The House of Favourite Newspapers

Waoo…! Kama Jana Vile!-23

0

ILIPOISHIA RISASI JUMATANO:

“Unajua baba Monica, hawa wanawake bwana wanataka ufuatiliaji kama huu ulioufanya wewe,” baba Salama alisikika akimwambia baba Monica…

JIACHIE SASA…

Mungu wangu…Mungu wangu, kumbe baba Monica yupo. Itakuaje sasa? Mimi si nimeachika? Kisa Magembe na vihela vyake. Loo!” alisema mama Monica. Hakuwa na jinsi tena zaidi ya kuondoka eneo hilo. Hakuona sababu ya kuendelea kusikiliza wakati kila kitu kilishakuwa wazi.

Badala ya kwenda kwenye biashara yake alirudi nyumbani, akafungasha kila kilicho chake, kwa maana ya nguo, yaani magauni, vitenge, kanga, suruali, sketi kisha akachukua na viatu vyake vyote mpaka sendoz, pia akambebea nguo mwanaye, Monica…

“Dada mimi naondoka zangu. Sitaishi tena na baba Monica, Mungu akubariki sana kwa kumlea mwanangu kwa muda wote huo,” alisema mama Monica huku akionekana ana haraka sana wakati anatoa mizigo nje ili asikutwe na mumewe…

“Kwani kuna nini dada?” msichana wake wa kazi alimuuliza kwa mshangao…

“Atakuja kukwambia baba Monica.”

Kule nje, mama Monica alikodi Bajaj, akaondoka zake kwenda kwa shangazi yake aishie Tabata Matumbi ambako alisimulia mkasa wake wote kwa shangazi huyo huku akimwaga machozi.

Shangazi yake alimshangaa sana, lakini hakumwambia neno wala kumshauri vinginevyo.

“Lakini shangazi pia inabidi niende Sinza pale Hospitali ya Palestina, tulikubaliana na huyo Magembe tukutane kwa ajili ya kupima Virusi vya Ukimwi,” alisema.

“Sawa, we nenda. Majibu utaniambia,” alisema shangazi mtu huyo.

Mama Monica aliondoka mwenyewe, akaanza na kwenye biashara yake mama lishe ambapo wasichana wake wa kazi za pale walimshangaa sana kumwona mama Monica akiwa katika sura ya kutoka kulia. Macho mekundu tena yalivimba lakini hawakumuuliza kwa vile ni bosi wao.

Baada ya kupangapanga mambo yake, saa nne mama Monica alianza safari ya kwenda Palestina huku akimpigia simu Magembe…

“Mimi nimepanda daladala sasa, wewe uko wapi?” aliuliza mama Monica.

“Nipo kazini mama Monica,” alisema Magembe ambaye awali alitamani sana asiipokee simu hiyo…

“Sasa itakuaje Magembe?” alihoji mama Monica huku akianza kulia hali iliyomshangaza Magembe mpaka akahisi kwamba, huenda mwanamke huyo alishakwenda kupima mahali mwenyewe na amepata majibu mabaya…

“Sasa sikia mama Monica, mimi niko fiti sana tu. Ila wewe una wasiwasi sana. Sasa kwa kuwa nimebanwa sana na kazi, wewe nenda kapime, mimi na wewe tutakwenda wote ili ukanishuhudie,” alisema Magembe.

“Sawa bwana…sawa tu Magembe,” alisema mama Monica na kukata simu.

Alimwachia maswali kibao Magembe, lakini naye hakujali, aliendelea na kazi zake licha ya kwamba kwa mbali alikuwa akihofia kila alipomkumbuka kaka wa mama Monica.

***

Mama Monica alikuwa kwenye foleni ya kuingia kwenye chumba cha kupimia Ukimwi ndani ya hospitali hiyo. Watumishi wake, walionekana kuzoea hali ya kuwapima watu kwani walikuwa wakiingia na kutoka na kuzungumza kwa sauti ya juu.

Mapigo ya moyo wa mama Monica yalikuwa yakimwenda kwa kasi. Hapo alibakiza mtu mmoja aliyekuwa ndani ya chumba cha kupimia. Akitoka huyo, anaingia yeye…

“Hivi nikikutwa na virusi itakuaje? Nitaishije kwanza? Ina maana mimi nitaitwa mwathirika. Afadhali basi ningepata maambukizi kwa njia nyingine kama wengine, lakini kisa mapenzi?! Mh!”

Mara, jina lake liliitwa, akaingia, akakaribishwa kwenye kiti. Dada mmoja anayepima alimtupia jicho mama Monica kisha akampa salamu.

Baada ya salamu, mpimaji akamuuliza…

“Anti umekuja kupima Virusi vya Ukimwi siyo?”

“Ndiyo.”

“Umeshauriwa na mtu au wewe mwenyewe?”

“Mimi mwenyewe.”

“Kuna nini kimekufanya uamue kupima?”

“Hakuna.”

“Una mume?”

“Ninaye.”

“Mbona hujaja naye?”

“Amesafiri. Lakini mbona maswali mengi sana jamani?”

“Ni kawaida anti.”

“Ah! Mi naona usumbufu kwangu, hujui tu! Kama mnanipima nipimeni nijue moja.”

“Oke, sawa anti. Je, uko tayari kupokea majibu ya aina yoyote yale?”

“Lakini yasiwe ya uongo,” alidakia mama Monica.

Ilibidi yule mpimaji acheke kwanza kwani aliamini amekutana na mteja wa aina yake siku hiyo.

“Hapa anti kila kitu ni cha kweli. Kipimo ni hiki na damu tutaichukua kwenye mkono wako kwa kutumia kifaa hiki huku wewe mwenyewe ukiona. Sawa?”

“Haya niwaone kwanza.”

Mama Monica alitakiwa kunyoosha mkono, akachomwa na kitu chenye ncha kali, damu zikatoka, zikachotwa na kipimo, kikawekwa kwenye meza.

Yule mpimaji aliweka boksi kubwa mbele ya kipimo ili mama Monica asione kile kipimo kinavyosoma majibu…

“Sasa anti mbona unaficha hicho kipimo? Kusudi unipe majibu ya uongo, si ndiyo ee?” alikuja juu mama Monica.

Hata kabla mpimaji hajamjibu, meseji iliingia kwenye simu ya mama Monica, akaifungua haraka sana ili kuisoma…

“Namshukuru sana Mungu kwa kuamua kuondoka mwenyewe nyumbani kuliko ningekuondoa mimi.”

 

Je, unajua nini kiliendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Risasi, Jumatano ijayo.

Leave A Reply