The House of Favourite Newspapers

Rage: TAKUKURU Wamenikuta Msikitini – Video

0

MBUNGE wa zamani wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage amesema ameshtushwa na kitendo cha taarifa kusambazwa kuwa amekamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wakati kiuhalisia si kweli.
Akizungumza na kipindi cha Front Page mapema leo, Rage alisema kilichotokea ni kwamba yeye aliitwa kwa ajili ya mahojiano na kwamba alihojiwa na kisha kuruhusiwa kuondoka zake.

Alisema, Takukuru walikuwa wamepata malalamiko dhidi yake hivyo wakamuita na akawapa ufafanuzi mmoja baada ya mwingine.
“Ni kwamba mimi Takukuru hawajanikuta mahala popote natoa hela wala hawajinukuta popote na wanachama wa CCM,” alisema Rage.

 

Akizungumzia kilichotokea siku ya tukio, Rage alisema maofisa wa Takukuru walimkuta nyumbani kwake Tabora wakamueleza kuwa wanamhitaji kwa ajili ya mahojiano.

 

“Nilikuwa nafuturu, wakaniambia alhaji wewe malizia futari halafu tutazungumza, nawashukuru waliniacha nimalize futari kisha tukaenda ofisini kwao kunihoji. Waliniambia wameletewa malalamiko; kwanza nimempa gari Katibu wa CCM Mkoa kwenda kwenye mkutano Dodoma nikawaambia mimi sijampa katibu gari na hilo gari si langu.

 

“Pili kuna malalamiko yamekuja hapa, toka tarehe 16 mwezi wa tatu, wanasema nimefanya kikao cha kampeni katika kata ya Tambukareli. Nikawauliza iweje tangu tangu tarehe 16 mje kunihoji leo siku 73 zimepita?” alihoji.

 

Akizungumzia hatma ya sakata hilo, Rage alisema walipokamilisha mahojiano hayo walimruhusu aondoke zake.
“Bahati nzuri ilipofika asubuhi saa mbili wakaniachia, wakaniambia shehe nenda upo huru na tukikuhitaji tutakuita. Nikawaambia mimi naishi Dar es Salaam, naweza kwenda hata sasa? Wakaniambia hata nje ya nchi nenda,” alisema.

 

Rage alisema kwa mtazamo wake anaona kinachotokea kwa sasa pengine ni mbunge aliyopo Tabora Mjini (Emmanuel Adamson Mwakasaka) kuwa na hofu na yeye sasabu ni mzawa wa Tabora.

 

“Mimi kwetu Tabora na bahati mbaya mbunge ambaye yupo sasa hatokei Tabora sasa nahisi labda ana hofu na mimi, kwanza mimi sijatangaza nia mpaka sasa wala sijaamua kwamba nitagombea au sitagombea. Napima upepo kwanza,” alisema Rage.
Rage alikuwa mbunge wa jimbo la Tabora Mjini mwaka 2010 hadi mwaka 2015 alipobwagwa na Mwakasaka.

 

Stori: Erick Evarist

 

Leave A Reply