The House of Favourite Newspapers

Roma Fundi wa Kukinukisha Bongo

0

ROMA Zimbabwe ndilo jina analotumia kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii. Kama kawaida yake rapa huyu bora Bongo ambaye kwa sasa maskani yake ni Marekani, amezua mjadala baada ya kusambaa vipande vya video fupi vinavyomuonesha akizungumza juu ya masuala yanayohusiana na sekta ya muziki Bongo na namna inavyolinganishwa na wanamuziki wa Nigeria.

 

Roma anafunguka kwa uchungu na hisia kali mno. Siku za karibuni wasanii wa Bongo Fleva; yaani Harmonize na Diamond Platnumz wamekuwa wakifanya shoo nje ya nchi hasa Marekani,

 

Hata hivyo, kumekuwa na maneno mengi mitandaoni kuwa wanashindwa kujaza baadhi ya shoo hizo na wanapokelewa vibaya tofauti na ilivyo kwa shoo za Wanigeria.

Wakati Roma akionekana kuitetea tasnia ya muziki na wasanii wa Bongo, lakini ni dhahiri kuwa anachokiongea ni cha kujenga na chenye maslahi mapana kwa tasnia mbalimbali Bongo.

 

Hakuna jambo alilolizungumza linalobomoa bali amezungumza kwa kuziba ufa unaojitokeza na uliojitokeza kwa wadau wa tasnia ya muziki na tasnia zingine juu ya kasumba ya kutotaka kuthamini mchango wa wasanii waliotoboa nje ya mipaka na badala yake kuwafananisha kwa kebehi na wasanii wa Nigeria kwa namna wanavyojaza kumbi za muziki na idadi kubwa wanaoitwa kupafomu majuu.

 

Ukweli mchungu, lakini lazima tuuzungumze; Wenzetu Wanigeria wametuzidi kwenye upande wa burudani, lakini haimaanishi wasanii wa Bongo hawawezi kufikia nafasi hiyo ya juu. Utakumbuka Diamond Platnumz kutoka Bongo amewahi kuzivunja rekodi kubwa zilizowahi kuwekwa na wasanii wa Kinigeria kama Davido kupitia wimbo wake wa Waah. Bado haitoshi kuamini Bongo tuna nafasi ya kufika walipofika Wanigeria?

Sasa twende pamoja tukichambue kile alichokizungumza Roma;

 

AFYA

Roma ambaye kwa muda mwingi sasa yupo nje ya nchi amedhihirisha ukweli kwamba siyo tu katika tasnia ya muziki, bali pia kwenye sekta ya afya kuna Wanigeria wengi kuliko Wabongo.

 

Sekta hii muhimu na yenye pesa ndefu majuu ni ngumu kumpata Mtanzania na hata ukimpata, basi ni wachache mno. Hivyo wakati tunawasema wasanii wa Bongo juu ya namna wasivyojaza katika shoo za mbele, basi tuwaseme. Pia watumishi wa afya Bongo kwa nini hawavuki mipaka kwenda kufanya kazi mtoni?

 

Tunahitaji kuwaona akina Dk Mwaka wengi wakitokea Bongo na kwenda kufanya kazi nje ya nchi katika mataifa makubwa kama Marekani na Uingereza. Hivyo hakuna budi kukaza buti na siyo kuona Wasanii tu ndiyo wanastahili kuvuka mipaka.

 

MICHEZO

Nani asiyejua Wanigeria wanafanya vizuri mno kwenye michezo nje ya nchi. Hii ilitokana na waasisi walioanza kupasua anga mapema na kukiwasha katika soka la kulipwa nje ya nchi na leo hii kuna Wanigeria wengi wanaokinukisha katika ligi kubwa za kandanda majuu. Kwa Tanzania wapo ila siyo wengi kama wenzetu Wanigeria, nikisema tutaje wanamichezo wanaocheza ligi kubwa Ulaya tutawatafuta kwa tochi zaidi ya Mbwana Samatta.

 

Haimaanishi wanasoka wa Kitanzania hawana uwezo wa kucheza soka majuu, hapana. Hapa ni kuwapa nafasi na muda zaidi maana muda unaongea. Hivyo kwa mwanamichezo kumsema vibaya msanii wa muziki Bongo eti haliwakilishi Taifa vyema ni busara pia akajiangali katika sekta yake ya michezo na kuona yeye analiwakilisha vyema taifa wapi.

 

HABARI

Nani asiyependa kuwaona akina Salim Kikeke wengi wakikiwasha kwenye vyombo vikubwa vya habari Ulaya na Uarabuni na duniani kote? Hakuna.

 

Wakati kukiwa na Wabongo wachache katika vyombo vya habari majuu, lakini kuna nyomi ya Wanigeria wanakiwasha tu. Huku Mwanahabari Bongo anakaa kumsikitikia msanii eti kwa nini havuki mipaka kwenda majuu wakati na yeye pia anastahili kuvuka mipaka hiyohiyo na kwenda kushika kipaza Ulaya na nchi zingine kubwa.

 

Kuna kila sababu wanahabari kuona umuhimu wa kukaza buti ili wapate nafasi katika vyombo vikubwa vya habari duniani.

 

SHERIA

Upande wa sheria mambo yanaonekana kuwa magumu zaidi. Roma anasema ni ngumu mno kumpata mwanasheria mwenye asili ya Kibongo akifanya poa huko Ulaya na nchi nyingine kubwa kama China au India.

 

Wakati wanasheria wa Kibongo wakiwa ni wa kuwatafuta kwa tochi nchini Marekani, lakini wanasheria wenye asili ya Nigeria wamejazana tu. Na wanafahamika mno kwa kazi zao nzuri za kisheria wanazozifanya majuu.

Unaweza kuona ni kwa namna gani Wanigeria wametupiga bao la mkono katika nafasi nyingi tu na siyo kwenye muziki pekee.

 

Tunahitaji wanasheria wakajazane huko mambele hasa Marekani ili na sisi tujivunie Ubongo wetu kuwa tuna wanasheria wanaosaidia watu wa nje hivyo na sisi tuna uwezo wa kufika huko na siyo tu kuwanyooshea vidole wasanii wa wa Bongo Fleva.

 

MA-DJS NA PROMOTA WA MUZIKI

Wakati tukishindanisha MADJS kibao waliojazana Bongo, lakini tunasahau kuwashindanisha na MADJS wengine waliopo majuu kama Marekani ambao asili yao ni Nigeria.

 

Kuna MADJS kibao wa Nigeria wanaokinukisha kwenye shoo kubwa za wasanii wakubwa, lakini kumpata DJ Mtanzania anayekiwasha huko majuu ni ngumu mno.

 

Vivyo hivyo, upande wa mapromota, Wabongo ni wachache lazima ukweli tuambiane. Lakini hatuwasemi wala kuwaongelea na kuwalinganisha na wenzao Wanigeria waliotusua anga badala yake tunakesha kuwanyooshea vidole wasanii wawili tu; Diamond na Harmonize kushindwa kujaza ukumbi. Hii siyo sawa.

 

BONGO FLEVA

Hapa lazima tuwaheshimu wasanii wanaojaribu kwa kila namna kuvuka mipaka na kutengeneza njia kwa vizazi vijavyo vya muziki wa Bongo.

 

Mtu kama Diamond amekuwa chachu kwa wasanii kibao Bongo kufanya video na kolabo na wasanii wa majuu. Harmonize naye kijana mdogo anakiwasha majuu na anawakalisha wasanii wakubwa huko. Kwa nini tusiwape heshima yao kwanza kabla bado hatujawalinganisha kwa kebehi na hao Wanigeria?

 

Alichokifanya Roma kuonesha ufundi wake wa kukinukisha Bongo ili kila mmoja ajitathmini, aone kama hapo alipo ndipo anapostahili kuwepo au naye anastahili kutoboa kimataifa? Vijana wanapambana na tunaona. Kazi iendelee.

MAKALA; BAKARI MAHUNDU, DAR

Leave A Reply