The House of Favourite Newspapers

Ringo: Sikuanguka Kwenye Ubunge, Mama Alinikataza!

0

KAMA ilivyo kwa wachekeshaji wakubwa duniani, Rowan Atkinson ‘Mr Bean’ na Charles Spencer Chaplin ‘Charlie Chaplin’ , vijana wengi Bongo wamekuwa wakifanya komedi ya visa vifupivifupi vya kumfanya mtu abaki midomo wazi.

 

Tumeona wengi wakitengeneza filamu na wengine vipande vifupi na kuvitupia kwenye mitandao ya kijamii.

Jacob William Mkweche almaarufu Ringo ni mchekeshaji mkali Bongo ambaye anapeperusha vizuri bendera kwa kukubalika kutokana na kazi zake.

Ringo amefanya poa na filamu kama Chifu, Bifu, Utani, Shumileta, Kokoro, Mburura, Bad Kid, Komando Kipensi, Zungusha na nyingine kibao.

 

IJUMAA WIKIENDA limefanya mahojiano maalum (exclusive interview) na Ringo ambapo amefunguka usiyoyajua juu yake, lakini kubwa zaidi ni kuanguka kwenye ubunge kupitia kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM);

IJUMAA WIKIENDA: Nani aligundua kipaji chako?

 

RINGO: Nilianza tangu nikiwa shule ya msingi, nilikuwa ninaiga sauti nikiwaangalia akina Mzee Majuto, Jongo na wengine. Basi watu wakawa wananiambia ninaweza ndipo nikaingia kwenye makundi ya kuigiza.

IJUMAA WIKIENDA: Ulikaa kimya kwenye gemu. Je, unakuja na kitu gani?

 

RINGO: Nakuja na filamu yangu inayokwenda kwa jina la Ringo is Back.

IJUMAA WIKIENDA: Je, umeshirikisha wasanii gani kwenye filamu hiyo?

RINGO: Katika filamu hiyo, kutakuwemo na wasanii kama Kingwendu, Masantula, mimi mwenyewe na wasanii chipukizi ambao tunawanyanyua.

 

IJUMAA WIKIENDA: Wewe ni mchekeshaji mzuri. Je, kwa upande wa filamu za siriazi, mikakati yako ikoje?

RINGO: Ikitokea fursa hiyo, ninaweza kufanya na niliwahi kuigiza kwenye Shumileta.

IJUMAA WIKIENDA: Kwa kuhesabu una filamu ngapi sokoni ambazo umewahi kuzicheza?

RINGO: Naweza nikahesabu za kwangu ni kama hamsini na zaidi, unajua zamani filamu za kushirikishwa tulikuwa tunaangalia maslahi.

 

IJUMAA WIKIENDA: Katika sanaa ya uchekeshaji, unaonaje upepo unavyokwenda ukilinganisha na zamani?

RINGO: Tulivyoanza kuna uzuri wake kwa sababu wasanii tulikuwa tunapendana, kushirikiana na kupeana mawazo. Tangu sanaa imeanza kulipa, tumekuwa na chuki na kutokushirikiana.

IJUMAA WIKIENDA: Umeonekana kucheza filamu nyingi na Martin (Tin White). Je, ukaribu wenu ukoje?

 

RINGO: Tin White ni rafiki yangu wa muda mrefu, japokuwa alihojiwa kama mimi ni ndugu yangu, akajibu mimi si ndugu yake, ila kwa upande wangu tuko pamoja kwa miaka kumi.

IJUMAA WIKIENDA: Mna ugomvi mpaka aseme hivyo?

 

RINGO: Tin ni ndugu yangu kabisa na ninampenda, hajawahi kunikosea na wala hatuna ugomvi, labda kusema hivyo alikosea tu.

IJUMAA WIKIENDA: Teknolojia inakuza vipi sanaa ya uchekeshaji?

RINGO: Niseme ni nzuri, maana imeongeza ajira kwa vijana, mashabiki zangu wategemee kuniona kwenye uchekeshaji wa mitandaoni.

 

IJUMAA WIKIENDA: Kufanya kazi kimataifa imekaaje kwa upande wako?

RINGO: Watu walimkosoa marehemu Steven Kanumba (Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema) alikuwa sawa, maana alikuza sanaa yetu nje ya nchi. Tutaanza kupenya taratibu na kufika huko hasa Afrika Mashariki.

IJUMAA WIKIENDA: Wasanii wengi wameonekana kuingia kwenye tamthiliya. Je, kwa upande wako, hujapata dili?

RINGO: Kikubwa niseme tu ni sawa, maana soko la filamu limeshuka, ndiyo sababu Rais wetu (John Pombe Magufuli) amesema akipita atatusaidia, maana wizi ulikua mwingi hapo kati kati.

IJUMAA WIKIENDA: Katika uigizaji, unamtazama sana nani (role model)?

RINGO: Nampenda Madebe Lidai, maana anafanya vitu vyenye uhalisia wa maisha yetu.

IJUMAA WIKIENDA: Ulionekana kuingia kwenye muziki. Je, nini kilikuvutia?

 

RINGO: Mimi ninapenda muziki, ila tatizo ni mdundo (beat) huwa unanichanganya, maana ninaimba kwa mdomo, halafu ninaisikia kwenye masikio.

Muziki wangu ninaufanya kwa utofauti, maana ninaitumia sanaa yangu ya maigizo. Namshukuru sana Prodyuza Man Water, ni mtu mzuri sana, ndiye anayenisaidia.

 

IJUMAA WIKIENDA: Unaitumiaje sanaa ya uchekeshaji kwenye maisha binafsi?

RINGO: Kipindi cha nyuma tulikuwa tunakaa kwenye filamu na kutokuangalia mambo mengine, ndiyo maana nikasema mashabiki wategemee makubwa.

IJUMAA WIKIENDA: Nini kilikushawishi hadi ukaamua kutangaza nia ya kugombea Ubunge wa Jimbo la Liuli, Songea?

 

RINGO: Mimi siyo mwanasiasa, ila nilikuwa niko Mwanza, kuna rafiki zangu wanatokea Songea, wakaniomba nigombee. Nilikuwa naogopa, ila nikaona ngoma inakwenda na watu wakanihamasisha, ndipo nikamshirikisha mama.

IJUMAA WIKIENDA: Mama alitoa neno gani baada ya wewe kutangaza nia?

RINGO: Mama alinikataza, akaniambia nisichukue fomu, nijifunze kwanza.

IJUMAA WIKIENDA: Ringo ni mtu wa aina gani nje ya sanaa?

 

RINGO: Nje ya kazi mimi ni mtu mwenye aibu sana, napenda watu, nina huruma; Mungu akinijaalia nikawa tajiri, nitasaidia watu wasiojiweza.

IJUMAA WIKIENDA: Sanaa imekunufaisha vipi?

RINGO: Imenikutanisha na watu tofauti, ninajikimu maisha yangu yanakwenda, nina kiwanja Chalinze, pia ninajenga Vikindu.

MAKALA: HAPPYNESS MASUNGA NA KHADIJA BAKARI, BONGO

Leave A Reply