The House of Favourite Newspapers

P Funk: Msishangae Siku Nikiokoka

0

PAUL Matthysse almaarufu kama P Funk, Halfani, Majani, Kinywele Kimoja, ni mtayarishaji mkubwa wa muziki na mmiliki wa Studio za Bongo Records zilizopo Bamaga jijini Dar.

Ni mtayarishaji mkongwe ambaye amekuwa na maajabu yake kwenye historia ya Bongo Fleva.

Katika kazi zake, alifanikiwa kumpandisha kwenye chati Juma Nature na kuwa nembo ya Bongo Fleva.

 

Amefanya kazi na mastaa karibia wote wakubwa wa kitambo hicho kama Solo Thang, AY, Zay B, Sista P, Mike T, Profesa Jay, Afande Sele, Ferooz na wengine wengi unaowajua wewe. Mwaka 2019, P Funk Majani alimuibua Rapcha, rapa mdogo anayechipukia kwenye muziki Afrika Mashariki akiwa na uwezo wa kurap na kuimba.

 

Rapcha ndiye msanii pekee aliye chini ya usimamizi wa P Funk. Kwa sasa anafanya poa na ngoma yake ya Amen akiwa na mkongwe wa gemu ya Bongo Fleva, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’.

 

OVER ZE WEEKEND imepiga stori kibwena na P Funk katika mahojiano maalum (exclusive interview) ambapo amefunguka mengi ikiwemo ishu ya lebo yake ya Bongo Records na maisha binafsi;

 

OVER ZE WEEKEND: Historia ya Lebo ya Bongo Records ikoje?

P FUNK: Lebo ya Bongo Records ilianza kabla ya Sound Solution, iliundwa mwaka 1994 na tulianza kama kundi. Tukatoa project chini ya lebo ikiwa na Nembo ya Bongo Records. Sound solution iliundwa mwaka 1999 ikiwa kama studio ya booking, nilikuwa na recording studio na recording lebo.

 

OVER ZE WEEKEND: Bongo Records ni lebo kubwa, lakini zimekuja lebo nyingine kama Wasafi na King’s Music, je, unadhani nini chachu ya kuwepo kwa lebo hizi?

 

P FUNK: Ni mifumo tu na watu wengi wanapenda kusema wana records lebo, lakini wanajiendesha kama recording studio. Kuwa na records lebo, si kuwa na wasanii wako studio, mnarekodi halafu mnajiita lebo. Lebo ina vitu vingi, lazima umsimamie msanii kwa kila kitu mwanzo-mwisho. Hivyo inachukua mtaji mkubwa kuwa na lebo.

 

OVER ZE WEEKEND: Ni vitu gani umeviona kwa Rapcha kama msanii wako?

P FUNK: Kwa kifupi ana kipaji. Vipaji viko vingi, lakini Rapcha ana muonekano na bado mdogo. Kuna wengine wana vipaji, lakini umri umekwenda, kwa huyu safari ndiyo imeanza maana mimi naangalia miaka kumi mbele, anakuja kuwa mkubwa kama MwanaFA, AY au Profesa Jay. Huwezi kuimba nyimbo mbili au tatu ukajilinganisha na watu kama wale.

 

OVER ZE WEEKEND: Kuna watu ambao wamekuwa wakizungumza kuwa ni ngumu sana wewe kurudi kwenye gemu hasa kutokana na mfumo wa maprodyuza jinsi ulivyo sasa, je, wewe kama mkongwe, unalizungumziaje?

 

P FUNK: Kwa bahati mbaya, naweza kusema mpaka leo tumezembea katika kudhibiti vipato kwenye upande wa muziki. Kuna sekta kama kuwa balozi, kupata streams, sekta ambayo inatakiwa iwape wasanii pesa ni mirabaha, mpaka sasa ni miaka mingi imepita.

 

OVER ZE WEEKEND: Unadhani kama mirabaha ingekuwepo, nani angefaidika zaidi?

P FUNK: Kama WCB wangekuwa wanapata milioni 570 kila mwaka kwa mirabaha, hivyo watu wangepata kipato cha ziada.

OVER ZE WEEKEND: Unahisi ni hatua gani ichukuliwe?

 

P FUNK: Kwanza wabadilishwe watu walioko pale (COSOTA), kwa sababu miaka nenda rudi tutasikia visingizio vilevile.

OVER ZE WEEKEND: Unadhani kinachowafelisha ni nini?

P FUNK: Kinachofelisha ni kutokuwa na umoja wa wasanii, kwa sababu mkiwa na sauti moja, mkapiga kelele kila mtu atasikiliza.

 

OVER ZE WEEKEND: Kwa mujibu wa Rais Magufuli, Basata na Cosota vimekuwa kwenye sekta moja, je, unadhani inaweza kusaidia kwenye suala la mirabaha?

P FUNK: Upande mmoja unaweza kusema inapunguza ugumu, kinachohitajika ni uongozi ambao uko serious na kazi zake maana muziki ni biashara.

 

OVER ZE WEEKEND: Watu watarajie nini kutoka kwako na Profesa Jay maana mlikuwa kwenye mgogoro na sasa mko freshi?

P FUNK: Tutarudi kama zamani maana tumetengeneza historia tangu enzi za Zali la Mentali, Ndiyo Mzee na nimetengeneza album zake nne.

 

OVER ZE WEEKEND: Mwaka jana uliposti kwenye ukurasa wako wa Instagram ukiwajulisha mashabiki kuhusiana na kutengeneza album yako ya mwisho, ni kwa nini?

P FUNK: Nimetengeneza album zaidi ya hamsini, maana kwenye muziki wetu watu hawazingatii sana album na hii ni kutokana na suala la kipato. Album ni ya Rapcha.

 

OVER ZE WEEKEND: Album ya Rapcha itatoka lini?

P FUNK: Itatoka baada ya single mbili au tatu, japo mwanzo tulikuwa na wazo ambalo jamii ya Kibongo haijawahi kuona.

 

OVER ZE WEEKEND: Ngoma ya Rapcha na Lady Jaydee imepokelewa vizuri na mashabiki, idea ilitoka wapi?

P FUNK: Idea ya kumshukuru Mwenyezi Mungu ilitoka kwangu, umri unavyozidi kwenda nimeanza kuwa karibu na Mwenyezi Mungu na kuabudu zaidi. Kuna wimbo tulitoa kama ya Nick Mbishi, wimbo ulikuwa unaitwa Amen na nyingine za kumshukuru Mungu hivyo msishangae siku nikaja kuokoka.

 

OVER ZE WEEKEND: Kwa mtazamo wako, isingekuwa kolabo ya Rapcha na Lady Jaydee, Rapcha ilikuwa afanye kolabo na nani?

P FUNK: Lady Jaydee tulimtaka mwanzo ila ikawa kimya tukashangaa, sekta ya kumuweka Lady Jaydee ilikuwa ni ya kurap.

 

OVER ZE WEEKEND: Master Jay ameanguka kwenye kura za maoni, je, unamwambiaje?

P FUNK: Siasa siyo Bongo Star Search, ajue hilo.

OVER ZE WEEKEND: Uliwahi kuwa jaji kwenye BSS, lakini kwa sasa umesema unaangalia vipaji kwenye mitandao ya kijamii, kwa nini?

 

P FUNK: Unajua vijana wengi hawajui kutumia fursa, hakuna kitu ambacho kimeturahisishia kujitangaza kama mitandao ya kijamii. Tumia fursa hata kwenye kazi zako, muda wa mtu na hisia zake za kazi maana unaweza ukapokea kazi kulingana na ulivyo kwa siku hiyo.

 

OVER ZE WEEKEND: Mameneja kama Said Fela na Babu Tale, wote umefanya nao kazi na wako menejimenti nyingine, unadhani kwa nini tunakosa menejimenti imara kwa wasanii wengine?

P FUNK: Unajua Nasibu (Diamond) ana akili sana, anajua kufanya kazi na mameneja kama wale. Wasanii wengi wanapata nafasi ila sekta ya kipato ukiwa mlafi na mroho, watu wanakukimbia na hawawezi kukufanyia kazi bure.

 

OVER ZE WEEKEND: Zamani kulikuwa na upendo sana kwenye huu muziki tofauti na sasa, je, inaweza ikawa ni sababu ya wewe kutodili na wasanii wengine au kuamua kuwekeza kwa Rapcha?

P FUNK: Unajua Lebo ya Bongo Records tulivyoanza, tulikuwa wasanii wengi na nilikuwa najigawa kotekote. Tuliishi kama familia tunazunguka, ila kulikuwa na wivu baina ya wasanii wenyewe. Kwa Rapcha nilitafuta wasanii nikiwaomba tumshike mkono ila wengine hawataki hata kusikia.

 

OVER ZE WEEKEND: Unadhani nini kilikurudisha nyuma?

P FUNK: Nilirudi nyuma kwa sababu ya kipato, nilikuwa nafanya kazi kama punda, nafanya kazi za bure. Kipato kilikuwa kinatoka kwenye shoo na nilikuwa sipati pesa na chanzo cha kurudi nyuma ni kung’ang’ania cha zamani, namaanisha kufunga ukurasa na kuanza upya.

MAKALA: HAPPYNESS MASUNGA

Leave A Reply