The House of Favourite Newspapers

Sababu za Beki Mzimbabwe Kutocheza Simba Hizi Hapa

0

KOCHA Mkuu wa Simba, Didier Gomes, amesema amefurahishwa na uwezo mzuri aliouonesha beki wake wa kati, Peter Muduhwa raia wa Zimbabwe, huku akitoa sababu zinazomfanya beki huyo kushindwa kupata nafasi ya kucheza ndani ya kikosi hicho tangu asajiliwe.

 

Muduhwa amesajiliwa na Simba maalum kwa ajili ya michuano ya kimataifa ambapo timu hiyo inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa hatua ya makundi.

 

Mzimbabwe huyo alitua Simba baada ya kumaliza majukumu yake katika timu ya taifa kwenye michuano ya CHAN iliyofanyika mapema mwaka huu nchini Cameroon.

 

Tangu asajiliwe, Muduhwa hajabahatika kucheza mechi yoyote ile ya kimataifa kati ya mbili dhidi ya AS Vita na Al Ahly.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Gomes alisema kuwa amefurahishwa na uwezo mkubwa aliouonesha beki huyo tangu atue Simba na mara kadhaa amekuwa akizungumza naye ili kumpa hali ya kujiamini zaidi.

 

Kocha huyo aliongeza kwamba, mkataba wake unambana kupata nafasi kutokana na kusajili maalum kwa michuano ya kimataifa pekee tofauti na wengine wanaocheza michuano yote.

 

“Muduhwa ni mchezaji mzuri sana, anatupa kitu bora sana mazoezini, ni bahati mbaya sana ana leseni ya kucheza Ligi ya Mabingwa pekee kwani angekuwa na leseni ya kucheza kwenye ligi na michuano mingine, naamini angepata nafasi ya kucheza ndani ya Simba.

 

“Huwa naongea naye ili kusaidia kumpa kujiamini zaidi, tayari kama benchi la ufundi tunaamini sana juu ya uwezo wake na tunaamini ni hazina kubwa na muhimu ndani ya klabu,” alisema kocha huyo.

 

Muduhwa amekosa nafasi ya kucheza mbele ya Joash Onyango, Erasto Nyoni na Pascal Wawa ambao wamekuwa wakicheza mara kwa mara.

Leave A Reply