The House of Favourite Newspapers

Queen Darlin Amchana Tanasha!

 

Siku chache baada ya mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kumtambulisha nyumbani kwao mchumba wake Tanasha Donna Oketch, dada wa msanii huyo Mwanahawa Abdul ‘Queen Darleen’ ameibuka na kubwatuka meneno makali dhidi ya wifi yake huyo.

 

Maneno hayo makali yamekuja mara baada ya Queen kubanwa maswali kuhusu uwepo wake katika tukio la utambulisho wa Tanasha, uliofanyika hivi karibuni kwenye nyumba mpya anayoishi Diamond au Mondi iliyopo maeneo ya Mbezi Beach-Kwa Zena jijini Dar.

 

IJUMAA LANASA UBUYU

Kwenye tukio hilo la utambulisho, Ijumaa Wikienda lilibaini uwepo wa ubuyu kwani karibu wale ndugu wote wa karibu wa Diamond walikuwepo isipokuwa Queen.

 

Walioonekana kumkaribisha Tanasha ndani ya mjengo huo wa kifahari siku hiyo ni mama Diamond, Sanura Kassim ‘Sandra’, Juma Lokole (rafiki wa familia) na Esma Khan (dada’ke Mondi).

 

IJUMAA WIKIENDA MZINGONI

Baada ya kuona Queen, dada wa Mondi ambaye wanashea baba hayupo katika tukio hilo lililoambatana na chakula cha jioni, Ijumaa Wikienda liliingia mzigoni kutaka kujua kulikoni?

 

MAJIBU YA UCHUNGUZI

Baada ya kuzungumza na vyanzo mbalimbali vilivyopo ndani ya familia ya Mondi, ilidaiwa kuwa Queen hakuwepo kwenye ‘mnuso’ huo kwa sababu ‘haziivi’ kivile na Tanasha. “Unajua Queen yeye katika wanawake wote wa Diamond, hakuna mwanamke ambaye anamkubali zaidi kama anavyomkubali Zari.

 

“Yeye chaguo lake ni Zari na si mwanamke mwingine. Ndio maana unaona hana taimu na Tanasha, Esma na mama yake wao hawana shida, wanaunga mkono mwanamke yeyote ambaye Mondi atawatambulisha,” alieleza mmoja wa watu wa karibu na familia ya Mondi.

 

MAJIBU YA QUEEN YATHIBITISHA

Ili kuweza kujiridhisha kuhusu Queen kutoivana na wifi yake mpya Tanasha, Ijumaa Wikienda lilimwendea hewani mrembo huyo, alipopatikana alithibitisha kutoivana na Tanasha.

 

Alipoulizwa kutokuwepo katika hafla hiyo, Queen alianza kwa kuhoji kuna ulazima gani kuwepo kwani Tanasha ni mtu wa kawaida tu. “Kwani Tanasha si mtu tu kama walivyo watu wengine?”

TUCHEKECHE KIDOGO JIBU LAKE

Jibu hilo lilionesha dhahiri kwamba endapo Queen angekuwa na maelewano mazuri na mrembo huyo, angemnenea mazuri na pengine kama alikuwa na udhuru wa kibanadamu ulimfanya ashindwe kutokea siku hiyo, angeusema.

 

TUENDELEE NA MAZUNGUMZO…

Alipoelezwa na Ijumaa Wikienda kuwa alipaswa kuwepo kwa kuwa ile ilikuwa ni shughuli rasmi ya kifamilia, Queen alisema hakuona umuhimu. “Kwa nini tungandanegandane? Si nilishamuona kule Kenya?” alihoji Queen kwa sauti ya ukali kidogo.

 

AMKANA DIAMOND

Kama hiyo haitoshi, alipobanwa zaidi katika mazungumzo hayo, licha ya kutoeleza moja kwa moja kwamba hamkubali Tanasha, alitoa kauli iliyoashiria kuvunja undugu wake na Mondi.

 

“Niwepo wakiwa pamoja wanaenda kutambulishana kwani mimi mwanafamilia? Mimi si ndugu wa Diamond, mimi ni msanii wake tu,” alisema Queen Darleen na kukata simu na hata alipopigiwa tena hakupokea.

 

TUJIKUMBUSHE

Penzi la Diamond na Tanasha limeibuka mwishoni mwa mwaka jana huku likionekana kutokubalika na baadhi ya wanafamilia akiwemo Queen.

 

Kabla ya Tanasha, Diamond alimwagana na mrembo wa Kiganda Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ aliyezaa naye watoto wawili ambaye anaonekana kukubalika na Queen pamoja na wafuasi wengi wa Diamond mitandaonI.

 

Stori: Shamuma Awadhi, Dar

Comments are closed.