The House of Favourite Newspapers

NYUMBA AWAMU YA PILI NI ZAIDI YA ZAWADI YA KWANZA

0

ZAWADI ya nyumba ambayo itatolewa kwa mshindi wa kwanza wa Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili inayotarajiwa kuchezwa hivi karibuni, imekuwa ni zaidi ya zawadi ya kwanza ambayo kwa kawaida hupata mtu mmoja, lakini hii kila mmoja anaitaka.

Baadhi ya wasomaji, wakiwemo waliopata ushindi wa pikipiki katika droo ndogo zilizochezeshwa na Global Publishers kwenye Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili, wamezungumzia droo kubwa inayotarajiwa kufanywa hivi karibuni kwa kusema na wao wanatamani kupata zawadi hiyo kubwa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa njia ya simu, washindi hao waliopata ushindi katika droo ndogo ya pili na nne, walisema pamoja na kupata pikipiki katika droo ndogo, lakini nyumba ndicho kitu ambacho kilikuwemo akilini mwao wakati walipoanza kushiriki shindano hilo kwa kukata kuponi zinazopatikana katika magazeti ya Uwazi, Risasi, Amani, Ijumaa na Ijumaa Wikienda.

Agness Lyimo, mkazi wa Tanga aliyeshinda pikipiki katika droo ndogo ya tatu ya Shinda Nyumba Awamu ya Tatu, alisema anashukuru Mungu kwa ushindi wake, lakini bado anaendelea kukata na kutuma kuponi za magazeti hayo, kwani ana matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi katika droo hiyo kubwa.

“Kwa kweli pikipiki inanisaidia sana katika mambo yangu madogomadogo kwa sasa, lakini kila mtu anafikiria kuhusu nyumba, ninatuma kuponi na naomba Mungu nifanikiwe. Niliposhinda pikipiki watu wa hapa Tanga waliniuliza nilifanyaje, sasa mimi sikuwa mchoyo, niliwaambia jinsi nilivyofanya na wao wakaanza kufuata.

“Mimi ni mfuatiliaji sana wa hadithi za Eric Shigongo, kwa hiyo nilikuwa napata vitu viwili kwa wakati mmoja, kwanza ni kusoma hadithi, lakini pia kujaribu bahati yangu, ninashukuru kwa kweli maana Mungu alinipa vyote, sasa safari hii naendelea, siyo mbaya kama nitapata hata dinner set,” alisema Agness.

Kwa upande wake, mshindi wa pikipiki katika droo ndogo ya pili, Victor Mubi, mkazi wa Mwenge jijini Dar es Salaam, alisema tangu ameshinda kifaa hicho, amekuwa akikitumia kwa shughuli zake binafsi, kwani anaogopa kuifanya bodaboda kwa vile hataki kukorofishana na vijana.

“Hii kitu kuweka bodaboda ninataka, lakini naogopa kugombana na hawa vijana, unaweza kumpatia kazi na akashindwa kuleta mrejesho, acha tu niitumie kwa shughuli binafsi. Lakini hapa kwenye nyumba kwa kweli, ninaitamani sana hii zawadi.

“Unajua pale mwanzo, watu hasa hawa nilionao huku, walikuwa hawaamini kama kweli mshindi anaweza kupatikana, sasa baada ya kushinda, nakuambia kila wiki ninaletewa lundo la kuponi hapa ili niwe nawaletea, nakuja hapo Global kila wiki kuleta kuponi.

“Hivi sasa kila mmoja anafuatilia hii droo kubwa na ile simulizi ya mshindi Nelly iliwasisimua watu wengi sana, kila mmoja ana ndoto za kuishinda, niwasihi wasomaji wenzangu tuendelee kukata kuponi, kila mmoja anaweza kujikuta anaibuka mshindi. Pia niwashukuru sana Global Publishers na niwaombe kama ikiwezekana, hizi bahati nasibu ziwe zinakuja kila mara maana zinawasaidia sana wasomaji wake,” alisema Mubi.

Hii itakuwa ni mara ya pili kwa Global Publishers kutoa nyumba katika bahati nasibu, kwani ilifanya hivyo mwaka jana baada ya Nelly Mwangosi wa Iringa kujishindia mjengo wenye thamani ya mamilioni ya shilingi, nyumba ambayo imejengwa jijini Dar.

Kuponi kwa ajili ya Bahati Nasibu hiyo zinapatikana katika magazeti yote ya Global Publishers ambayo ni Ijumaa, Championi, Ijumaa Wikienda, Risasi, Amani na Uwazi na safari hii inadhaminiwa na kampuni ya Premier Bet.

NA MWANDISHI WETU

Leave A Reply