Rekodi ya Simba Yaivuruga Al Ahly

REKODI ya Simba katika michuano ya kimataifa inapocheza katika uwanja wa nyumbani wa Benjamin Mkapa imeonekana kuibeba zaidi timu hiyo kuelekea mchezo wake dhidi ya Al Ahly kiasi cha kuwavuruga kichwa na kuwatishia amani Waarabu hao.

 

 

Simba inatarajiwa kucheza dhidi ya Al Ahly katika mchezo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika wa Kundi A kesho Februari 23 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar.

 

 

Kuelekea mchezo huo, Al Ahly wataingia wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa mwisho kucheza katika uwanja huo ambapo timu hiyo ilifungwa kwa bao 1-0 lililofungwa na Meddie Kagere akipokea pasi ya kifua kutoka kwa John Bocco katika msimu wa mwaka 2018/19 wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

 

Simba katika michezo tisa iliyopita ya Ligi ya Mabingwa Afrika uwanjani hapo, haijapoteza mchezo hata mmoja ambapo kwenye michezo hiyo tisa, imefanikiwa kuibuka na ushindi katika michezo sita huku ikitoka sare michezo mitatu.

 

 

Hata hivyo, timu hiyo imeonekana kuwa na uwiano mzuri wa kufunga mabao ikiwa na wastani wa kufunga mabao mawili katika kila mchezo kutokana na Simba kufunga jumla ya mabao 18 katika michezo hiyo tisa, huku ikiwa imefungwa mabao matatu tu.

 

 

Matokeo ya Simba katika michezo tisa ya mwisho kwa Mkapa yalikuwa hivi, Simba 4-0 Mbambane Swallows, Simba 3-1 Nkana, Simba 3-0 JS Saoura, Simba 1-0 Al Ahly, Simba 2-1 AS Vita, Simba 0-0 TP Mazembe, Simba 1-1 UD Songo, Simba 0-0 Plateau na Simba 4-0 Platinum.

 

Marco Mzumbe,

Dar es Salaam

Toa comment