The House of Favourite Newspapers

Sakata la Ofisa Ubalozi wa Syria Kushambuliwa Dar, Dereva Ahusishwa!

KAMANDA wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Jumanne Murilo, amesema kushambuliwa kwa ofisa wa ubalozi wa Syria nchini, Hassan Alfaouri (53) na kuibiwa Euro 93,000 ambazo ni sawa na Sh. mil. 251 za Kitanzania, ni mpango uliopangwa na dereva wake.

 

“Tukio hilo la  unyang’anyi kwa kutumia nondo lilifanyika kwa mhasibu wa ubalozi wa Syria, akiwa anatoka kwenye ubalozi huo kuelekea benki akiwa na dereva ambaye jeshi langu linamtafuta.  Dereva huyo aliacha kupita njia ya kuelekea mjini huku akiendesha gari polepole na baadaye kulisimamisha akidai limeharibika,” alisema Muliro na kuongeza:

 

“Mhasibu alivamiwa na watu watatu ambao wanatuhumiwa kuwa ni majambazi, walimjeruhi kwa kipande cha nondo kichwani, wakaondoka na dereva na gari la ubalozi na fedha hizo.”

 

Aliendelea kusema kuwa mara baada ya kupokelewa kwa taarifa hiyo katika kituo cha polisi msako mkali ulianza na kufanikiwa kulikamata gari hilo lililoondoka na watuhumiwa hao likiwa limetelekezwa eneo la Msasani Bonde la Mpunga.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa tukio hilo lilipangwa na baadhi ya wafanyakazi wa ubalozi wasio waaminifu akiwemo dereva huyo aliyetoroka ambaye wakati wa tukio zima la uporaji, hakuonyesha kutoa msaada wowote na alitoweka huku akiwaendesha watuhumiwa hao ambao wote wanatafutwa.

Gari la ubalozi wa Syria lililokutwa limetelekezwa eneo la Msasani, Bonde la Mpunga.

Wakati huohuo, Kamanda Muliro alisema jeshi lake limewakamata watuhumiwa watatu, Ramadhani Said, Jamilla Abdal na Muhidin Saidi wote wakazi wa Bunju, jijini Dar es Salaam, kwa kujihusisha na uuzajiwa madawa ya kulevya.

 

Comments are closed.