The House of Favourite Newspapers

Saa ya Milioni 290 ya Mondi Yazua Gumzo

0

AMEVAA milioni 290 mkononi! Siku chache baada ya staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au Mondi kutupia picha na video akiwa amevaa saa ya bei mbaya huku akijisifia, video hiyo imeibua gumzo kutokana na thamani ya saa hiyo ambayo imetajwa kuwa zaidi ya Sh milioni 290, Risasi Mchanganyiko linaripoti.

 

Baada ya Mondi kuwa anaonekana na saa hiyo ndipo watu wakaanza kufukunyua na kugundua kuwa saa hiyo ni aina ya Patek Philipe Rose Gold.

 

Kwa mujibu wa video aliyoposti kwenye Insta Story yake (IS) Instagram, Mondi aliinunua kwa gharama ya shilingi milioni 13 za Kenya (zaidi ya shilingi milioni 290 za Kitanzania).

Kupitia Insta Story, Mondi alieleza kuwa saa hiyo alijinunulia kwa gharama hiyo kama sehemu ya kujipongeza kwa kupata mtoto wa kiume na mwandani wake, Tanasha Donna, yapata mwezi mmoja uliopita.

 

GUMZO LILIVYOIBUKA

Kutokana na aina ya saa hiyo ambayo ilitengenezwa kwa muda wa miaka mitano na Patek Philipe huko Geneva Uswis katika miaka ya 1839, baadhi ya vyombo vya habari nchini Kenya viliibua madai kuwa, rangi ya saa aina ya Patek Philipe Rose Gold ‘orijino’ inatofautiana na hiyo ya Mondi.

 

Hata hivyo, vyombo hivyo vilienda mbali zaidi ya kutumia maoni ya baadhi ya wachangia kwenye mitandao hiyo ya kijamii ili kuonesha utofauti huo.

 

“Ukiitazama vizuri ile ya Mondi ina rangi ya bluu-bahari, tofauti na Patek Philipe Rose Gold orijino ambayo ina rangi ya dhahabu,” alisema mmoja wa wafuasi wa Mondi kwenye picha aliyoposti kwenye ukurasa wake wa Instagram, inayomuonesha akiwa amevaa saa hiyo huku akiwa amechuchumaa mbele ya gari aina ya Rolls-Royce Phantom, lenye rangi nyeusi.

 

Gumzo lingine ni kwenye bei ya saa hiyo ambayo kwa mujibu wa tovuti mbalimbali inaonesha kuwa mbali na bei ya Sh milioni 290, pia zipo saa za Patek Philipe ambazo zinatofautiana aina na bei zake hadi kufikia sh bilioni 25 kwa saa moja.

 

…UBORA WA KIPEKEE

Pamoja na kutazama kwa kina aina ya saa hiyo aliyoinunua Mondi, jina la saa za aina nyingine zilizozalishwa na Patek Philipe pia ipo ambayo imeshika namba saba duniani katika orodha ya saa ghali na zenye ubora. Pia tafiti za masuala ya saa zinasema kuna vitu vitatu muhimu vya kuzingatia kuhusu ubora na gharama za saa hizo.

 

Kwanza saa yenye thamani ya juu sharti iwe na sehemu zilizoundwa na mawe yenye thamani ya juu kama vile almasi, platinum, dhahabu, na mawe kutoka anga ya mbali.

Pili saa hiyo lazima iwe imechukua muda mrefu sana kuitengeneza na iwe na uwezo wa kufanya kazi bila hitilafu ya mara kwa mara.

 

Tatu saa hiyo pia lazima iwe na uwezo wa kipekee wa kutekeleza majukumu yake mbali na kueleza wakati. Hivyo ndivyo vipengele vitatu muhimu ambavyo vinajirudia katika orodha ya saa tano ghali zaidi duniani kulingana na jarida la saa ghali zaidi la Alux.

 

SAA ZA PATEK PHILLIPE

Ni dhahiri kuwa Mondi amenunua saa zilizo katika kundi la saa za bei ghali zaidi duniani kwa sababu mbali na Patek Philipe Rose Gold aliyonunua msanii huyo kwa Sh milioni 290, pia kuna Patek Philipe Ref. 1518 – Wristwatch ambayo inauzwa Sh bilioni 25.2 na imeshika namba saba kwa saa ghali zaidi duniani wakati saa aina ya Patek Philippe – Henry Graves – Pocket inayoshika namba tano inauzwa Sh bilioni 55.1 kwa mujibu wa jarida la Alux lililotolewa mwaka huu.

 

Saa za Patek Philippe hutoa aina mbalimbali za saa ghali duniani kwani saa hizo ziliweka rekodi hiyo kwa kipindi kirefu.

Kwa mfano saa aina ya Patek Philippe – Henry Graves – Pocket Watch ilitengenzwa mwaka wa 1933 mahsusi kwa ajili ya mmiliki wa benki, Henry Graves.

 

Mtengenezaji wake Patek Philippe anasema ilimchukua miaka mitano kuikamilisha saa hiyo ya kipekee.

Aina hiyo ya saa imejijengea sifa ya kuwa saa ya pekee duniani yenye uwezo wa kutekeleza majukumu 24 kwa wakati mmoja.

Saa hiyo iliundwa kutokana na dhahabu yenye ubora wa karati 18. Hadi mwaka wa 2013 hakuna saa yoyote iliyowahi kuishinda saa hiyo kwa ubora.

 

ORODHA YA SAA TANO BORA

Namba tano ni saa ya Patek Philippe – Henry Graves – Pocket Watch ambayo inauzwa dola za Marekani milioni 24, namba nne ni Chopard 201- carat ambayo inauzwa kwa dola milioni 25.

 

Namba tatu ni Breguet grande complication marie- Antoinette inauzwa dola za Marekani milioni 30. Namba mbili ni saa aina ya Graff Diamonds The Fascination inayouzwa kwa dola za Marekani milioni 40 wakati namba moja ni saa aina ya Graff Hallucination ambayo inauzwa dola milioni 55.

 

MONDI AMEPIGWA?

Aidha, gumzo kubwa lililoibuka nchini Kenya nyumbani kwa mzazi mwenzake, Tanasha, zilikuwa ni kumuonesha Mondi kuwa ‘amepigwa’ kwa kununua saa feki.

Haijulikani waliokuwa wakiposti aina hiyo ya saa kwenye mitandao ya kijamii hasa ya Kenya walikuwa wanalenga nini juu ya Mondi.

 

Tangu hapo Mondi hakujitokeza tena kuzungumzia kupigwa au kutopigwa kwa kununua saa hiyo na kuacha mambo yaishe kimyakimya bila ukweli kujulikana.

STORI: MWANDISHI WETU, RISASI

Leave A Reply