The House of Favourite Newspapers

Raha Iliyoje! Wema, Wolper Sasa Kupata Watoto

HATIMAYE mchongo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kuanza kutoa huduma ya kupandikiza mimba kuanzia Januari, mwakani (2020), umeelezwa kuwa mkombozi kwa mastaa wa Kibongo.

 

Hatua hiyo imeelezwa kuwa kicheko kwa mastaa wengi wakiwemo waigizaji Wema Isaac Sepetu, Jacgueline Wolper, Blandina Chagula ‘Johari’ na wengine wengi ambao sasa wanaamini watapata watoto kwa njia ya upandizaji pale Muhimbili.

 

Wakizungumzia ishu hiyo, mastaa Wema na Wolper walionesha kufurahishwa na jambo hilo na kwamba, wao wapo tayari kwa ajili hiyo.

 

“Nani asiyejua ninavyoumizwa na suala la kupata mtoto? Nasema ni jambo jema sana na Mungu akinijalia muda ukifika nitafanya hivyo,” alisema Wema.

“Mimi lazima nitaenda naamini nitapata mtoto maana kiukweli nimetafuta kwa muda mrefu bila mafanikio,” alisema Wolper.

 

Mara kadhaa Johari amekuwa akiyaambia Magazeti ya Global namna ambavyo anatamani kuwa angalau na mtoto mmoja bila mafanikio hivyo jambo hilo litakuwa ni faraja kwake.

 

Mbali na mastaa, lakini pia Watanzania wengi ambao wamekuwa wakilia na kusaka watoto na wengine ndoa zao kuingia shubiri kutokana na tatizo la kukosa mtoto watakuwa wamepata faraja.

Tatizo hilo la kukosa mtoto limechangia kuongezeka kwa talaka ambapo kwa mujibu wa utafiti wa kufuatilia kaya Tanzania, wa mwaka 2014/15 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ulionesha kuwa kiwango cha talaka kimeongezeka kwa asilimia 1.1

 

Hii ina maana kuwa kwa sasa kuna wanandoa takriban wanne kwa kila 100 ambao wametengana kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo tatizo la kukosa mtoto.

Vivyo hivyo kwa upande wa baadhi ya mastaa ambao wamewahi kuieleza jamii wazi kuwa wanatamani kupata watoto ingawa bado hawajabarikiwa.

wolper

MUHIMBILI MKOMBOZI

Novemba 19, mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Muhimbili, Profesa Lawrence Museru alisema tayari wamepeleka wataalam nchini India kuangalia namna ambavyo huduma ya upandikizaji mimba (IVF) inavyotolewa katika hospitali za umma, miundombinu na vifaa vinavyohitajika.

 

Profesa Museru ambaye alikuwa akitoa taarifa ya mafanikio ya miaka minne ya Muhimbili (MNH) tangu Rais Dk John Magufuli alipoapishwa kuwa kiongozi mkuu wa nchi, alisema kwa sasa wahandisi wameanza kukarabati jengo katika hospitali hiyo litakaloanza kutumika kwa ajili ya kutoa huduma hiyo kabla ya jipya litakalojengwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila.

 

“Ununuzi wa vifaa unafanyika na mipango imeanza, tayari wataalam wameshatayarishwa, tunatarajia katika miezi miwili ijayo tutaanza rasmi kufanya upandikizaji,” alisema Profesa Museru.

Alisema huduma hiyo itakuwa ya kulipia; “Tutataka watu wailipie hatujajua itagharimu kiasi gani, hiyo ni mpaka wataalam watakapofanya uamuzi, lakini asiyeweza kulipia pia tutaingia kwenye mfumo wa huduma za namna hiyo.”

 

GHARAMA ZA KUSAKA WATOTO KUSHUKA?

Ingawa MNH haijaweka wazi viwango vya gharama za utoaji wa huduma hiyo nchini, takwimu mbalimbali zinaonesha kuwa nchini Kenya wanapandikiza kwa shilingi milioni 5.4, Uganda inagharimu shilingi milioni 9 wakati Uingereza inagharimu zaidi ya shilingi milioni 10.8 na kwa wenza zinafikia shilingi milioni 21.6 kwa kila mzunguko huku Marekani ikigharimu shilingi milioni 10.62 na shilingi milioni 19.8 kwa mzunguko.

 

Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya cha TMH, Dk Isack Maro anasema licha ya kwamba hapa nchini huduma hiyo hutolewa na hospitali binafsi kwa muda mrefu, tatizo kubwa linalokwamisha Watanzania wengi ni gharama.

“Kwa sababu gharama kubwa zinatokana na chemicals, pamoja na vifaa vinavyotumika, kwa hiyo kwa kuwa hiyo itakuwa hospitali ya Serikali labda zitashuka,” alisema.

 

IDADI YA WAOSAKA WATOTO ILIVYOPAA

Kutokana na tatizo hilo la kutopata watoto kuendelea kushamiri nchini, ilielezwa kuwa idadi kubwa ya wanandoa hukimbilia Kenya kupata huduma ya upandikizaji wa watoto kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 5 za Kitanzania ambayo ndiyo ya bei nafuu zaidi ikilinganishwa na nchi nyingine.

 

Mwaka 2012 ilibainika kuwa kati ya wageni 10 wanaokwenda katika vituo vya upandikizaji vya Aga Khan na Nairobi IVF Centre nchini humo, wanne wanatoka Tanzania, hii inadhihirisha kuwa hali sasa inaweza kuongezeka maradufu hivyo ujio wa IVF Muhimbili inaweza kuwa suluhisho la wanandoa wengi.

 

UPANDIKIZAJI UNAVYOKUWA

Akifafanua namna upandikizaji huo unavyofanyika, Dk Maro alisema hufanyika kwa kuchukua mbegu za mwanamume na kuzikuza kwenye maabara maalum na baada ya muda ndipo huzipandikiza katika mirija ya uzazi ya mwanamke.

 

Alisema mwanamke mwenye matatizo huweza kwenda peke yake kupandikizwa kwa kununua mbegu zilizohifadhiwa katika kliniki au wanandoa kwenda pamoja na mwanamume kutoa mbegu ambazo zitapandikizwa kwa mwanamke.

“Tiba huchukua mwezi mmoja, huanzia siku ya pili baada ya mwanamke kumaliza hedhi na siku ya yai kurutubishwa, lakini mwanaume hutumia siku moja tu pale mbegu zake zinapohitajika.”

 

Dk Maro alisema sababu ya kuanza tiba siku ya pili baada ya mwanamke kumaliza mzunguko wake wa mwezi ni kulenga tarehe za uchavushaji, kwani kipindi hicho mbegu za mwanaume hupandikizwa na kusababisha mimba kutungwa.

“Mbegu zilizorutubishwa huachwa kwa siku mbili hadi tano ndani ya chombo maalum ili kukuza kiinitete (embryo) kabla ya kuhamishwa katika nyumba ya uzazi ya mwanamke kwa ajili ya kutungisha mimba ya kawaida.”

 

Aidha, aliongeza kuwa tatizo la ugumba linaongezeka duniani na njia hiyo inatumika kuwasaidia wanawake wasiokuwa na mayai ambao mirija yao ya kuyasafirishia imeziba na wanaume ambao manii yao ni dhaifu na hushindwa kuogelea hadi kufikia yai la mwanamke.

STORI: GABRIEL MUSHI NA IMELDA MTEMA, DAR

Comments are closed.