The House of Favourite Newspapers

RC Makalla Apokea Mwenge Wa Uhuru, Miradi ya Bilioni 21 Kukaguliwa

0

Leo Julai 13, 2023 Mkoa wa Mwanza umepokea Mwenge wa Uhuru kwenye Kijiji cha Muluseni wilayani Ukerewe ukitokea Mkoani Mara ambapo unatarajiwa kukimbizwa kwa takribani Siku 8 kwa umbali wa Kilomita 813.4 nchi kavu na majini.

Akipokea Mwenge huo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amesema ukiwa Mkoani humo unatarajiwa   unatarajiwa kukimbizwa kwenye miradi 51 yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 21.

Mhe. Makalla amesema Mwenge wa Uhuru Mkoani humo unatarajiwa kuweka Mawe ya Msingi kwenye miradi 17 yenye zaidi ya Bilioni 13.7, kufungua miradi 9 yenye thamani  ya Bilioni 3.5, kuzindua mradi 15 yenye thamani ya Bilioni 3.1 huku ukitarajiwa kutembelea miradi 10 iliyogharimu Milioni 609.2.

CPA. Makalla ameongeza kuwa, kwa mwaka 2022 Mwenge wa Uhuru Mkoani Mwanza ulitembelea jumla ya Miradi 52 yenye thamani ya Bilioni 18.7 na kwamba kwa mwaka 2023 Mwenge huo utatembelea Miradi 05 iliyowekewa mawe ya Msingi mwaka jana kwa ajili ya kuifungua.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 Abdalla Shaib Kaim ameomba ushirikiano kwa Mkoa wa Mwanza hususani usahihi wa taarifa za miradi na nyaraka ili kufanikisha mbio za Mwenge huo kwa mwaka 2023.

Wakati huohuo, Mhe. Mkuu wa Mkoa amemkabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Hassan Bomboko kwa ajili ya kuukimbiza kwenye miradi 6 ya wilaya hiyo kwa siku ya kwanza ya tarehe 13, Julai, 2023.

Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2033 inasema “Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa viumbe hai kwa Uchumi wa Taifa.

Leave A Reply