The House of Favourite Newspapers

Nyosso apewa Makambo, Ngassa

KATIKA kuhakikisha anabakiza pointi tatu nyumbani, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amesema tayari amekiandaa vyema kikosi chake kupambana na Yanga.

Kagera Sugar iliyopo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 17, itashuka dimbani kesho Jumapili katika Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera kuivaa Yanga yenye pointi 29 katika nafasi ya pili.

 

Maxime ameweka wazi kuwa amewapa majukumu mazito wachezaji wake wa safu ya ulinzi inayoongozwa na Juma Nyosso kuhakikisha hairuhusu bao na wale wa kiungo na ushambuliaji wapambane kuhakikisha wanapata mabao ya haraka ili wawachanganye wapinzani.

 

Kocha huyo ambaye amewahi kukiri ni ngumu timu nyingine kuchukua ubingwa wa ligi kuu labda kidogo ukizitoa Yanga, Simba na Azam, aliongeza kuwa wanahitaji pointi tatu katika mchezo huo bila kujali matokeo yaliyopita ya wapinzani wao hao.

 

“Maandalizi yetu yanaendelea vizuri na tunamuomba Mungu Jumapili iweze kufika ili tuweze kucheza mechi, nimekiandaa vyema kikosi changu safu zote kuanzia ushambuliaji hadi mabeki ili tuweze kupata mabao ya haraka.

 

“Tunachohitaji ni kuona tunafanikiwa kushinda katika uwanja wetu wa nyumbani kwa kupata pointi tatu, tumejipanga kukabiliana na Yanga bila ya kujali kama wametoka kushinda ama la au watakuja na usafiri gani, tunachohitaji sisi ni ushindi tu,” alisema Maxime.

Khadija Mngwai, Dar es Salaam

Comments are closed.