Nkunku Amalizana na Chelsea, Mkataba Mrefu Kusainiwa Majira ya Kiangazi
NYOTA wa klabu ya RB Leipzig na Timu ya Taifa ya Ufaransa Christopher Nkunku atakuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na klabu ya Chelsea ya nchini Uingereza mara baada ya mchezaji huyo pamoja na klabu ya Chelsea kwa pamoja na RB Leipzig kukubaliana dili la uhamisho lenye thamani ya zaidi ya Euro milioni 60.
Usajili wa Nkunku ambaye ni moja kati ya wachezaji walio katika kiwango cha hali ya juu kwenye ligi ya Bundesliga unaelekea kukamilika ikiwa ni baada ya kukamilisha vipimo vya afya mwezi septemba mwaka huu chini ya uangalizi wa timu ya madaktari kutoka Stamford Bridge.
Nyota huyo kwa sasa ni majeruhi baada ya kuumia katika mazoezi ya timu ya taifa ya Ufaransa iliyokuwa ikijiandaa na mashindano ya Fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea kwa sasa nchini Qatar, hali iliyopelekea nyota huyo kuenguliwa katika orodha ya wachezaji wanaotakiwa kuiwakilisha ufaransa katika mashindano hayo.
Mkataba wa Nkunku na Chelsea unatarajiwa kusainiwa mara moja mapema kabla ya dirisha dogo la usajili la mwezi Januari ingawa yeye atajiunga na klabu yake mpya ya Chelsea majira ya kiangazi mwaka 2023.