The House of Favourite Newspapers

Penzi Kabla Ya Kifo-5

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA

Alikuja kupatwa na usingizi saa saba usiku, muda wote huo alikuwa akiendelea kumfikiria tu. Alipoamka saa tatu asubuhi, kitu cha kwanza kabisa ni kumpigia simu Candy na kumtaka kufika nyumbani kwake.

SONGA NAYO…

 Ninataka unisindikize sehemu,” alimwambia rafiki yake huyo.

“Wapi tena?”

“Kule kwa jana, ninataka kuonana na yule mwanaume leo hiihii,” alisema Elizabeth.

“Mmh!”

“Mbona unaguna.”

“Tutamuona vipi?”

“Wewe twende tu,” alisema Elizabeth.

Elizabeth alikuwa rafiki yake mkubwa na ndiye aliyemuweka mjini, Candy hakuwa na jinsi, akakubaliana naye na hatimaye safari ya kuelekea Afrikana kuanza.

Hawakutaka kutumia gari walilotumia jana yake, wakabadilisha gari kwani lile lilijulikana mno kwa kuwa hakukuwa na mtu aliyekuwa akiendesha gari la thamani nchini Tanzania zaidi yake, gari lile likawa nembo, kila lilipoonekana, watu walijua kwamba mahali hapo kulikuwa na Elizabeth.

Hawakuchukua muda mrefu, wakafika walipokuwa wakienda. Alichokifanya Elizabeth ni kuteremka na kisha kuwafuata wanaume kadhaa waliokuwa pembezoni mwa bahari ili kuwauliza.

“Za saa hizi!” aliwasalimia.

“Aaah! Elizabeth!”

“Ndiyo mimi! Samahanini kama nitawapotezea muda wenu.”

“Hakuna tatizo mrembo!”

“Ninauliza ni nani anaishi nyumba ile pale,” alisema Elizabeth huku akiinyooshea kidole nyumba ile.

“Kuna jamaa fulani hivi anaitwa Edson, mmiliki wa ile hoteli kubwa ya Amazon Five ya kule Upanga, yeye ndiye anaishi mle.”

“Ana mke?”

“Ndiyo na mtoto mmoja.”

“Sawa. Ofisi yake ipo wapi?”

“Ipo pale kwenye Jengo la Ubungo Plaza, pia ni meneja wa Shirika la Ndege ya Flying 15, ukifika hapo, ukimuulizia, utaambiwa alipo,” alisema kijana mmoja.

“Umesema anaitwa Edson?”

“Ndiyo! Edson Gwamanya.”

“Nashukuru!”

Hakutaka kuwaacha vijana wale hivihivi kwani walionekana kuwa msaada mkubwa mno kwake, hivyo akawapa fedha ili wagawane. Hiyo haikutosha, walichokiomba ni kupiga naye picha, hilo wala halikuwa tatizo, akapiga nao picha na kuondoka huku akiwaacha wakiwa na furaha mno.

Kidogo moyo wake ukaridhika, kitendo cha kuambiwa mahali alipokuwa akifanyia kazi Edson kilimridhisha, hakutaka kuchelewa, alichokifanya ni kuelekea huko huku akiwa na furaha mno.

Walitumia dakika arobaini mpaka kufika katika jengo refu la Ubungo Plaza, wakateremka na kuanza kuelekea ndani. Kila mtu aliyemuona Elizabeth, alibaki akimkodolea macho, msichana huyo alikuwa na mvuto mkubwa mno, kila alipopita, watu walikuwa bize kumwangalia tu.

“Samahani! Ninamuulizia Edson Gwamanya,” alisema Elizabeth, alikuwa akizungumza na msichana mmoja ndani ya jengo hilo.

“Yupo ghorofa ya saba,” alisema msichana yule na kumpa maelekezo zaidi ya kufika huko. Wakaenda kusubiri lifti iwapeleke juu.

Lifti ilipofika chini, ikafunguka, wakapanda na kwenda juu. Moyo wa Elizabeth ukaanza kudunda kwa nguvu, hakujiamini kabisa, alijikuta akianza kutetemeka kwani kukutana na mwanaume huyo kwa mara ya pili kulimtia hofu moyoni mwake.

Lifti ilipofika ghorofa ya saba, ikasimama na kuteremka. Macho yao yakatua katika mlango ulioandikwa Flying 15, wakaanza kupiga hatua kuufuata mlango huo, muda wote huo mapigo ya moyo wa Elizabeth yalizidi kudunda zaidi, hakuonekana kujiamini hata mara moja.

“Subiri kwanza,” alisema Elizabeth, alimsimamisha Candy.

“Kuna nini?”

“Mbona naogopa hivi hivi?”

“Jamani! Hebu jipe nguvu, tuumalizie huu mkia, tushamla ng’ombe mzima,” alisema Candy, Elizabeth akashusha pumzi nzito.

Wakapiga hatua mpaka walipoufikia mlango ule na kisha kuufungua, mtu wa kwanza kukutana naye alikuwa sekretari ambaye walimsalimia kisha kukaa katika viti vilivyokuwa mahali hapo.

Kipindi chote sekretari yule alibaki akimwangalia Elizabeth, alikutana na msichana aliyekuwa supastaa, aliyependwa na wanawake wengi, kila alipomtazama, alijisikia raha moyoni mwake.

Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia wiki ijayo.

Leave A Reply