chona, Jumanne Elfadhili, James Mwasote pamoja na Salum Kimenya.

Lakini alipoingia kuchukua nafasi ya Said Makapu, alibadilisha mchezo na Yanga ikaanza kulishambulia kwa kasi lango la Prisons na baada ya muda ilifanikiwa kupata mabao mawili ambayo upatikanaji wake ulianzia kwake na kuiwezesha kumaliza dakika 90 za mchezo huo ikijikusanyia pointi tatu.

Hali hiyo, pia ilimfanya beki wa kati wa Yanga, Mtogo, Vincent Bossou ashindwe kuzuia hisia zake na kujikuta akimpongeza Niyonzima kutokana na kazi kubwa aliyoifanya uwanjani na kufanikisha upatikanaji wa mabao hayo.

“Niyonzima ni mchezaji mzuri ambaye kila siku huwa natamani kumuona uwanjani akicheza, ni muhimu sana katika kikosi chetu nampongeza kwa kazi nzuri aliyoifanya baada ya kuingia na tukafanikiwa kuibua na ushindi,” alisema Bossou.

Leave A Reply