Sababu ya wanandoa vijana kuhamia kwa wazee hii hapa

Asalam alaikum /Bwana Yesu asifiwe. Bila shaka mpo sawasawa. Kwa wagonjwa nawaombea kwa Mungu awape uzima tele.

Leo nimeamua kuja na mada hii kwa sababu siku hizi si ajabu kusikia mwanaume f’lani anatoka na mwanamke ambaye si rika lake. Au anatoka na mwanamke wa kuweza kumzaa yeye, kwa maana ya mama. Hii si ajabu kabisa kutokea.

Je, kwa hili mnadhani sababu ni nini? Wanawake wadogowadogo siku hizi hawaolewi. Na hata wakiolewa wanaume wao hawadumu, wanahamia kwa wakubwa. Naweza kusema wasichana wa siku hizi wao wenyewe ndiyo sababu kwani wanashindwa kuwalea waume zao ipasavyo.

Mnajua wanaume hukaa vijiweni na kubadilishana mawazo. Wengi wao husifia jinsi wake zao wanavyowafanyia na wengine husema sababu zilizowafanya kuwa na ‘nyumba ndogo’ watu wazima kuliko wake zao.

Si wanaume tu, hata wanawake wana vijiwe vyao. Wengi kwenye vijiwe hivyo hupendelea kuwasema waume zao walivyo mabahili, hawawanunulii nguo na wengine hutoa hata siri za chumbani kitu ambacho si sawa.

Kwa mwanaume kuongea ni kawaida lakini kwa mwanamke kwanza ni aibu sana kutoa siri za chumbani.

Kama ulivyofundishwa mwanamke huwa hatoi siri huwa anaifungia kabatini na sifa ya mwanamke bora siku zote ni kuwa msiri.

Sasa baada ya kuwapa maneno haya makali ngoja niende kwenye mada iliyonisukuma kukuambia haya.

Mwanaume mmoja alisimulia jinsi alivyo na amani baada ya kumpata mwanamke mtu mzima  wakati akiwa na mkewe ambaye ni mrembo na mwenye kutambua kuwa ana mume.

“Nakumbuka siku niliyomuoa mke wangu alinifanya nijivunie kuoa kwa jinsi alivyonihudumia na kunionesha mahaba kwani alinifanya kama mtoto ndani ya nyumba na kunisahaulisha ubachela ambao niliutumikia kwa muda wa miaka 20 tangu niwe kijana.

Kilichonifanya nihamie kwa mwanamke mtu mzima ni jinsi mke wangu alivyoanza kubadilika siku hadi siku hasa baada ya siku arobaini za ndoa yetu.

Kumbe pale alikuja na mafunzo kutoka kwa mfundaji ambaye alimuweka ndani siku chache kabla ya kuolewa lakini haikuwa tabia yake kwani baada ya kukaa siku chahe alianza kunionesha tabia aliyolelewa nayo,” alisema mwanaume huyo aliyejitambulisha kwa jina la Adamu.

Nini umejifunza hapa?

Mwanamke mwenzangu unayenisoma hapa kisa cha mwanaume kuhamia kwa mwanamke mtu mzima ni kufuata matunzo ambayo awali alioneshwa na mke wake lakini baada ya hina kuisha akaanza visa na kutoa kucha zake.

Mke hatandiki kitanda mpaka saa sita.

Mwanaume huyo aliamua kuhama kisa mkewe mchafu. Hatandiki kitanda mpaka saa sita mchana au anashinda kitandani mume akirudi yeye ndiyo anamwambia ngoja nikung’ute ulale. Kwa nini asihame huyo kwa hali kama hiyo?

Nawaku-mbusha wanawake wenzangu, mwanaume hufuata kitu kidogo tu kwa mwanamke wa nje. Hebu jiimarishe kila idara uone kama ataondoka!  Lakini ukifanya siku za mwanzo ukaacha ni kama kumpa maziwa paka halafu siku zinazofuata ukampa chai, akienda kwa jirani akakuta maziwa atahamia hukohuko.

Wanafuata malezi, wanaume kwa wanawake watu wazima wanafuata malezi, kupendwa pia kwani wakifika huko hudekezwa kama wako kwa mama zao. Kwa nini wasihame sasa, kwani watu wazima wana tatizo gani?

Kama alishaumia huko nyuma na penzi limejileta lenyewe kwa nini asioneshe manjonjo? Msibweteke wanandoa, ‘utu uzima dawa’ jamani. Mwisho wa siku utabaki ukilalamika na kusema; ‘kwanza mwanamke mwenyewe kazeeka’ lakini nani alikwambia ng’ombe anazeeka maini?

Wapendwa mnaowapoteza wanaume kwa uzembe wenu hebu jiangalieni upya. Ndoa ni adimu siku hizi ukipata unashukuru tu.


Loading...

Toa comment