The House of Favourite Newspapers

Rugemalira, Singasinga Watubu kwa DPP, Huenda Wakaachiwa

WAFANYABIASHARA James Rugemalira na Habinder Sethi ‘Singasinga’ ambao pia ni wamiliki wa kampuni ya kufua Umeme ya IPTL, wamedaiwa kuandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kuomba msamaha na kukiri mashitaka ya uhujumu uchumi yanayowakabili katika Mahakama ya Kisutu.

 

Imedaiwa kuwa, Seth aliandika barua hiyo iliyopitia kwa Mkuu wa Gereza mapema, mwezi huu wa Oktoba baada ya Rais  John Magufuli kumshauri DPP, Biswalo Maganga,  kuona uwezkano wa kuwasamehe washtakiwa wa uhujumu uchumi ambao wako tayari kukiri makosa yao na kurudisha pesa waliozoisababishia serikali hasara.

 

Mapema leo, Oktoba 10, 2019, Wakili Michael Ngaro anayemtetea Rugemalira amedai kuwa mteja wake ameandika barua kwa DPP kuomba kukiri makosa ya uhujumu uchumi yanayomkabili na kwamba mpaka sasa hawajapata majibu.

Kufuatia taarifa hiyo Ngaro ameuomba upande wa mashtaka kufanya mchakato ili wapate majibu ya barua hiyo haraka.

 

Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, amedai kuwa, ni kweli wamepokea barua za washtakiwa wote wawili na kwamba zinafanyiwa kazi na watapatiwa majibu.

 

Kesi hiyo ambayo leo ilikuja kwa ajili ya kutajwa imeahirishwa hadi Oktoba 24, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa tena.

 

Washtakiwa hao kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani hapo Juni 19, 2017, wakikabiliwa na mashitaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha na kuisababisha serikali hasara ya Dola 22,198,544.60 na Tsh 309,461,300,158.27.

Comments are closed.