The House of Favourite Newspapers

Penzi Kabla ya Kifo-23

0

Msichana bilionea, Elizabeth na mpenzi wake wapo nchini Ujerumani walipokwenda kumuuguza mtoto Glory. Wanapofika huko, Elizabeth anapigiwa simu na mwanaume aliyewahi kumpenda sana, Rasheed ambaye anamwambia kuwa anataka kuonana naye.
SONGA NAYO…

Elizabeth alimwambia ukweli Rasheed kwamba katika kipindi hicho hakuwa nchini Tanzania bali alikuwa nchini India ambapo baada ya muda fulani angeondoka kuelekea nchini Ujerumani kwa ajili ya matibabu ya mtoto Glory.
Alichokisema Rasheed ni kwamba hata naye angekwenda huko Ujerumani, kitu pekee alichotaka kumwambia msichana huyo ni jinsi alivyompenda, suala hilo halikuwa la kuzungumzia kwenye simu, walitakiwa kuonana na kuzungumza ana kwa ana.

Kwa upande wa hospitalini, huo ndiyo kwanza ulikuwa mwaka wa kwanza na waliambiwa kuwa walitakiwa kusubiri kwa miaka mitano kwa Glory kupona. Kilikuwa kipindi kirefu mno lakini hawakuwa na jinsi. Katika kila hospitali waliyokuwa wamepitia, waliambiwa kwamba Glory asingeweza kupona, angeendelea kuwa vilevile mpaka pale atakapofariki dunia.

Wakati Elizabeth akipata barua pepe kutoka kwa Rasheed alikuwa chumbani amekaa peke yake, alikuwa akiangalia mambo mengine kwenye mtandao, alitaka kuona jinsi dunia ilivyokuwa ikiendelea kwa wakati huo.
Hapo ndipo alipoona barua pepe kutoka kwa Rasheed, alichokifanya ni kuifungua na kuanza kuisoma. Kwanza alishtuka, hakushtuka kupokea barua pepe bali kitu kilichomfanya kushtuka ni kuona akiambiwa kwamba alitakiwa kuonana na Rasheed.

Hapo ndipo uzuri wa mwanaume yule ulipoanza kumjia kichwani mwake, alimkumbuka vilivyo, mara ya kwanza kukutana naye tu alihisi kwamba alikutana na malaika kwani mwanaume huyo alikuwa mzuri mno.
Huku akimfikiria Rasheed, hapo ndipo picha ya James ilipoanza kumjia kichwani mwake, alihisi moyo wake ukiwa kwenye mapenzi mazito kwa James kiasi kwamba hakutaka kumuona mwanaume yeyote yule akiliingilia penzi lake.
Alichokifikiria ni kwamba inawezekana mwanaume huyo alitaka kuonana naye kwa ajili ya kuzungumzia biashara kwani ndivyo ilivyokuwa kila alipokuwa akikutana na mabilionea wengine.

Baada ya siku mbili Rasheed akafika nchini Ujerumani ambapo moja kwa moja akapanga sehemu nzuri ambayo angeweza kuonana na Elizabeth ili kumwambia ukweli kile kilichokuwa kikiutesa moyo wake kwa kipindi hicho.
Mawasiliano yalikuwa yakiendelea kama kawaida, siku iliyofuata, walichokifanya ni kuonana katika Mgahawa wa Mamarita uliokuwa katikati ya Jiji la Munich. Kitendo cha kumuona Elizabeth tu, akahisi moyo wake ukiridhika, kila alipokuwa akimwangalia, aliuona uzuri aliokuwa nao kipindi cha nyuma ukiwa umeongezeka zaidi.
“Umependeza sana, uzuri wako umeongezeka maradufu,” alisema Rasheed huku akimwangalia Elizabeth kimahaba.

“Nashukuru sana.”
Walizungumza mengi mpaka pale Rasheed alipoona kwamba huo ndiyo muda maalumu kwa ajili ya kulitoa dukuduku lake. Kwanza akaanzia mbali, tangu alipomuota msichana huyo, uzuri aliokuwa nao na jinsi walivyokuwa wakifurahia pamoja.
“Sijaelewa unamaanisha nini? Ni ndoto au kuna lingine?” aliuliza Elizabeth.
“Ndiyo! Lingine lipo.”
“Lipi?”
“Ninakupenda Elizabeth!” alisema Rasheed kwa sauti ndogo.
“Unanipenda mimi?”
“Ndiyo! U msichana mrembo mno, nimeshindwa kuvumilia na nimeamua kukwambia ukweli na ndiyo maana nimesafiri kutoka mbali kuja kukwambia hili,” alisema Rasheed.

Elizabeth alikaa kimya kwa muda, akaanza kumwangalia Rasheed usoni, alionesha kile alichokuwa akikisema, alimaanisha kutoka katika mtima wa moyo wake, alichokuwa akikisikilizia ni jibu kutoka kwa msichana huyo mrembo.
Elizabeth hakuwa na haraka ya kujibu, alitulia tu huku akichukua glasi ya juisi na kunywa. Uso wake ukaanza kuonesha tabasamu pana lililompa matumaini Rasheed.
“Umechelewa Rasheed.”
“Hapana! Sijachelewa, nimekuja muda muafaka.”
“Umechelewa. Ninaye mtu nimpendaye, ungeniambia tangu kipindi kile, nahisi ningekukubalia, bali niliporudi nchini Tanzania tu, kila kitu kikabadilika baada ya kukutana na James,” alisema Elizabeth.
“James ndiye nani?”
“Mwanaume wangu mpya.”
“Ana fedha kama mimi? Ana akili kama mimi?”
“Rasheed! Fedha si mapenzi, ukiwa na fedha ni rahisi kununua ngono ila si rahisi kununua mapenzi, unaweza kununua hata dawa, ila huwezi kununua uhai,” alisema Elizabeth huku akionesha tabasamu pana.
“Elizabeth…..” aliita Rasheed huku akionekana kuumia moyoni mwake.
Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake wiki ijayo.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply