Chuzi Ndo Hilo, Hakuna Kuonja!-15

ILIPOISHIA IJUMAA WIKIENDA:

Bajaj iligeuzwa kwa kasi kutokana na hali ya uso wa baba Shua, dereva akajua anawahi sehemu kwa dharura.

“Nipeleke kule, kanyaga mafuta kama unafukuza mwizi.”

***

Mama Shua alizama ndani ya gari la Musa…

“Ondoa gari, maana kama sijamuelewa mume wangu, anaweza akafuatilia,” alisema mama Shua.

ENDELEA MWENYEWE SASA…

Ile anafunga mlango tu, Bajaj aliyopanda mume wake ikatokea kwa mbali kidogo.

Baba Shua alitumbua macho mbele akiamini kama mke wake atakuwa anaondoka na daladala lazima angemwona anakaribia kituoni na kama hayupo, ina maana atakuwa ndani ya gari analoliona mbele yake ambalo ni la Musa ambapo yeye baba Shua halijui.

“Unaweza kuendesha kwa kasi hadi kulifikia lile gari?” baba Shua alimuuliza dereva ambaye badala ya kujibu aliongeza mafuta kwa kasi.

Lakini wakati analikaribia, gari hilo likawa limeshaingia barabara kuu. Kwa mbali, ndani aliona watu wawili akiwemo dereva lakini hakuweza kupata mtazamo kamili kama ni wanaume, wanawake au mwanaume na mwanamke kwa vile vioo vya gari vilikuwa ‘tinted’…

“Unajua kuna Bajaj inatufuata kwa kasi sana,” Musa alimwambia mama Shua. Ilibidi mwanamke huyo ageuke kuiangalia lakini akaiona kwa gizagiza sana. Kwa hiyo hakujua ndani ya gari lile mlikuwa na nani na ni nani!

Baba Shua alimwambia suka waishie pale lakini akaisoma namba na kuandika kwenye simu yake kisha akarudi nyumbani akiwa amefura sana. Aliamini moyoni kwamba, mkewe alipanda lile gari…

“Yaani mama Shua sasa amefika pabaya, anafuatwa na magari hadi nyumbani! Hii kwa kweli siwezi kuivumilia hata kidogo,” alisema moyoni huku akituma meseji kwenda kwa mkewe…

“Kwa hiyo sasa umefikia hatua ya kufuatwa na gari hadi nyumbani ili likupeleke kazini. Tutawezana kweli?”

Mama Shua aliposoma meseji hiyo alishtuka sana…

“Mh! Au alikuwa kwenye ile Bajaj nini?”

Alitaka kumfowadia meseji Musa lakini akahisi atakuwa anamtisha kijana wa watu, akaacha…

“Gari gani mume wangu?”

Wakaanza kujibizana sasa…

“Gari gani? Kwani we umepelekwa kazini na gari gani?”

“Nilipanda basi baba Shua.”

“Usinidanganye mimi wewe. Umepanda gari lenye namba za usajili T 349 CAT, unabisha?”

Mama Shua hakuzijua namba za gari lile, lakini akajitutumua na kujibu kwa ufupi…

“Ina maana uliniona nikiingia kwenye gari au?”

“Ndiyo,” baba Shua alifanya kusudi kujibu hivyo ili aone, mkewe atajibu nini.

Mama Shua alihema kwa kasi, akajua kweli alionekana na mumewe, ilibidi asiijibu meseji hiyo.

Baba Shua alipoona nusu saa inapita bila majibu, alituma meseji nyingine…

“Mimi umenichosha na vitabia vyako vya siku hizi, kwa nini usije kuchukua vitu uondoke hapa nyumbani? Maana najua unataka uhuru hapa kwangu umebanwa!”

Ilikuwa meseji nzito sana kwa mama Shua. Alianza kuingiwa na wasiwasi. Aliamini hali ndani ya ndoa yake si nzuri, akaanza kuona hatari ya siku za mbele.

Hakuwahi kufikiria hata siku moja kwamba, mumewe angeweza kumtamkia maneno mazito kama hayo, lakini siku hiyo alitamka bila kutumia lugha ya mafumbo. Hata meseji hiyo hakuijibu.

***

Saa saba juu ya alama, Musa alimpigia simu mama Shua…

“Haloo,” alipokea mama Shua bila maneno ya kuchombezea kama ‘haloo baby’, ‘niambie darling’ na mengineyo…

“Vipi sweet, mbona umepokea simu kama hunifahamu vile?”

“Ah! Siko sawasawa bwana…”

“Kuna nini?”

Mama Shua alijua akisema amwambie yaliyojiri, hata yeye Musa angeshtuka na kuogopa sana, akamdanganya…

“Mwili wangu kama unaumauma kwa mbali halafu moyo kama hauna furaha vile.”

“He! Kuna nini tena? Uko wapi kwani?”

“Nipo job. Wewe..?”

“Mimi nipo hapa hotelini napata mchemsho wa samaki. Kama vipi njoo unywe.”

“Ah! Yaani hata kutoka hapa pia sijisikii kabisa.”

“Basi twende chumbani baby, nikakupetipeti, nikakufinyefinye wee mpaka useme basi. Halafu mambo yetu yawe kama ya siku ile, unasemaje?” alisema Musa na kumfanya mwanamke huyo kusisimka, akajikuta akichangamka mwili…

“Jamani baby, usinifanye nicheke darling…lo! Maneno yako matamu kama asali…”

“Hata mimi mwenyewe nipo kama asali kama ulivyo wewe,” alisema Musa, mama Shua sasa akawa si yule aliyepokea simu, akaachia kicheko cha haja…

“Wapi sasa?”

“Si nimekwambia napata mchemsho…”

“Ina maana huko kunifinyafinya utanifinyia hapohapo hotelini?”

“Aah! Si kule bhana…”

“Saa ngapi?”

“Wewe tu, hata ukisema leo mimi niko tayari.”

“Kweli?”

“Kweli kabisa. Mimi nitaondoka kazini maana leo sina kazi nyingi sana,” alisema Musa na kumfanya mama Shua kuliangalia begi lake lilipo.

Alichofanya, alimtumia meseji mumewe…

“Naumwa, nakwenda hospitali.”

Mumewe hakuijibu meseji hiyo zaidi ya kuachia tabasamu la mshangao huku moyoni akisema…

“Amejua ana msala sasa anatafuta namna ya kuumaliza.”

Mama Shua aliomba ruhusa kazini, akisema anakwenda hospitali hajisikii sawasawa.

Alichukua usafiri huku akimtumia meseji Musa ya kumuuliza kule hotelini aende muda huo au bado!

“We umeshatoka kwani?”

“Niko njiani.”

“Tangulia na mimi natoka hapa nakwenda chukua gari kisha hotelini, hapa nilipo mawazo yangu yote nipo na wewe kitandani.”

Je, nini kitaendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda, siku ya Jumatatu.

Loading...

Toa comment