The House of Favourite Newspapers

Nyumba ya Shehe Yavunjwa, Yazua Balaa – Video

0

 

MZEE Sharif Mohammed (75), mkazi wa Vingunguti-Kwamnyamani jijini Dar, ameibua balaa la aina yake kwenye nyumba inayodaiwa ni ya shehe aliyetajwa kwa jina la Abdul Wakati.

 

Mzee huyo anadai kupoteza mali zake nyingi baada ya kuvunjiwa nyumba hiyo na sasa analala nje.

Akitoa kilio chake mbele ya Gazeti la IJUMAA WIKIENDA, Mzee Sharif alidai kuwa, miaka kadhaa iliyopita alichangiwa pesa na Waislam wenzake wakiwemo Waarabu ambapo alimwambia Shehe Wakati amtafutie nyumba ya kuishi na familia.

Alidai kuwa, ni kweli Shehe Wakati alifanya hivyo, lakini sasa amemgeuka na kwenda kuibomoa nyuma hiyo.

 

“Nilianza kuishi kwenye nyumba hii (ipo Vingunguti- Kwamnyamani) tangu mwaka 2016.

“Nakumbuka kuna siku msikitini, nikachangiwa pesa na waumini wakiwemo Waarabu wanne.

“Pesa zilizopatikana zilitosha mimi kutafutiwa nyumba, hivyo pesa hizo alipatiwa Shehe Wakati ambaye naye baada ya saa kadhaa, aliniambia nyumba imepatikana.

 

“Nilipoingia kwenye nyumba hii, Shehe Wakati alinipa karatasi ambazo hazijabadilishwa jina la muuzaji wa nyumba.

“Nakumbuka ilikuwa ni usiku hivyo sikuona sababu ya kuendelea kuuliza sana.

“Niliingia kwenye nyumba na familia yangu huku nikisubiri kumuuliza siku nyingine, lakini akawa ananipiga chenga.

 

“Hivi karibuni ndiyo ametuma watu wamekuja kubomoa nyumba yangu.

“Vitu vyangu vingi vilikuwa ndani, lakini sivioni, mpaka kuku wangu niliokuwa nategemea kuendesha maisha siwaoni.

“Ilibidi nisafirishe familia yangu kwenda Zanzibar, halafu mimi nikabaki hapa ili nihangaikie haki yangu,” alisema Shehe Sharif.

 

IJUMAA WIKIENDA: Kwa nini shehe akuvunjie nyumba?

Mzee Sharif: “Ni majungu kutoka kwa watu wasionipenda mtaani. Watu wanamwambia kuwa nilishawahi kuchukua kuku akiwa hai na kuwatwanga kwenye kinu, jambo ambalo si kweli.

“Baada ya watu kuja kubomoa nyumba, ilibidi niende Ofisi za Katibu Tarafa na Mkuu wa Wilaya (Ilala).

“Nilipofika kwa Mkuu wa Wilaya, alinisikiliza kisha akanipa pesa ya chakula.

“Baada ya hapo Mkuu wa Wilaya alimuita Shehe Wakati na kutupangia siku ya kwenda tena kutusikiliza.”

 

Kwa mujibu wa mmoja wa majirani wa Mzee Sharif aliyeomba hifadhi ya jina alisema; “Inavyosemekana huyu mzee alikuwa analala msikitini na familia yake.

“Baadaye Shehe Wakati alimuonea huruma akamleta hapa na familia yake.

“Kuna kipindi huyu mzee alikosana na mkewe, ikabidi mke na watoto waondoke, hivyo akabaki mwenyewe.

 

“Sasa Shehe Wakati aliyemfadhili, akawa anataka ajenge madrasa na huyo mzee ampe chumba kimoja cha kuishi.

“Lakini wakati mchakato ukiendelea, ndipo huyu mzee akawa anadai anataka kutapeliwa nyumba.

“Ilifika hatua akaandikiwa mpaka barua zaidi ya tano na Kata ya Kiislam, lakini hakwenda.

Mwisho uongozi wa Kata ya Kiislam ukafikia uamuzi wa kujenga madrasa kwa sababu huyu mzee alikuwa anapuuza wito.”

 

IJUMAA WIKIENDA lilifunga safari mpaka kwa mwenyekiti wa mtaa huo, Said Mwaikala ambaye alikiri kulifahamu sakata hilo na kwamba mzee huyo anatakiwa alipwe vitu vyake vilivyopotea kwani utaratibu uliotumika kubomoa si sahihi.

“Wiki mbili zilizopita nilipokea taarifa za kubomolewa kwa nyumba hiyo na Mamlaka ya Masjid Taqwa maarufu kama Msikiti wa Bungoni kupitia Shehe Wakati.

 

“Nikiri kwamba kitendo kilichofanyika hakikuzingatia haki, lakini nishauri pia mamlaka zinazohusika kuangalia njia stahiki zinazotakiwa kuchukuliwa ili kila upande upate haki yake,” alisema mwenyekiti huyo.

Baada ya gazeti hili kusikiliza maelezo yote hayo, lilimtafuta mlalamikiwa ambaye ni Shehe Wakati ili kujibu tuhuma zilizoelekezwa kwake ambapo alikuwa na haya ya kusema;

 

“Nakumbuka mwaka 2016 alikuja huyo mzee akiwa na mke wake na watoto watano.

“Walifikia upande wa nyuma wa msikiti wetu, wakawa wanaishi hapo katika mazingira magumu sana. Ilibidi niwaulize matatizo waliyo nayo, wakaniambia wamefukuzwa walikokuwa wakiishi.

“Niliwaonea huruma, ikabidi tupitishe mchango msikitini, zikapatikana shilingi 260,000.

 

“Lengo lilikuwa tumpangishie nyumba ya kuishi na familia yake angalau kwa miezi sita.

“Kwa kuwa nilikuwa na nyumba pale Vingunguti (Kwamnyamani), nikaona bora nitumie fursa hiyo kumpangishia.

“Kwa hiyo ulifanyika utaratibu wakawa wanaishi pale. Miezi sita ilipokwisha hakulipa kodi, lakini sikumuondoa akaendelea kuishi.

 

“Baadaye nilipohitaji eneo langu, nilimwita na kumweleza, lakini Mzee Sharif hakutoa ushirikiano.

“Kutokana na ile nyumba kuwa imeanza kutengeneza nyufa, nilihofia inaweza ikaleta madhara hivyo ilibidi nianze kutoa mabati na zile kuta ambazo zilikaa vibaya kisha nikaondoa matofali, hicho ndicho kilichotokea,” alisema Shehe Wakati huku akionesha vithibitisho vyote vya umiliki wa nyumba hiyo.

STORI: MEMORISE RICHARD, DAR

Sakata lake shuhudia hapa!

Leave A Reply