The House of Favourite Newspapers

Papii Kocha Afunguka Kurudi Kivingine Kwenye Muziki

0

PAPII Kocha ni mtoto wa nguli wa muziki wa Dansi nchini; Nguza Viking au Babu Seya na amerejea mtaani na bendi mpya, Tukuyu Sound.

 

Kwamba, Papii na baba yake walikuwa habari ya mjini kweli kwa ubora wao huko nyuma, lakini Papii amerudi kivingine na sasa amekumbana na changamoto ya kuwa na watu wapya na mashabiki wapya.

 

Ni wakati wa kuvuna pesa baada ya kusota jela kwa muda mrefu. ‘Enewei’ hakuna jambo gumu kama mtu aliyekuwa kileleni akashuka na kutaka kurudi tena kileleni. Angalia ubora wa Papii katika kuchezea sauti na katika utunzi, uimbaji, sasa anajitahidi kurudi ‘on top’.

 

Kama sauti, majina, utunzi na bado anapumua, hakuna kitakachomshinda. Natamani kusikia kionjo cha ‘Baba na Mwana Tunaimba na Kucheza’.

Yule Seya wa viwalo ambaye alifanya jiji litikisike na runinga zipate moto huku masikio yakishindwa kuchoshwa na mirindo ya sauti zao. Na zaidi pesa za watu zikiteketea kwa viingilio kwenye shoo zao ule muda ambao Papii aliibeba dansi kwenye mabega yake.

 

Kwa kiwango ambacho siyo tu hajui atoe wimbo gani, lakini ameelewa aanzie wapi na ameanzia kwenye Tukuyu Sound Band. Hapa ndipo akili za watu wenye upeo wa burudani zilipohitajika, lakini ardhi nayo ina yake yenyewe. Imeendelea kumeza akili zote zenye akili duniani.

Papii Kocha ametoka kimuziki kwa kushirikiana na Kalala Junior, mtoto wa Hamza Kalala ambaye naye pia ni mwanamuziki wa Dansi.

 

Pengine ‘taimingi’ ilikuwa mbovu baada ya kutoka jela. Kwa sasa inabidi itumike akili iliyovuka akili ya kawaida ya binadamu kumrudisha Papii Kocha katika ubora wake na naamini kwa kuunda bendi hiyo mambo yatakuwa moto.

 

Anaweza kuwa ana rundo la nyimbo na hazina ya mashairi kichwani, lakini tazama wale kaka zake aliowaacha nyuma yake pale FM Academia wana hali gani?

 

Kama wao waliokuwa uraiani pia wamekata ringi kisanii itakuwaje kwake? Lakini Mungu ana maajabu yake.Yawezekana muziki wa Dansi kwa jumla wake umeyumba, lakini hiyo si sababu kwa kuwa Papii alishaanza kuwa mtu wa masauti tayari kabla ya kwenda jela.

 

Alikuwa na ‘singo’ zake kibao tu. Alianza kukimbiza kitambo akiwa ‘solo atisti’. Alijitegemea bila kutegemea uwepo wa bendi wala kikundi, lakini hii leo ana Bendi ya Tukuyu Sound, tutagemee makubwa.

 

Kuna watu wanalazimisha upende kitu bila kulazimishwa ubora na utimamu wa kile wafanyacho ndiyo sumu inayokupindua kutoka katika Dunia hii kwenda Dunia nyingine.

 

Papii alifanya wale machizi wa Hip Hop wamhusudu katikati ya mizuka ya Bongo Fleva ile ngumungumu. Papii hakuhitaji kufanya uhuni ili apendwe na wahuni.

 

Hakuhitaji apake nywele rangi na kutoboa masikio kama siyo kusuka ili totozi zimuelewe. Na hata sasa amekuwa yuleyule alivyo na kuendelea kuteka watu kisanaa kuanzia mitaani hadi kwenye vipindi redioni.

 

Uliza watu.Papii anabaki kuwa mfano wa mtu aliyetendewa ukatili na muda. Tunatenganishwa kinguvu na kipaji cha ajabu kwa sababu ya muda. Alianza kukimbiza akiwa bado kinda sana kwenye Bendi ya FM Academia.

Jina lake likazidi kupaa kisanaa kadiri siku zilivyosonga.

 

Miaka ya 2000 mwanzoni alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa Smooth Vibes, chanzo cha THT.Wacha maisha yaendelee.

 

Lakini muda ni kitu cha msingi sana katika kila jambo. Hakuna binadamu aliyefanikiwa kwenye kila jambo bila kujali muda. Kila jambo ni wakati.Papii na baba yake, Babu Seya wametoka jela, wapo mtaani tangu mwaka 2017, lakini bado wamekosa ‘linki’ na mtaa.

 

Siku anaachiwa huru, watu mbalimbali ndani na nje ya nchi walipokea kwa shangwe kuachiwa huru kwa wanamuziki hao maarufu wa muziki wa Dansi nchini, Nguza Viking (Babu Seya) na mwanawe, Johnson Nguza (Papii Kocha) baada ya kuwa gerezani kwa miaka 13 na miezi minne.Wawili hao walitoka Gereza la Ukonga saa 12:00 jioni na kulakiwa na umati wakiwamo marafiki na ndugu zao.

 

Rais Dk. John Magufuli, aliwaachia huru wafungwa hao ikiwa ni sehemu ya wafungwa 8,157 waliopata msamaha kwa kuachiwa huku wafundwa 666 wakiwa ni wale wenye vifungo vya maisha kama ilivyokuwa kwa Babu Seya na Papii Kocha. Rais alitumia Ibara ya 45 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayotoa mamlaka kwa Rais kutoa msamaha kwa wafungwa.

 

“Sisi sote ni binadamu na hata mimi huwa namwomba Mungu anisamehe, ingawa sisi wanadamu ni wagumu kusamehe.

 

Hivyo natangaza msamaha kwa familia ya Nguza Viking maarufu kama Babu Seya na watoke leo,” alisema Rais Magufuli.Tulifurahi walipotoka jela na kuungana nasi, lakini wameungana nasi kiupeo tu na kihisia, kisanaa walikuwa bado wapo nje ya muziki wa Dansi. Walishindwa kurudi kwenye kilele chao, tuliwakaribisha kwa shangwe ya kuonana tena.

 

Ila bado tunapaswa tuwakaribishe mtaani kisanaa hasa baada ya kuundwa kwa Tukuyu Sound Bend ambayo ilizinduliwa Jumamosi iliyopita katika Ukumbi wa Mawasiliano Park uliopo Ubungo jijini Dar.

MAKALA: ELVAN STAMBULI

⚫️ Kwa UPDATES zote, Download GLOBAL APP: ⚫️ ANDROID:http://bit.ly/38Lluc8 ⚫️ iOS:https://apple.co/38HjiCx

WOOW! HARMONIZE AMSAPRAIZ KAJALA KWA GARI JIPYA ALILOMNUNULIA, TAZAMA KAJALA ALIVYOLIPOKEA..

Leave A Reply