The House of Favourite Newspapers

Ally Keissy: Rais Magufuli Aongoze Miaka 20 – Video

0

 

MBUNGE wa Nkasi (CCM), Ally Kessy amesema kwa jinsi ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli ametekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) basi anashauri aongezewe miaka 20 zaidi ya kuongoza.
Kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais anatakiwa kutumikia nafasi hiyo kwa kipindi kisichozidi miaka 10.

 

Akizungumza mapema leo kwenye kipindi cha Front Page cha +255GlobalRadio, Kessy alisema kwa upande wake haoni tatizo kusema hivyo na kwamba muda utakapofika wa kufanya hivyo basi utafanyika mchakato wa kukusanya kura za maoni ya wananchi.

 

“Ningemshauri Rais aongozewe muda hata miaka 20. Tutapiga tu ya maoni ya wananchi tuone wanataka au hawataki. Rais amekamilisha Ilani ya CCM kwa asilimia 80. Angalia kule ziwa Victoria daraja kubwa linajengwa, ma-flyover, madege amenunua, barabara za lami, mradi wa Julias Nyerere kuna nini tena,” alisema Kessy.

 

Kwenye mahojiano hayo, Kessy alisema kutokana na jinsi ambavyo amekuwa mstari wa mbele kupigania masuala ya ubadhilifu katika jimbo lake, amekuwa akiendelea kupata vitisho mara kwa mara kwa wakandarasi waliokuwa wakitaka kufanya ubadhilifu huo.

 

Alisema, hajali sababu haohao ndio wamekuwa wakimchafua kisiasa lakini hajali kwani anajivunia mtaji wa wananchi wa kawaida ambao amewaletea maendeleo makubwa katika jimbo lake.

 

“Vitisho bado vinaendelea, baadhi ya watumishi na wakandarasi ndio wanakuwa na chuki na mimi. Baada ya Rais kufanya ziara, wamekuja wakaguzi kupitia miradi yote niliyobainisha ubadhilifu na taarifa ipo kwa CAG,” alisema Kessy.
Aidha, Kessy alizungumzia kuhusu suala la haki katika majimbo na kwamba kuna baadhi ya majimbo hayastahili kuwepo kwani yanainyonya Serikali.

 

“Tusioneane. Ukubwa wa majimbo lazima uwe sawa, kuna wengine wana majimbo makubwa, wengine madogo. Kuna watu wana kata 3, wengine kata 28 na wote mnapata posho sawa. Majimbo yapunguzwe, tunaingiza hasara tu kwa Serikali,” alisema Kessy na kuongeza.

 

“Ndio maana Rais tangu ameingia madarakani kuongeza majimbo amekataa, kuongeza kata amekataa ameona ni upuuzi tu.”
Kuhusu kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020, Kessy alisema anatarajia kuendelea kutetea jimbo hilo kama wananchi watampa ridhaa na kwamba hana wasiwasi kwani ametimiza wajibu wake kama mbunge.

 

“Mimi nakwambia kwa wananchi wa kawaida mimi nalala usingizi kabisa. Nimeingia Nkasi kuna vijiji havikuwa na umeme lakini sasa hivi vijiji vyote vina umeme, mpaka visiwani. Wananchi wa kawaida sina shida nao ni hawa watumishi tu wachache wanaopita kunichafua ambao hawana nguvu yoyote,” alisema.

 

Mbunge huyo machachari aliwaonya baadhi ya wasanii ambao wanamuimba vibaya Rais Magufuli.
“Rais ni kama Mungu wa Dunia, unamchezeaje. Nilishamwambia mheshimiwa Rais anikabidhi mimi hata wiki tatu nitawanyoosha hawa wanaomuimba vibaya Rais,” alisema mbunge huyo.

 

Stori: Erick Evarist

 

 

Leave A Reply