The House of Favourite Newspapers

NMB Yamuahidi JPM Kuendelea Kutumia Mifumo ya Kieletroniki

BENKI ya NMB imemuhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kuwa itaendelea kutumia mifumo ya kielektroniki  ili kuwawezesha wateja wa benki kunufaika zaidi na kurahisisha utendaji kuliko kutumia mfumo wa malipo kwa kutumia pesa taslim.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa NMB, Ineke Bussemaker wakati wa ufunguzi wa Kituo cha Kibiashara cha benki hiyo mkoani Mtwara huku akieleza kuwa nia ya NMB ni kuendelea kukua zaidi huku ikitoa suluhu ya vipaumbele vya serikali na kujikita katika ukusanyaji wa mapato ya serikali kwa njia za kielektroniki.

“Kwa kutumia teknolijia mbalimbali, NMB tumewekeza zaidi kwenye kutatua changamoto mbalimbali za wateja wetu na hivyo kutoa fursa za kutumia zaidi njia za benki kuliko kutumia njia za malipo kwa kutumia pesa taslim,” alisema Ineke.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB, Prof. Joseph Semboja alisema kuwa NMB imefanya maboresho makubwa na hivyo kuwa na uwezo mkubwa wa kutoa huduma za kifedha kwa kila Mtanzania na serikali kwa ujumla.

Prof.  Semboja alisema kuwa Serikali kwa sasa inamiliki hisa asilimia 32 ndani ya Benki ya NMB zenye thamani ya zaidi ya Bilioni 430 hivyo kuiwezesha serikali kupata gawio la zaidi ya bilioni 75 ndani ya miaka mitano.

“Kama mkutano mkuu wa wanahisa utakaokaa mwezi Juni mwaka huu, utabariki Kiwango cha gawio, serikali itapata gawio la shilingi Bilioni 16.5 zinazotokana na faida iliyopatikana mwaka 2016,” alisema Prof. Semboja.

Nae Rais Magufuli  aliwapongeza NMB kwa huduma wanazotoa na kutoa wito kwa viongozi wa serikali na wakuu wa wilaya na viongozi waliopo ndaniya serikali kufanyabiashara na NMB kwani serikali inahisa kwenye kwenye benki hiyo na hupata faida kutoka NMB.

“Nikuombe Waziri, toa maelekezo kwa sababu wewe ndo unasimamia pesa, pesa ya serikali ipitie NMB ili nipate gawio kubwa zaidi, wale wengine wanaofanya biashara bila kuifaidisha serikali na kugawana gawio wao kwa wao huku serikali haipati faida yoyote, hatutafanya biashara nao,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli pia aliiomba NMB kushiriki katika kuunga mkono ajenda ya serikali katika kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

“Naomba NMB mshiriki katika kukopesha viwanda hasa viwanda vidogo vidogo na hivyo kuunga Mkono juhudi za serikali katika kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda,” alisema Rais Magufuli.

Comments are closed.