The House of Favourite Newspapers

Sakata la Lissu, Mbowe Avishutumu Vyombo vya Dola

0
mwenyekiti wa chama cha demokrasia
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe akizungumza na waandishi wa habari
mwenyekiti wa chama cha demokrasia
…Akionyesha baadhi ya stakabadhi za matibabu ya Lissu ya nchini Kenya.

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe, amesema mtuhumiwa mkuu wa shambulio dhidi ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, ni vyombo vya ulinzi na usalama nchini.

Mbowe aliyasema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam ambapo alisisitiza kwamba shambulio hilo lilikuwa limelengwa dhidi ya chama chake, dhidi ya haki, dhidi ya ubinadamu na dhidi ya Watanzania kupitia mwili wa mbunge huyo.

“Suspect wetu namba moja katika tukio la Lissu ni vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi hii,” alisema Mbowe akiongeza kwamba viashiria vyote vya tukio hilo “tangu linatokea, kauli za viongozi, kusita kwa viongozi, kauli za kujiosha na mazuio yasiyokuwa na mantiki, mtu yeyote mwenye akili atasema vyombo hivyo vilihusika.”

Awali, kiongozi huyo aliyesema aliondoka Nairobi, Kenya, jana, aliwajulisha waandishi wa habari kwamba hali ya Lissu anayetibiwa jijini Nairobi inaendelea vizuri. “Watanzania msiwe na wasiwasi,” alisema Mbowe.

Akizidi kufafanua mkasa huo, Mbowe alitoa shukurani kwa madaktari wa Dodoma ambao walianza kumpatia matibabu ya awali, na pia madaktari wa Nairobi ambao wanaendelea naye hivi sasa, akisema walifanya kazi kubwa ya kuokoa maisha ya Lissu ambaye hali yake ilikuwa mbaya baada ya shambulio hilo. Vilevile alishutumu hatua ya kuchelewesha Sh milioni 43 zilizochangwa na wabunge kwa dharura kwa ajili ya kugharamia matibabu ya mbunge huyo.

“Fedha hizo hadi leo hazijafika,” alisema Mbowe akiongeza kwamba bado zinashikiliwa kwa nia zisizojulikana licha ya kwamba zilichangwa na wabunge akiwemo yeye. Mbowe pia alikanusha madai kwamba kuna mbunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyegharimia ndege iliyompeleka Lissu Nairobi, akisema hadi sasa gharama zote za matibabu za mbunge huyo zimebebwa na Chadema na watu wengine wa kawaida waliojitolea kusaidia. Pia aliishangaa hatua ya jana ya serikali ya kuwa tayari kugharimia matibabu hayo ambapo mwanzoni ilikataa kuyabeba.

“Bunge na serikali walikataa kugharimia matibabu haya tangu tukiwa Dodoma, tunashangaa hivi sasa wanasema wako tayari kumtibu mahali popote duniani, kwani Kenya siyo duniani? “ alisema.

Kuhusu uchunguzi wa tukio hilo, alisema ili kupata matokeo ya kweli ni lazima pawe na jopo la uchunguzi litakalokubalika na pande zote, akiongeza kwamba katika mazingira ya sasa hawana imani na uchunguzi kufanywa na upande mmoja.

Alitoa mifano ya kuuawa kwa mwanachama wao Alphonce Mawazo na kupotea kwa msaidizi wake, Ben Saanane, ambapo hadi leo hakuna uchunguzi wala matokeo yoyote yaliyowahi kutolewa na polisi na vyombo vingine vya usalama.

Lissu alishambuliwa na watu wasiojulikana hadi leo mjini Dodoma karibu wiki mbili zilizopita ambapo alipata majeraha mengi na makubwa kiasi cha kukimbizwa kwenda kupata matibabu Nairobi, Kenya, aliko hadi sasa.center;”>Mbowe Aipinga Vikali Serikali Sakata la Matibabu ya Tundu Lissu.

Mbowe Aipinga Serikali Sakata la Matibabu ya Lissu -Video

Leave A Reply