The House of Favourite Newspapers

Roma kwa hili utalosti, jiangalie upya dogo!

0

ROMAMKATOLIKI1

UGUMU wa maisha Bongo umewafanya watu wengine kujitoa ufahamu. Asubuhi na mapema, unamkuta kijana wa Kitanzania amekamata kinywaji chake aina ya kiroba anakunywa, anataka ashinde akiwa hana akili sawasawa, maana hajui jinsi siku yake itakavyoisha.

Anapowaona viongozi wakikatisha ndani ya magari ya thamani kubwa, anasema ‘wenye nchi hao bwana, ndiyo wanakula maisha’. Akilini mwake anaamini kabisa kuwa kuna kundi f’lani dogo la wateule, ndilo la wenye nchi, wao na familia zao.

Ndiyo maana siyo jambo la ajabu kuona kijana akitukana matusi makubwa ya nguoni mbele za watu, haoni tabu, kwani maisha yake yamegubikwa na tabu.

Hata ukija kwa wanaharakati, nao wana hasira. Wamekua wote mtaani na watoto wa vigogo, wakawaona wenzao wakipelekwa shule za bei mbaya na baadaye wakasoma ng’ambo.

Leo ndiyo maofisa Benki Kuu, TRA, Bandari na mashirika yote makubwa ya serikali na binafsi. Ndiyo maana wanapiga kelele, ufisadi! Ufisadi!

Ni kweli, nchi haiendi sawa. Kila mwenye nafasi ya kukemea anachoona hakiendi sawa, anaruhusiwa kupaza sauti pasipo kuvunja sheria.

Ibrahim Mussa maarufu kama Roma, ni mmoja kati ya wasanii wanaharakati, wenye uthubutu wa kutoa maoni yao kupitia muziki. Niseme ukweli, ninamkubali sana huyu dogo, maana anajua kuwakilisha kama ambavyo Hip Hop inataka.

Hip Hop ina misingi ya ukweli na inasimamia hapo. Inasema rangi inayoonekana, kama ni nyeupe, nyeusi, njano na yoyote iliyo mbele yake. Ni kwa misingi hiyo, ndiyo maana kibao chake kile cha 2030, kilikamata sana. Ni kwa sababu alizungumza kile ambacho kipo. Mimi ni shabiki sana wa ile ngoma!

Lakini kwa namna ya kusikitisha sana, Roma ametoa kazi nyingine mpya inayokwenda kwa jina la Viva Roma Viva. Ni kazi nzuri pia, inayotambaa katika misingi ileile ya ukweli. Inaakisi mambo yanayoendelea ndani ya jamii yetu.

Lakini lipo tatizo la kimsingi kabisa ambalo Roma kama msanii ambaye tunaambiwa kuwa ni kioo cha jamii, alipaswa kuliepuka mapema. Lugha aliyotumia, ingawa ni kisanii kama inavyojulikana, lakini imekaa ndivyo sivyo.

Ametumia maneno makali mno kuwasilisha hisia zake, kiasi kwamba vituo vingi vya redio vinasita kuupiga. Mwenyewe anaamini watu wa redio wanaubania tu wimbo wake, kwamba ni mzuri na wenye ujumbe murua.

Busara inayotumiwa na watu wa redio kutopiga wimbo huo, ndiyo ileile ambayo Roma alipaswa kuitumia mapema wakati akiutunga na hata kurekodi. Maneno makali na yaliyokosa staha hayawezi kuupaisha wimbo, bali yatauzuia kufika kwa walengwa.

Dogo angeweza kuiboresha lugha yake, lakini ikabeba ujumbe uleule aliokusudia na ungewafikia wengi, wakiwemo wahusika na bila shaka wangejifunza. Alichofanya, ni sawa na wale waigizaji wetu mbumbumbu ambao huvaa nusu utupu wakiamini filamu zao zitafunika wakati wanajidhalilisha.

Matokeo yake ni kuwa wanaosikiliza wimbo huo, siyo watu wa hali ya chini ambao aliwatetea, bali wale wenye uwezo wa kumiliki simu zenye internet au kompyuta ambao ni wachache. Lakini angeenda vizuri, wimbo huo ungekuwa kivutio redioni kiasi kwamba hata ndugu zangu kule Mkumbi wangeusikia na kuuelewa!

Roma bado ni msanii mchanga na aina ya muziki alioamua kuufanya ni mgumu. Unahitaji weledi wa hali ya juu na kubadilika kila wakati ili kufikia kileleni. Kama anaufanya muziki kama hobi ni sawa, lakini kama analenga naye kujikwamua kimaisha, bado ni mapema kutumia lugha kali anayojaribu kuifanya.

Kwa jinsi ya kichwa chake kilivyo, ni bora atumie zaidi nahau, methali na misemo ya mitaani ili kuwasilisha hisia zake, kwani tayari watu wanaelekea kumwelewa!

Leave A Reply