Punguzo la Bei Kili Marathon mwisho leo

WAKATI ukiwa umesalia mwezi mmoja na nusu kabla ya kufanyika kwa mbio maarufu za Kilimanjaro Premium Lager Marathon, punguzo la bei kwa wanaoshiriki mbio za kilometa 42 na 21 linakwisha leo Januari 14, 2020.

 

Taarifa iliyotolewa na waandaaji wa mbio hizo ilisema usajili umekuwa ukiendelea kwa njia ya mtandao na Tigopesa na kuwataka washiriki waendelee kujisajili leo kwa wingi kabla ya saa sita usiku ili waweze kupata punguzo hili la asilimia 20.

 

Kwa sasa bei hizo ni 15,000 kwa mbio hizo mbili na elfu tano kwa mbio za kilomita 5 maarufu kama fun run. Lakini kuanzia kesho itakuwa Tsh 20,000. Hii ni kwa watanzania na raia wan chi za Afrika Mashariki tu.

 

Washiriki wanajisajili kwa kupitia www.kilimanjaromarathon.com na kwa Tigopesa kwa kubonyeza *149*20#.

 

Mkurugenzi wa Mbio hizo nchini, John Bayo alisema usajili utafungwa Februari 16, 2020 au pale ambapo idadi maalumu ya washiriki inayotakiwa kwa mbio zote tatu (Kilimanjaro Premium Lager Km 42, Tigo km 21 na Grand Malt Km 5) ikifikiwa ili kuhakikisha kuwa mbio hizo zinaendana na viwango vya Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF) ili kuhakikisha usalama unazingatiwa.

 

Kwa mujibu wa Bw. Bayo, hii pia itahakikisha washiriki wanafurahia mbio hizo bila ya msongamano na pia kutoa nafasi kwa waandaaji waweze kutoa huduma zinazotakiwa katika njia ya mashindano na sehemu ya kumalizia pia.

 

Kwa wageni wakazi au wenye vibali vya kuishi na kufanya kazi na wale wa nchi za SADC watalipa USD 35 kwa km 42 na 21 na USD 5 kwa km 5 kuanzia Oktoba 1, 2019 hadi Januari 14, 2020 lakini kuanzia Januari 15, 2020 hadi Februari 16, 2020 wanaojisajili watalipa USD 45 kwa km 42 na 21 na USD 5 kwa km 5.

 

Washiriki wa kimataifa watalipa USD 70 kwa km 42 na 21 na USD 5 kwa km 5 kuanzia Oktoba 1, 2019 hadi Januari 14, 2020 na kuanzia Januari 15 hadi Februari 16, 2020 watalipa USD 85 kwa km 42 na Km 21 na USD 5 kwa km 5.

 

Washiriki pia wamekumbushwa kuhusu vituo vya kuchukulia namba zao za ushiriki ambapo kwa Dar es Sallaam ni Mlimani City kuanzia February 22-23, 2020, Arusha ni Hoteli ya Kibo Palace kuanzia Februari 25-26 na Moshi ni Hoteli ya Keys kuanzia Februari 27-28. “Washiriki watatakiwa kujitambulisha na kuthibitisha kuwa wameshalipia kabla ya kukabidhiwa namba zao,” ilisema taarifa ya waandaaji.

 

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli, alisema muamko ni mkubwa na wanategemea kuwa mbio za mwaka huu zitafana zaidi na kuwataka watanzania waendelee kufanya mazoezi ili kujihakikishia nafasi nzuri na zawadi zibaki nyumbani.

 

Kilimanjaro Premium Lager imekuwa imdhamini mkuu wa mbio hizi tangu kuanzishwa kwake miaka 18 iliyopita.

Naye Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael alisema usajili kwa kupitia Tigo Pesa umepata muamko mkubwa kwani kwa sasa hakuna usajili wa makaratasi.

 

Wadhamini wa mbio za Kilimanjaro Marathon 2020 ni Kilimanjaro Premium lager, Tigo, Grand Malt Kilimanjaro Water, TPC Limited, Simba Cement, Barclays Bank na watoa huduma rasmi ni Kibo Palace Hotel, Keys Hotel, GardaWorld Security, Precision Air na CMC Automobiles.

 

Mashindano ya Kilimanjaro Marathon yanayoandaliwa na Wild Frontiers na kuratibiwa kitaifa na kampuni ya Executive Solutions, yanatarajiwa kufanyika Machi 1, 2020 katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.


Loading...

Toa comment