The House of Favourite Newspapers

OKWI ANANUKA FEDHA, NDIYE GHALI BONGO

0

 

Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi.

KUANZIA leo Jumatano, zitakuwa zimebaki takribani siku 11 kabla ya usajili wa dirisha kubwa Tanzania Bara halijafungwa ambapo timu kadhaa zimekuwa zikiimarisha vikosi vyao. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetoa siku 52 kwa timu za Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili kujenga vikosi vyao kwa kufanya usajili kuanzia Juni 15 mpaka Agosti 6, mwaka huu.

 

Tangu kufunguliwa kwa dirisha hilo, kumekuwa na vurugu kwa wachezaji kuhama timu moja kwenda nyingine huku tukishuhudia baadhi ya timu zikigombania mchezaji mmoja na kila upande ikihitaji saini yake. Katika vurugu hizo, kuna wachezaji wamesajili kwa madau makubwa na kuwafanya kuwa wachezaji ghali katika soka la Bongo kwa sasa. Championi ambalo tangu siku ya kwanza ya usajili limekuwa makini kufuatilia mchakato huo, linakuletea tathmini ya kile kilichofanyika mpaka sasa na kubainisha nani amesajili kwa mkwanja mrefu.

 

EMMANUEL OKWI

Mganda huyu mpaka sasa ndiye mchezaji aliyenunuliwa kwa dau kubwa akijiunga na Simba akitokea Villa ya Uganda, ambapo mpaka mchakato wake unakamilika wa kujiunga na timu hiyo amechota kiasi cha milioni 115. Fedha hizo zilizotolewa na Simba kumpa Okwi zinamfanya kuwa mchezaji ghali kwenye usajili huu.

Haruna Niyonzima.

HARUNA NIYONZIMA

Bado mashabiki wa Yanga wanauguza donda la kuondokewa na nyota wao kipenzi, Haruna Niyonzima ambaye ameikacha timu hiyo na kutua kwa wapinzani wao Simba kwa usajili uliowakosti dola 50 (sawa na milioni 115 za Kitanzania) ambapo fedha hizo zinamfanya aingie daraja moja na Okwi.
Mnyarwanda huyu nae ni mmoja wa wachezaji nyota ambao wamesajiliwa kwa dau kubwa katika dirisha hili la usajili akiwa sambamba na Mganda, Emmanuel Okwi.

Mshambuliaji mpya wa Yanga,Ibrahim Ajibu.

IBRAHIM AJIBU

Ndiye mchezaji ghali kwa upande wa wachezaji wa ndani ya nchi baada ya klabu ya Yanga kutumia milioni 70 kukamilisha mchakato wa kumtoa Simba na kumshusha kwenye kikosi chao. Ukimuondoa Okwi na Niyonzima, mshambuliaji huyu naye anafuata kwenye orodha ya wachezaji waliovuta mkwanja mnene kwenye kipindi hiki cha usajili.

ROSTAND YOUTHE

Ameletwa ndani ya Yanga kurithi mikoba ya makipa, Deogratius Munishi ‘Dida’ na Ally Mustapha ‘Barthez’ ambao kwa msimu ujao hawataonekana na kikosi hicho. Barthez ameenda Singida United na Dida yeye yupo kwenye hatua za kutua Afrika Kusini. Kipa huyu raia wa Cameroon naye hayupo mbali kwenye orodha ya wachezaji ghali kwenye msimu huu baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuwatumikia mabingwa hao wa ligi kuu msimu uliopita baada ya kutia kibindoni milioni 40.

MBARAKA YUSUPH

Straika ambaye ameanza msimu mpya kwa majanga
bada ya kupigwa kisu ‘operesheni’ ambayo itamuweka nje kwa wiki sita ambapo muda huo utamfanya akose mechi za awali za timu yake mpya ya Azam. Mpaka usajili wake unakamilika wa kujiunga na kikosi hicho cha Wauza lambalamba, Mbaraka aliyepachika kambani mabao 12 msimu uliopita amevuna kiasi cha milioni 40.

 

SHOMARY KAPOMBE

Beki kisiki wa Azam, Shomary Kapombe kwa msimu ujao ataonekana akiwa ndani ya uzi wa Simba baada ya kukubali kujiunga na timu hiyo kwa mkataba wa miaka miwili. Kapombe naye ni miongoni mwa wachezaji ghali katika dirisha hili la usajili baada ya kutia kibindoni milioni 35 zilizofanikisha usajili wake kutua ndani ya timu hiyo. Wachezaji wengine ghali kwenye dirisha hili la usajili ni pamoja na kipa Aishi Manula (kutoka Azam kwenda Simba, milioni 35), kiraka, Erasto Nyoni (milioni 30), John Bocco (milioni 35) na kipa Emmanuel Mseja (aliyetoka Mbao kwenda Simba milioni 25).

STORI: SAID ALLY, CHAMPIONI JUMATANO

Leave A Reply