The House of Favourite Newspapers

Sakata la mchele wa Marekani lamuibua Waziri Bashe, Afunguka Mazito

0
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe

Serikali ya Tanzania imeitaka Taasisi inayofanya mradi wa kutoa misaada ya chakula ikiwemo mchele ulioongezewa virutubisho katika Shule mbalimbali Nchini, waiambie Marekani kwamba Tanzania kuna mchele na maharage kwahiyo zile fedha wanazowapa Wakulima wa Marekani wawape Wakulima wa Tanzania na virutubisho viongezwe hapa Nchini wakati Watanzania wakiwa wanaona.

Akiongea kwenye kongamano la kurasa 365 za Mama Vol 3 lililoandaliwa na Clouds Media Group Jijini Dar es salaam Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema “Mmeona jana na leo mitandaoni umeibuka mjadala mkubwa sana kuhusu Tanzania kupewa msaada wa chakula, ni NGO ndio inafanya ule mradi katika Shule za Msingi na Sekondari, sasa tumewaambia ile NGO wawaambie Wamarekani hivi mchele upo, maharage yapo kwenye Nchi hii kwahiyo zile fedha wanazowapa Wakulima wa Marekani wawape Wakulima wa Tanzania”

“Tununue huo mchele na maharage kutoka Tanzania halafu hivyo virutubisho mnavyotaka kuweka tuwekee hapahapa Tanzania wote tunawaona”

Kauli ya Bashe inakuja baada ya kuibuka kwa mjadala mtandaoni muda mfupi baada ya Ubalozi wa Marekani Nchini Tanzania kutoa taarifa iliyosema “Chini ya mpango wa ‘Pamoja Tuwalishe’, Wizara ya Kilimo ya Marekani, kwa ushirikiano na Jumuiya za Kimataifa, imetoa msaada wa kwanza wa mchele ulioongezwa virutubisho, maharage na mafuta ya alizeti kutoka kwa Wakulima wa Marekani moja kwa moja hadi Shuleni katika eneo la Dodoma Nchini Tanzania, zaid ya kutoa milo yenye lishe, Wanafunzi katika shule zaidi ya 300 zinazoshiriki, pia wataanzisha bustani za Shule, na kujifunza mbinu za kuvuna maji ya mvua, ikiwa ni mfano kamili unaoweza kuigwa, programu hii inaakisi ahadi na dhamira ya dhati ya Marekani ya kukuza afya, elimu, na fursa kwa Watoto kote Ulimwenguni”

Leave A Reply