The House of Favourite Newspapers

RC amtumbua mwalimu tuhuma za kudhalilisha wanafunzi

0

Stephano Mango,   SONGEA
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu amemvua madaraka na kumhamisha Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Namabengo wilayani Namtumbo, Shaibu Champunga aliyekuwa akituhumiwa na wanafunzi wa shule hiyo kuwa na lugha chafu na amekuwa akiwadhalilisha kwa kuwashika matiti na makalio pamoja na kuwachapa viboko visivyokuwa na idadi kinyume na sheria za shule.

Akizungumza na gazeti hili juzi kwa njia ya simu, Mwambungu alisema kuwa amechukua uamuzi huo wa kumvua madaraka na kumhamisha makamu huyo juzi alipokwenda kusikiliza kero za wanafunzi ambao hivi karibuni walikuwa wameandamana kwa kutembea kwa miguu kutoka Namabengo wilayani Namtumbo kwenda Songea kwa lengo la kutaka kuonana naye na maandamano hayo kuzuiwa na polisi wa Namtumbo.

Mwambungu alieleza kuwa aliamua kwenda kwenye shule hiyo kwa lengo la kusikia kilio chao wanafunzi ambao walikuwa wanataka kuonana naye na badala yake malalamiko hayo waliyatoa kwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Namtumbo, Alkwini Ndimbo ambaye baadaye aliwasiliana na uongozi wa shule hiyo kisha wanafunzi waliofanya maandamano walihojiwa na walikiri kufanya maandamano bila kibali jambo lililosababisha kupewa adhabu kwa kuchapwa viboko vitatu kila mwanafunzi na wanafunzi ambao wanadaiwa kuwa ni viongozi walisimamishwa masomo kwa muda wa wiki tatu na watakaporudi shuleni wanatakiwa waende na wazazi wao kwa hatua nyingine ya kinidhamu.

Mwambungu alisema kuwa alipofika kwenye shule hiyo hatua ya kwanza aliichukua kwa kuongea na wanafunzi wote ambao walieleza kero nyingi dhidi ya Champunga, baadaye alikutana na walimu pamoja na uongozi wa shule lakini ilibainika kuwa Champunga alikuwa na mapungufu mengi ambayo yalimfanya alazimike kumvua madaraka na kumhamisha shule na amewataka walimu pamoja na uongozi wa shule hiyo kuona umuhimu wa kuzingatia kanuni na sheria pale wanapochukua hatua ya kutoa adhabu kwa wanafunzi.

Leave A Reply