The House of Favourite Newspapers

Penzi Kabla Ya Kifo-10

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA
“Edson….Edson…nakupenda Edson…nahitaji uwe wangu Edson…” alisema Elizabeth huku machozi yakimbubujika.Endelea…

Hakukuwa na kitu kilichobadilika, kama siku nyingine, usiku wa siku hiyo alikuwa na mawazo tele, nyumbani hakukukalika, kila wakati alimfikiria mwanaume huyo kiasi kwamba alihisi angechanganyikiwa na mawazo aliyokuwa nayo.

Kesho yake alichokifanya ni kuelekea dukani akanunua maua, kadi za mapenzi CD ambayo aliingiza nyimbo nzuri za mapenzi huku kukiwa na kipande cha karatasi kilichobeba ujumbe mzito.

Hakuwa na kingine alichoweza kukifanya, kama kumwambia kwa mdomo, alishindwa, hivyo aliona njia nyepesi ni kuufikisha ujumbe wake kwa kutumia maandishi na vile vitu vingine alivyonunua.

Siku hiyohiyo baada ya kukamilisha kila kitu, akachukua gari lake mpaka katika ofisi ya Edson na kumwachia sekretari kile alichokuwa amekibeba kwa ajili ya mwanaume yule aliyeuteka moyo wake kisha kuondoka.

Hakujua ni kitu gani kingetokea, hakujua Edson angechukulia vipi kile alichokifanya, kwake, aliona kwamba ile ndiyo ingekuwa njia nyepesi ya kuuteka moyo wa mwanaume huyo ambaye alikuwa na mke na mtoto wake mdogo, kwa Elizabeth hilo wala hakujali.
****
“Kuna mzigo wako bosi.”
“Kutoka wapi?”

“Kwa Elizabeth!”
“Waoo! Yaani kishamaliza kushona?”
“Mmh! Sijui!”

Alichokifanya sekretari yule ni kuchukua ule mfuko uliokuwa na urembo mwingi kisha kumpa bosi wake. Edson akauchukua na kuanza kuelekea nao ndani. Alichokijua yeye ni kwamba mle ndani kulikuwa na nguo aliyomwambia Elizabeth amshonee kwa ajili ya mkewe.

Alipofika ofisini, akaufungua ule mfuko na kuanza kutoa vitu vilivyokuwemo ndani. Kwanza akashtuka, hakuamini kile alichokiona kwa mara ya kwanza, kitu ambacho kilikuwa cha kwanza kutoka ndani ya mfuko ule yalikuwa ni maua mekundu mawili.

Akashtuka, akayaangalia maua yale vizuri, alionekana kama mtu aliyeshangazwa na hali ile, hakuishia hapo, akatoa vitu vingine, akakutana na kadi, alipoifungua tu, akasoma ujumbe uliokuwepo, ulikuwa ni wa kimapenzi.
“Mungu wangu!”

Kitu kingine kukitoa kilikuwa ni kipande cha karatasi, akakichukua kisha kukifungua. Kilikuwa na ujumbe mfupi ulioandikwa kwa mwandiko mzuri wa kike, maneno yaliyopangiliwa, uliosomeka:

Edson….
CD imejieleza kila kitu.
Elizabeth.

Hapo ndipo alipoingiza mkono wake ndani ya ule mfuko, akakutana na CD moja ambayo aliichukua kisha kuichomeka katika mlango wa laptop yake na kuchukua hedifoni na kuanza kusikiliza.

CD ile ilikuwa na nyimbo kadhaa zilizoimbwa na waimbaji wengi wa Kimarekani, kulikuwa na Wimbo wa Fly Without Wings wa West Life, Just Go wa Lionel Rich na Never Let You Go wa Justin Bieber.

Edson alizisikiliza nyimbo zile zote ambazo aliambiwa kwamba zilikuwa na ujumbe kuhusu kile alichokuwa akikihisi moyoni mwake juu yake. Nyimbo zote hizo zilikuwa na ujumbe mkali wa mapenzi, alipozisikiliza, alihisi kitu cha tofauti moyoni mwake.

Hakikuwa mapenzi, ilikuwa ni chuki kubwa kwa msichana huyo, kwa kile alichokifanya, aliona kama alivuka mipaka kwani hakutegemea msichana kama Elizabeth kufanya jambo hilo ambalo aliliona kama kuingiliwa katika maisha yake na wakati alikuwa na mke aliyempenda kuliko wanawake wote.

“Hebu subiri kwanza, kumbe hanijui,” alisema Edson kwa hasira.
Hakutaka kupoteza muda, hapohapo akachukua simu yake, moyo wake uliwaka kwa hasira, alijiona ghafla akimchukia Elizabeth, japokuwa alikuwa msichana maarufu, mwenye fedha na mrembo mno lakini hiyo haikuwa sababu ya kumfanya kumsaliti mke wake.

Simu ile ikaita mpaka ikakata, hasira zikampanda zaidi. Alichokifanya ni kutoka ofisini kwake, hakutaka kukaa, kazi zisingefanyika hata mara moja, alichokitaka ni kumfuata msichana huyo nyumbani kwake.

“Kumbe huyu hanijui, sasa subiri….” alisema Edson huku akiwa na hasira kali kama mbogo aliyejeruhiwa. Akawasha gari na kuanza kuelekea nyumbani kwa Elizabeth aliyekuwa akiishi hukohuko Mbezi Beach.

Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia wiki ijayo.

Leave A Reply