The House of Favourite Newspapers

Penzi lisiloisha     055

0

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kutoa figo yake moja na kumpa Anna ambaye alikuwa na matatizo ya figo zake kushindwa kufanya kazi. Anaamua pia kukataa kusomea upadri akiamini kwamba akimaliza shule, ataoana na Anna ili waishi kama mume na mke.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa Anna, wazazi wa msichana huyo wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi Jafet na wazazi wake. Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani.

Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William. Mapenzi yao yanaendelea na baadaye Anna anaanza kuona dalili zisizo za kawaida. Anapoenda kupima anagundulika ni mjamzito lakini kijana huyo anaonesha kukasirishwa na hali hiyo, anataka wakautoe ujauzito huo.

Anna anaamua kutoroka kurejea nyumbani kwao, Mwanza bila Jafet kujua chochote lakini akiwa anaelekea uwanja wa ndege, anakutana na Jafet katika mazingira ambayo hakuyategemea.

Je, nini kitafuatia?

SONGA NAYO…

“Jafet! Jafet!” sauti ya msichana iliyoonekana kutokuwa ngeni masikioni mwake, ndiyo iliyomshtua Jafet aliyekuwa amezama kwenye mazungumzo ya kawaida na wanachuo wenzake.

Harakaharaka akageuka nyuma na kutazama sauti hiyo ilikokuwa inatokea, Jafet akashindwa kuyaamini macho yake kwa alichokuwa anakiona. Ilibidi afikiche macho yake, akihisi labda yupo kwenye ndoto ya kusisimua.

“Anna! Ni wewe?”

“Ni mimi Jafet! Naomba unisamehe kwa yote yaliyotokea, naomba nikufafanulie kilichotokea,” alisema Anna huku akitokwa na machozi kwa wingi.

“Jafet! Huyu ni nani kwani? Twende darasani tunachelewa kipindi,” sauti ya msichana mwingine mrembo, ambaye naye alikuwa amevaa kama Jafet kuonesha kwamba walikuwa wakisoma pamoja, ilimzindua kutoka kwenye lindi la mawazo machungu, msichana huyo akamshika mkono Jafet na kuanza kumvuta, Anna akawa ni kama haamini alichokuwa anakiona.

“Suleikha! Hebu ngoja kwanza niongee na huyu dada, tunafahamiana.”

“Jafet! Umeanza lini kusimama na wasichana barabarani? Isitoshe muda wa kuanza kipindi umefika, twende bwana.”

“Suleikha ‘please’, nipo chini ya miguu yako.”

“Ok! Nakupa dakika mbili lakini lazima na mimi nisikie mnazungumza nini.”

“Lakini Suleikha tumeanza lini kuchungana kiasi hiki?”

“Jafet! Nikwambie mara ngapi kwamba nakupenda mwenzio? Kwa nini unanitesa lakini?”

“Sikutesi Suleikha, mimi na wewe bado hatujawa wapenzi sasa kwa nini unipangie watu wa kuzungumza nao?”

“Jafet unanijibu mimi hivyo? Kwa hiyo kwa sababu ya huyu kinyago ndiyo leo unaniona sina maana? Ahsante! Ahsante sana,” alisema Suleikha huku akilia.

Msichana huyo shombeshombe mwenye uzuri wa kipekee kuanzia kwenye sura yake, macho yake meupe, mrefu kiasi, mwenye nywele nyingi zilizoangukia mgongoni na umbo linalokaribia kufanana na namba nane, aliondoka eneo hilo akiwa anatokwa na machozi kwa wingi mithili ya mtu aliyepokea taarifa za msiba.

Japokuwa ni kweli Jafet alikuwa bado hajamkubalia ombi lake la siku nyingi la kutaka wawe na uhusiano wa kimapenzi, alikuwa akimpenda mno kijana huyo kiasi kwamba ilifika mahali wanachuo wenzao wengi walikuwa wanahisi kwamba huenda tayari wawili hao ni wapenzi kwani Suleikha alikuwa akimganda Jafet kama ruba.

Kila mahali alipokuwepo Jafet, Suleikha naye alikuwepo, kuanzia wakiwa darasani, wakiwa kantini mpaka kwenye hosteli aliyokuwa akiishi Jafet. Japokuwa siku za mwanzo Jafet alikuwa mgumu sana kumruhusu msichana huyo kumzoea kiasi hicho, alijikuta akishindwa kuendelea kushikilia msimamo wake kutokana na jinsi msichana huyo alivyokuwa akimuonesha mapenzi ya dhati.

Ukaribu wao ukazidi kuongezeka baada ya Jafet kurejea kutoka Mwanza alikomshuhudia Anna akitoka uwanja wa ndege akiwa ameongozana na mwanaume ambaye bila hata kuuliza alijua moja kwa moja kwamba alikuwa na uhusiano naye wa kimapenzi.

Kitendo cha Suleikha kuondoka huku akilia, kilimuumiza mno Jafet kwa sababu japokuwa ni kweli hawakuwa kwenye uhusiano rasmi wa kimapenzi, msichana huyo hakuwahi kumfanyia jambo lolote baya kustahili maumivu ya kiasi hicho. Harakaharaka Jafet akamkimbilia na kumsimamisha.

“Suleikha jamani, kwa nini unakuwa hivyo? Naomba dakika mbili tu nizungumze naye, wewe simama hapahapa unisubiri, nakuomba usijisikie vibaya,” alisema Jafet huku akimpigapiga msichana huyo mgongoni kama ishara ya kumbembeleza. Kitendo hicho kilisaidia sana kumtuliza Suleikha, akafuta machozi yaliyokuwa yanamtoka na kusimama pembeni kama Jafet alivyomuelekeza.

Harakaharaka Jafet akarudi mpaka pale Anna alipokuwa amesimama, akishuhudia kila kitu kilichokuwa kinaendelea. Kitendo cha kumuona Jafet akiwa anambembeleza msichana mwingine, ambaye kwa kumtazama alikuwa mrembo zaidi yake, kilimuumiza mno Anna, akajihisi kama amechomwa na kitu chenye ncha kali kwenye moyo wake.

“Samahani kwa usumbufu uliojitokeza, enhee nakusikiliza.”

“Kwani yule ni nani?”

“Anaitwa Suleikha, nasoma naye na ni rafiki yangu kipenzi.”

“Mh! Kwani siku hizi unasomea nini?”

“Nasomea udaktari hapa Muhimbili.”

“Nilikuwa nakuomba unisamehe kwa yote yaliyotokea Jafet, nahitaji kuzungumza na wewe nikueleze kilichotokea, tafadhali niko chini ya miguu yako.”

“Huna cha kunieleza Anna, mwanzo nilikuwa nahisi labda ulilazimishwa kwenda mbali na mimi kama mlinzi wenu alivyoniambia lakini nilikushuhudia mwenyewe kwa macho yangu siku unarudi kutoka huko ulikokuwa, nimekuona Uwanja wa Ndege wa Mwanza ukitoka na mwanaume, tena mkiwa mmekumbatiana kimahaba, huna cha kuniambia tena Anna,” alisema Jafet huku akionesha kutokuwa na hata chembe ya masihara.

Kauli hiyo ilimshtua mno Anna kwani hakuwahi kuhisi kwamba siku aliyokuwa anawasili uwanja wa ndege, Jafet alikuwepo eneo hilo. Bila kujali watu wengi waliokuwa wakipita barabarani, Anna alipiga magoti huku akilia mithili ya mtu aliyepokea taarifa za msiba, akimsihi Jafet amsamehe na kumpa nafasi ya kumsikiliza kwa sababu alikuwa kwenye matatizo makubwa.

“Anna, naomba unielewe, nimesimama hapa kwa sababu ya heshima yako tu, vinginevyo nisingesimama. Isitoshe sasa hivi ni muda wa kuingia darasani, kwa heri,” alisema Jafet huku akigeuka na kumuacha Anna amepiga magoti palepale chini. Akatembea harakaharaka mpaka pale Suleikha alipokuwa amesimama, wakaondoka na kuzamia upande wa madarasa ya chuo hicho, wakamuacha Anna akiendelea kulia kwa uchungu.

“Kwani yule ni nani mbona anakulilia?”

“Ni stori ndefu, nikipata muda nitakusimulia kila kitu usijali,” alisema Jafet wakati wakipandisha ngazi za kuingilia darasani.

“Dada! Unanichelewesha, utaniongeza pesa za kukusubiria?” dereva teksi aliyekuwa amevuka barabara kumfuata Anna, ndiye aliyemzindua msichana huyo kutoka kwenye lindi la mawazo machungu. Anna akasimama na kushtuka kugundua kuwa kuna watu wengi walikuwa wamekusanyika kumzunguka, kila mmoja akimshangaa kwani halikuwa jambo la kawaida.

Anna alisimama pale alipokuwa amepiga magoti, akajifuta machozi na kamasi na kumuomba yule dereva teksi amsaidie kumvusha ili wakaendelee na safari yao ya kuelekea uwanja wa ndege, dereva akamshika mkono na kumvusha.

Wakaingia ndani ya teksi huku Anna akiendelea kulia kwa kwikwi, wakaondoka eneo hilo na kuwaacha watu wengi wakiendelea kuulizana maswali yaliyokosa majibu. Anna aliendelea kulia kwa uchungu huku akijilaumu sana, wakati mwingine akimlaumu William na wakati mwingine akiwalaumu wazazi wake kwa kilichotokea.

Bado akilini mwake aliendelea kubabaika kufikia uamuzi wa kurudi nyumbani kwao, Mwanza au kuahirisha safari na kujaribu kwa mara nyingine kutafuta nafasi ya kuzungumza na Jafet. Mpaka wanawasili uwanja wa ndege, bado Anna hakuwa na majibu kama aendelee na safari au arudi kwenda kuzungumza na Jafet.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

Leave A Reply